Wednesday, April 10, 2013

KOCHA RHINO APIGWA FAINI, AFUNGIWA MECHI SITA
KAMATI ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imempiga faini ya sh. 400,000 na kumfungia mechi sita Kocha wa Rhino Rangers, Renatus Shija kwa kushiriki vitendo vinavyoashiria imani za ushirikina na kumdhihaki mwamuzi kwenye mechi za Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 31(1)(a) na (b) cha Kanuni za FDL ambapo Kocha huyo aliyeipandisha daraja Rhino Rangers kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) alifanya vitendo hivyo kwenye mechi mbili tofauti.

Mechi hizo ni kati ya Kanembwa JKT na Rhino Rangers iliyochezwa Februari 23 mwaka huu Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, na ile kati ya Rhino Rangers na Morani iliyochezwa Machi 17 mwaka huu Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Pia klabu ya Rhino Rangers imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na Polisi Wanajeshi- MP kuwapiga walinzi milangoni kwenye mechi hiyo dhidi ya Kanembwa JKT ili kupisha washabiki wa timu hiyo waingie bure uwanjani.

Mchezaji wa timu ya Pamba ya Mwanza, Leonard Nahole amepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi nne baada ya kumrushia chupa ya maji mwamuzi kwa madai amependelea kwenye mechi dhidi ya Polisi Tabora iliyochezwa Machi 16 mwaka huu.

Nao wachezaji Joseph Mapalala, Yohana Mirobo, Noel Makunja, Mkome Pastory na Rudenzi Kilinga wa Polisi Mara wamepigwa faini ya sh. 200,000 kila mmoja na kufungiwa mechi tatu kwa kufanya vitendo vinavyoshiria ushirikina na kumkimbiza mwamuzi kwenye mechi dhidi ya Morani iliyochezwa Machi 9 mwaka huu. Adhabu za wachezaji hao ni kwa mujibu wa kifungu cha 27(1)(g) cha Kanuni za FDL.

Klabu ya Villa Squad imepigwa faini ya sh. 150,000 kwa kuchelewa uwanjani kwenye mechi yake dhidi ya Ashanti United wakati Majimaji imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi dhidi ya Mbeya City iliyochezwa Uwanja wa Majimaji.

Vilevile Msimamizi wa Uwanja wa Majimaji aliyetambulika kwa jina moja la Mapunda aliwatukana waamuzi kwenye mechi hiyo, na suala lake litafikishwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya hatua za kinidhamu.

Pia uongozi wa Uwanja wa Mafinga unaotumiwa na timu ya daraja la kwanza ya Kurugenzi umetakiwa kuufanyia marekebisho, vinginevyo hautatumika kwa mechi za FDL msimu ujao.

MKUTANO WA WAANDISHI WA HABARI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kesho (Aprili 11 mwaka huu) litakuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari. Mkutano huo utafanyika saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF.
Boniface Wambura
Ofisa Habari

UEFA KUANZISHA ADHABU MPYA

SHIRIKISHO la Soka barani Ulaya-UEFA limepanga kuanzisha adhabu mpya kali ya kupambana na ubaguzi wa rangi ambap wachezaji watakaokutwa na hatia ya kufanya vitendo hivyo watafungiwa si chini mechi 10. Katika Mkuu wa UEFA Gianni Infantino amesema pia watafunga viwanja kwa muda viwanja ambavyo mashabiki wake watafanya tukio kama hilo kwa mara ya kwanza na kuufunga kabisa kama mashabiki wa timu husika watarudia tukio hilo kwa mara ya pili pamoja na faini ya fedha nyingi. Adhabu hizo mpya ambazo zilizungumziwa katika kikao cha kamati ya utendaji ya UEFA kilichokutana jana kitahusisha mechi zote za mashindano barani Ulaya. Infantino alifafanua kuwa kama mashabiki wa klabu fulani watakutwa na hatia ya kufanya vitendo hivyo basi upande wa uwanja uliohusika na tukio hilo utafungwa lakini kama tatizo ilikijirudia basi mashabiki wote watazuiwa kuingia uwanjani na kutozwa faini itakayofikia dola 65,300.

MCHEZA gofu namba moja duniani, Tiger Woods amesema yuko katika kiwango kizuri tayari kukata ukame wa miaka mitano kupita bila kushinda taji kubwa la Masters wiki hii. Woods ndio anapewa nafasi kubwa ya kunyakuwa zawadi ya Koti ya Bluu toka alipofanya hivyo mwaka 2005 na taji la kwanza kubwa toka mwaka 2008 baada ya kurejea kileleni mwa orodha ya wachezaji bora wa mchezo huo kwa kushinda mataji matatu mwaka huu. Nyota huyo alianguka mpaka katika nafasi ya 58 mwaka 2011 kufuatia kukumbwa na kashfa katika maisha yake binafsi na pia kusumbuliwa na majeruhi. Akihojiwa Woods mwenye umri wa miaka 37 amesema kwasasa anajisikia kurejesha makali yake ya zamani hivyo anategemea kufanya vizuri zaidi mwaka huu.