Wednesday, May 7, 2014

MAMBO YAIVA,RAIS MPYA SIMBA SC KUPATIKANA JUNI 29

Kamati ya uchaguzi ya Simba imepanga uchaguzi mkuu wa klabu hiyo kufanyika juni 29 mwaka huu baada ya msajili wa vyama vya michezo na klabu kuipitisha katiba yao iliyofanyiwa marekebisho.
DSC_0027 Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Simba yalipopo mtaa wa Msimbazi Kariakoo, jijini Dar es salaam leo mchana, mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya Simba sc, mwanasheria na wakala wa wachezaji wa FIFA, Dkt. Damas Ndumbaro amesema kamati yake imekutana jana na kuamua tarehe hiyo ya uchaguzi ili kupata rais mpya, makamu wa rais na wajumbe wapya wa kamati ya utendaji.
“Kamati yangu ina watu makini na wenye uadilifu mkubwa. Pia wana mawazo ya kuijenga klabu ya Simba”.
“Jana tulikutana na kupanga ratiba ya uchaguzi. Hatutakuwa na huruma na watu watakaoenda kinyume na kanuni za uchaguzi”. Alisema Ndumbaro.

Ndumbaro alisema kuanzia mei 9 mwaka huu mchakato wa kuanza kutoa fomu kwa watu wenye nia ya kuwania nafasi za uongozi utaanza rasmi, na siku ya kurudisha fomu ni mei 14 mwaka huu.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA TASWA

WIKI iliyopita kulifanyika Mkutano Mkuu wa Chama cha Kimataifa cha Waandishi wa Habari za Michezo (AIPS) jijini Baku, Azerbaijan.
Mkutano huo ulishirikisha viongozi wa vyama 116 vya waandishi wa habari za michezo duniani, ambapo Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kiliwakilishwa na Katibu Mkuu, Amir Mhando.
 
amir-mhandoKatika mkutano huo msisitizo mkubwa umewekwa kwa nchi wanachama kutilia mkazo program za kuwaendeleza waandishi chipukizi wa habari za michezo, lakini pia AIPS yenyewe nayo pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Afrika (AIPS-Afrika) vimechukua jukumu la kusaidia kwa wale watakaokidhi vigezo wanavyohitaji.
 
Hivyo kila nchi mwanachama itatuma wasifu wa majina ya wanahabari chipukizi wasiozidi watano, ambao AIPS yenyewe itaangalia wale watakaofaa na kuwaandalia mafunzo baadaye mwaka huu.
 
Kwa upande wa AIPS Afrika yenyewe itaendesha mafunzo kwa wanahabari chipukizi 25, ambayo yatafanyika Morocco, lakini kipaumbele cha kwanza kitakuwa kwa nchi 16 zitakazocheza fainali za mataifa ya Afrika mwakani nchini humo na nafasi zingine zitabaki kwa nchi ambazo hazitaenda Morocco.
 
Mafunzo ni ya wazi kwa waandishi wowote chipukizi wasiozidi umri wa miaka 25, hata wale waliopo kwenye vyuo vya uandishi wa habari wataruhusiwa kuomba. Tanzania imewahi kupata nafasi moja mwaka 2011, ambapo Mwita Mwaikenda wakati huo akiwa mwanafunzo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alishiriki mafunzo hayo yaliyoandaliwa na AIPS akiwa miongoni mwa Waafrika watatu tu waliopata nafasi hiyo.
 
Utaratibu kuhusiana na suala hili utaelezwa vizuri baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya TASWA kitakachofanyika Jumatatu wiki ijayo kujadili masuala mbalimbali.
 
B: Ziara Uganda
Kulifanyika kikao cha viongozi wa nchi wanachama wa AIPS ambao wanatoka Afrika Mashariki, ambapo nchi za Burundi, Kenya, Tanzania na Uganda zilishiriki na kukubaliana kufanyike ziara ya kimafunzo itakayohusisha waaandishi wa habari za michezo Septemba 25-29 mwaka huu Kampala, Uganda. Rwanda licha ya kutoshiriki mkutano wa AIPS, lakini tulikubaliana nayo ialikwe.
Katika makubaliano hayo kila nchi itakuwa na washiriki wasiopungua 20 na wasiozidi 35, ambapo pia litafanyika kongamano kuhusiana na masuala mbalimbali ya waandishi wa habari za michezo kwa ukanda huo na siku ya mwisho litafanyika bonanza la michezo mbalimbali. Taarifa zaidi za ziara hiyo itatolewa siku za usoni.

C; Ushirikiano wa kimafunzo
 Baadhi ya nchi zilizoshiriki mkutano huo wa 77 wa AIPS, zilikubaliana kuanzisha utaratibu wa kubadilishana utaalamu wa kitaaluma kwa nchi mbalimbali, kwa kuwatoa baadhi ya wanahabari kwenda nchi zilizo katika makubaliano hayo kujifunza kwa gharama za nchi mwenyeji.
 
Hata hivyo makubaliano hayo, yataanza kufanya kazi baada ya kila nchi kupata baraka za Kamati ya Utendaji na kutuma majibu kwa waratibu kwamba wanaafiki. Kamati ya Utendaji ya TASWA katika kikao chake kijacho hilo litakuwa moja ya ajenda.

KINDA ANAEKIPIGA UJERUMANI AOMBA KUITWA STARS

Mwanandinga Kinda anayekipiga barani ulaya soka ya kulipwa Ujerumani, Charles Mishetto ameomba kuitwa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars aisaidie katika kampeni za kuing’oa Zimbabwe.
Hatua hiyo inakuja baada ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kuikubalia TP Mazembe ya DRC ambayo imegoma kuwaachia Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu kuitumikia Taifa Stars katika mechi ya kuwania kushiriki fainali zijazo za Afrika (AFCON) dhidi ya Zimbabwe.
FIFA imesema klabu hazitashurutishwa kuwaachilia wachezaji wao ili washiriki mechi za kufuzu kwa michuano hiyo itakayofanyika Morocco mwakani, kwa sababu ipo nje kalenda ya mechi za shirikisho hilo.
Boniface Wambura, Ofisa Habari na Mwasiliano wa  TFF amesema kuwa wawili hao hawatakuwamo kwenye kikosi cha kovha
mpya Mholanzi Mart Nooij kitakachoivaa Zimbabwe mwishoni mwa wiki ijayo kwa vile wanahitajika kwenye klabu yao.
Mechi za kuwania kufuzu AFCON zitafanyika Mei 16-18, tarehe ambayo haipo kwenye ratiba ya FIFA na kwa hivyo haitakuwa lazima wachezaji wa klabu kuruhusiwa kuondoka.
Hata hivyo, michuano ya makundi itakayoshirikisha Ghana, Nigeria na Cameroon, zitakuwa katika tarehe iliyoidhinishwa na FIFA , ikimaanisha kuwa klabu vya soka kote duniani lazima ziwaruhusu wachezaji wao kushiriki mechi hizo.
Mbali na Samata na Ulimwengu, wachezaji kama Edward Sadomba, wataathiriwa na mgongano wa tarehe zilizo kati ya mechi za kufuzu zitakazofanyika 2015 na michuano ya klabu. Sadomba atahitajika kwa wakati mmoja na klabu yake ya Al Ahli Benghazi pamoja na timu yake ya taifa Zimbabwe itakayokipiga dhidi ya Taifa Stars.
Lakini FIFA lilikaririwa na BBC juzi likieleza kuwa wachezaji wanaweza tu kuondoka ikiwa maafisa wa klabu na mashirikisho ya nchi husika wanaweza kukubaliana.