Thursday, June 27, 2013

FEDERER ASEMA BADO ATAENDELEA KUCHEZA MCHEZO HUO".

Mchezaji tenesi mahiri wa Switzerland, Roger Federer amesisitiza kuwa bado ataendelea kucheza mchezo huo kwa miaka mingi ijayo pamoja na kutolewa mapema katika michuano ya Wimbledon jana. Nyota huyo ambaye anashika namba tatu katika orodha za ubora duniani amesema hana hofu yoyote pamoja na kutolewa na Sergiy Stakhovisky wa Ukraine katika mzunguko wa pili wa michuano hiyo. Katika mchezo huo Federer aliburuzwa kwa kufungwa 6-7 7-6 7-5 7-6 na Stakhovsky anayeshika namba 116 katika orodha za ubora duniani. Baadhi ya wadau wa mchezo huo wamekuwa wakihoji kiwango cha Federer mwenye umri wa miaka 31 na kudai kuwa amekwisha lakini mwenye amesisitiza kuwa bado yuko fiti na ataendelea kucheza kwa miaka kadhaa ijayo. Kwa upande wa wanawake mwanadada nyota anayeshika namba mbili kwa ubora kwa upande wanawake Maria Sharapova wa Urusi naye aliyaaga mashindano hayo baada ya kukubali kipigo cha 6-3 6-4 kutoka kwa Michelle Larcher de Brito wa Ureno anayeshika namba 131 katika orodha hizo.

SCOLARI AMEKIRI KUWA TIMUYA BRAZIL BADO HAIKO FITI-DUNIA

KOCHA wa timu ya taifa ya Brazil, Luis Felipe Scolari amekiri kuwa kikosi chake bado hakiwezi kuanza kuweka matumaini ya kutwaa kombe lao la sita la Kombe la Dunia mwaka ujao lakini wamebakisha mechi moja kunyakuwa taji lao la tatu la Kombe la Shirikisho baada ya kuiengua Uruguay katika hatua ya nusu fainali. Scolari amesema anafikiri kikosi hicho kimefikia mahali pazuri lakini bado kuna vitu vingi vya kufanyia marekebisho mpaka kikamilike kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia mwakani. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa kwasasa wanahamishia nguvu zao katika mchezo wa fainali na baada ya hapo wataangalia mapungufu yalijitokeza ili kuhakikisha wanakuwa na kikosi imara kitakachoweza kulibakisha Kombe la Dunia nyumbani. Brazil kwasasa wanasubiri mshindi wa nusu fainali nyingine ya michuano hiyo itakayopigwa baadae leo kati ya mabingwa wa Ulaya na Dunia Hispania watakaochuana na Italia.

ABEL NA KISPANG WAJITOA TIMU YA WANARIADHA WA KENYA

BINGWA mara mbili wa dunia mashindano ya mbio ndefu Abel Kirui na mshindi wa medali ya shaba katika michuano ya olimpiki Wilson Kipsang wamejitoa katika timu ya wanariadha ya Kenya itakayoshiriki michuano ya riadha ya dunia itakayofanyika jijini Moscow. Makamu wa rais wa Chama cha Riadha cha nchi hiyo Paul Mutwii amedai kuwa Kurui aliwafahamisha kwamba amejitoa kwasababu ya kusumbuliwa na majeraha wakati Kipsang yeye amewaambia kuwa ana majukumu mengine. Kirui ambaye alishinda taji la dunia la mbio ndefu mwaka 2009 na 2011 amekuwa akisumbuliwa jeraha la kifundo cha mguu wake wa kulia na anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa kipindi cha wiki sita. Kuziba nafasi hizo Mutwii amesema wamewaita Mike Kipyego ambaye alishinda mbio za marathon jijini Tokyo mwaka jana, Bernard Kipyego mshindi wa medali ya fedha mbio za nusu marathon 2009 na bingwa wa mbio za marathoni za Paris Peter Some. Kikosi cha mwisho kitakachokwenda Moscow kitatajwa mwezi ujao baada ya kufanyika mbioza mchujo.

JUVESTUS YATANGAZA RASMI KUMSAJILI TEVEZ

KLABU ya Juventus ya Italia jana ilimtangaza rasmi kumsajili mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Argentina, Carlos Tevez kutoka timu ya Manchester City kwa mkataba wa miaka mitatu. Taarifa zinadai kuwa klabu yenye maskani yake katika jiji la Turin wamelipa kiasi cha paundi milioni 10 kwa nyota huyo mwenye umri wamiaka 29. Lakini Tevez atatakiwa kumaliza adhabu yake ya kutumikia jamii kwa saa 250 ili kuondoka jijini London salama na kuepuka kuburuzwa tena mahakamani. Tevez alikatisha likizo yake huko Amerika Kusini na kupanda ndege kuelekea Italia jana lakini pia atatakiwa kumaliza adhabu yake aliyopewa na mahakama ya Macclefield April mwaka huu kwa kuendesha huku akiwa amefungiwa kufanya hivyo.