Mafunzo hayo ambayo yanafanywa na mkufunzi kutoka Chama cha Makocha Tanzania (Tafca), George Komba, yanafadhiliwa na Chama cha Makocha Mkoa wa Rukwa, ambako yatakuwa ya siku 12, yakishirikisha washiriki kutoka wilaya zote mkoani hapa.
Akizungumza na mwandishi wa blog hii Katibu wa Tafca Rukwa, Lusungu Kihaha ameeleza kuwa lengo ni kuwanoa makocha hao ili waweze kuzielewa kwa kina kanuni zote 17 za soka.
Ameongeza na kusema kuwa ni matarajio yake ifikapo 2013-14 kuona soka la kistaarabu likichezwa viwanjani, kwani mpira wa miguu si uwanja wa vita, bali ni kuboresha mahusiano baina ya wachezaji, pia makocha na makocha wenzao.
Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Rukwa (Rurefa), Godfrey Seko, alisema kuwa mara baada ya mafunzo hayo, hakuna kocha yeyote asiye na sifa atakayeruhusiwa kuketi katika benchi la ufundi kiwanjani wakati timu yake ikicheza.
Aidha amesema ni makocha wale tu wenye cheti cha awali, ndio watakaoruhusiwa kuketi kwenye benchi la ufundi wakati timu zao zikiumana na si vinginevyo.
hata hivyo Awali akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Sumbawanga, Kevas Masawe, amewataka washiriki hao kuutumia ujuzi huo shuleni na katika timu za mitaani ili kuinua vipaji vya soka vya Mkoa wa Rukwa.