Thursday, August 15, 2013

KANU ANAAMINI NCHI YAKE NIGERIA INA UWEZO MKUBWA"

Mshambuliaji wa zamani Arsenal, Nwankwo Kanu, anaamini Nchi yake Nigeria inao uwezo wa kufuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia huko Brazil Mwaka 2014 na pia kufanya vyema.
Kanu amesema lengo lao ni kutwaa Ubingwa wa Dunia Mwaka 2014 kwa ajili ya Afrika.
Hadi leo hakuna Nchi hata moja ya Afrika iliyoweza kutinga Nusu Fainali za Kombe la Dunia na katika Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2010 huko Nchini Afrika Kusini, Ghana ilikosa kidogo kuwa Nchi ya kwanza kuingia Nusu Fainali ilipofanyiwa ukatili na Luis Suarez pamoja na Uruguay yake.
Kanu, aliewahi kuzichezea Klabu za Portsmouth, Arsenal, Inter Milan na Ajax, anaamini Nigeria, ambao ndio Mabingwa wa Afrika, wanayo Timu imara na Benchi la Makocha mahiri ambalo linaweza kuiwezesha Nchi hiyo kufuzu kwenda Brazil na kuonyesha maajabu.
Kanu, mwenye Miaka 37, alisema: “Ni wazi tutafika Fainali za Kombe la Dunia Mwakani na tunataka kutwaa Kombe kwa ajili ya Afrika. Bado tuna Mechi na Malawi na tuko tayari na tutafanya kila tuwezalo.”
Baada ya kutwaa Ubingwa wa Afrika Mwezi Januari, Nigeria waliiwakilisha Afrika kwenye Mashindano ya FIFA ya Kombe la Mabara huko Brazil Mwezi Juni lakini waliishia hatua ya Makundi tu waliposhindwa kufuzu toka Kundi lao lililokuwa na Timu za Spain, Uruguay na Tahiti.
Ili kufika Fainali za Kombe la Dunia huko Brazil Mwaka 2014, Nigeria wanahitaji kutofungwa Mechi ya Nyumbani ya mwisho ya Kundi lao dhidi ya Malawi hapo Septemba 7 na kisha kuifunga Timu watakayopangiwa kwenye Raundi ya Mwisho ya Mtoano ambapo zitachezwa Mechi mbili za Nyumbani na Ugenini.
Wakati huo huo, hapo Jana huko Moses Mabhida Stadium Nchini Afrika Kusini, Nigeria waliwafunga Afrika Kusini Bao 2-0 na kutwaa Taji la Nelson Mandela Challenge huku Bao zote zikifungwa Kipindi cha Pili na Uche Nwofor alietokea Benchi.