Meneja wa klabu ya Barcelona, Tito Vilanova ana nia ya kuendelea kuinoa klabu hiyo msimu ujao pamoja na athari za matibabu yake ya kansa ya koo na pia anaamini kuwa kikosi chake inaweza kuitoa Bayern Munich na kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Akihojiwa katika mkutano wake wa kwanza na waandishi toka alipotoka katika matibabu ya mionzi jijini New York mwezi mmoja uliopita, Vilanova amesema bado ana shauku kubwa na kuendelea na kazi yake na hakuna mara moja alipofikiria kuacha. Vilanova amesema madaktari kuwa kitu kizuri cha kufanya kwasasa ili kumsaidia kupona ni kufanya kazi na anafurahia jambo hilo. Kocha huyo pia mbali na timu yake kugaragazwa na Bayern kwa mabao 4-0 Jumanne iliyopita lakini ameonyesha kujiamini kwamba wachezaji wake wanauwezo wa kugeuza matokeo katika mchezo wa marudiano utakaopigwa katika Uwanja wa Camp Nou Jumatano ijayo. Vilanova amesema anaamini wachezaji wake wanaweza kufanya maajabu katika mchezo huo haswa ikizingatiwa watakuwa wakicheza mbele ya mashabiki wao ingawa amekiri itakuwa kazi ngumu kwani wapinzania wao nao hawataifanya kazi yao iwe rahisi.
MAKAMU wa rais wa klabu ya Santos ya Brazil, Odilio Rodriguez amebainisha kuwa Neymar ameiambia klabu hiyo kuwa yuko tayari kuondoka kwenda timu nyingine na hatarajii kusaini mkataba mwingine. Mkataba wa mshambuliaji huyo nyota unatarajiwa kuisha katika kipindi cha majira ya kiangazi mwaka 2014 na Santos walikuwa na nia ya kumbakisha kinda huyo mpaka baada ya michuano ya Kombe la Dunia 2014. Hatahivyo, Neymar mwenye umri wa miaka 21 ameweka wazi kuwa muda wake wa kuwepo Santos unakaribia kufikia mwishoni ambapo anataka kwenda kuonyesha ujuzi wake mahali pengine. Rodriquez alithibitisha hilo na tayari vilabu mbalimbali vikubwa barani Ulaya vimekuwa vikipigana vikumbo kutaka sahihi ya nyota huyo.
