Friday, July 12, 2013

KAMPUNI YA MADUKA NCHINI BRAZIL WATISHIA KWENDA MAHAKANI KUHUSU USAJILI NEYMAR

Kampuni ya DIS inayomiliki maduka makubwa nchini Brazil na ambao wanamiliki asilimia 40 ya haki za usajili wa Neymar wametishia kwenda mahakamani kuhusiana na mgao wao kwa nyota huyaa o katika usajili wake kwenda Barcelona. Kampuni hiyo inayoendeshwa na Idi Sonda imedai kuwa na haki ya kupata fedha zaidi juu ya makubaliano ya ziada kati ya klabu ya Santos na Barcelona ambayo yako nje ya ada ya uhamisho wake ambayo ilifikia kiasi cha euro milioni 57. Mkurugenzi Mtendaji wa DIS, Roberto Moreno ameomba kupewa taarifa kamili ya hati ya uhamisho wa Neymar kwenda Barcelona ili kupata ufafanuzi kuhusu malipo ya baadae watakayopewa Santos. Moreno amesema mpaka kipindi hicho hawajaonyeshwa hati yoyote, hivyo atafunga safari kwenda makao makuu ya Santos kufuatilia hati hiyo na baada ya hapo wataamua kama watahitaji kwenda mahamani. Hatua ya kampuni hiyo imekuja kufuatia taarifa zilitolewa na vyombo vya habari nchini humo kwamba Santos watapata nyongeza ya euro milioni mbili kama mchezaji huyo atakuwemo katika orodha ya wachezaji watatu kwenye tuzo ya Ballon d’Or kwenye kipindi cha miaka mitano ijayo.

FIFA YA FUATILIA KWA KARIBU KASHFA YA UPANGAJI MATOKEO

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA linafuatilia kwa karibu kashfa ya upangaji matokeo inayozikabili vilabu viwili vya soka vya ridhaa nchini Nigeria iliyotokea wiki iliyopita. Katika matokeo ambayo yanaonekana kama ya mchezo wa kriketi, klabu ya Plateau United Feeders iliibugiza Akurba FC kwa mabao 79-0 wakati Police Machine wao waliitandika Bubayaro FC kwa mabao 67-0 mwishoni mwa wiki iliyopita. Hatua uchunguzi kwa vilabu hivyo imekuja kutokana na timu hizo kuhitaji matokeo ya aina hiyo ili waweze kupanda daraja. Ambapo katika taarifa yake FIFA imedai kuwa inafuatilia tukio hilo la tmu hizo za Nigeria kwa karibu ili kuona jinsi gani Shirikisho la Soka la nchi hiyo, NFF litatatua tatizo hilo. FIFA inafanya hivyo kwa kutambua kuwa suala hilo ni la ndani hivyo NFF ina wajibu wa kufanya uchunguzi na kuchukua hatua zinazostahiki kama ikigundulika aina yoyote ya udanganyifu katika mechi hizo.

TAIFA STARS SASA MMEIVA KUPAMBANA- TENGA

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema kikosi cha Taifa Stars sasa kina uwezo wa kushindana katika mashindano yoyote, kwani tayari kimeiva.
Akizungumza na wachezaji wa timu hiyo kambini kwao hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam, Rais Tenga aliwaambia kuwa kiwango walichoonesha kwenye mechi zilizopita za mchujo za Kombe la Dunia dhidi ya Morocco na Ivory Coast kimethibitisha hilo.
“Kiwango mlichoonyesha katika mechi hizo kila Mtanzania anayewafuatilia amekiona, hivyo hatuna shaka kuwa mtatuwakilisha vizuri kwenye mechi ya kesho dhidi ya Uganda,” amesema Rais Tenga na kuwataka kupigana kwa ajili ya Tanzania.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kesho (Julai 13 mwaka huu) saa 9 kamili alasiri Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itacheza na Uganda (The Cranes) katika mechi ya kwanza ya raundi ya mwisho kuwania tiketi ya kucheza Fainali za CHAN zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Rais Tenga amesema TFF, mdhamini Kilimanjaro Premium Lager, Kamati ya Ushindi na Watanzania kwa ujumla wanawaunga mkono kwani wamekuwa wakiboresha kiwango chao kila wanavyozidi kucheza mechi tangu wake chini ya Kocha Kim Poulsen, Mei mwaka jana.
Wakati huo huo, Rais Tenga ameahidi kumpatia tiketi ya kwenda Uganda kwenye mechi ya marudiano mshabiki Wiseman Mwakyusa Luvanda anayetembea kwa miguu kutoka Mbeya kuja Dar es Salaam kushuhudia mechi ya kesho.
“Kama ni kweli anakuja kwa kutembea, huyu ameonyesha kiwango kikubwa cha uzalendo kwa timu ya Taifa, nitampatia tiketi ya kwenda Kampala kuishangilia Taifa Stars kwenye mechi ya marudiano,” amesema Rais Tenga.

POULSEN, MICHO WATABIRI MECHI KALI
Makocha wa timu hizo Kim Poulsen wa Taifa Stars na Sredojvic Micho wa The Cranes wamesema mechi ya kesho itakuwa ngumu kwa vile kila mmoja amejiandaa kuhakikisha anafanya vizuri.

Wakizungumza na Waandishi wa Habari leo, makocha wote waliezea ubora wa wapinzani wao, lakini wakasisitiza kuwa wanaingia uwanjani kuhakikisha wanashinda ili kujiweka katika mazingira mazuri kwa ajili ya mechi ya marudiano itakayochezwa Kampala wiki mbili zijazo.
Kim alisema Uganda ndiyo inayoongoza kwa ubora wa viwango vya FIFA katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, hivyo ni changamoto kwao ingawa wachezaji wake tayari wamejipanga vizuri kwa ajili ya mechi hiyo.
Naye Micho aliyefuatana na nahodha wake Hassan Wasswa alisema Taifa Stars imekuwa ikifanya vizuri tangu iwe chini ya Kim, na itakuwa na wachezaji tisa wa kikosi cha kwanza kinachocheza mechi za mchujo za Kombe la Dunia wakati kwa upande wake atakuwa na wachezaji wawili tu.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)