WACHEZAJI wawili waliochaguliwa
kwenda kwenye kambi ya Copa Coca-Cola ya Dunia nchini Brazil wamekabidhiwa
bendera tayari kwa safari hiyo inayofanyika leo (Juni 4 mwaka huu).
Hafla ya kukabidhi bendera hiyo kwa
Ali Shabani Mabuyu na Juma Yusuf imefanyika leo katika hoteli ya
Hyatt Regency
jijini Dar es Salaam. Naibu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo katika Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juliana Yassoda ndiye alikabidhi bendera.
Wakati Mabuyu kutoka Ilala
alikuwa mchezaji bora wa michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini
ya miaka 15 kwa mwaka 2013/2014, Yusuf kutoka Zanzibar ndiye aliyeibuka
mfungaji bora katika michuano hiyo.
Wachezaji
hao watakuwa katika kambi hiyo itakayokuwa katika Jiji la Sao Paulo kwa siku
kumi ambapo watafundishwa masuala mbalimbali ya mpira wa miguu. Pia
watashuhudia mechi ya ufunguzi ya Fainali za Kombe la Dunia katika ya wenyeji
Brazil na Croatia itakayochezwa Juni 12 mwaka huu.