Mshambuliaji wa zamani Arsenal, Nwankwo Kanu,
anaamini Nchi yake Nigeria inao uwezo wa kufuzu kucheza Fainali za
Kombe la Dunia huko Brazil Mwaka 2014 na pia kufanya vyema.
Kanu amesema lengo lao ni kutwaa Ubingwa wa Dunia Mwaka 2014 kwa ajili ya Afrika.
Hadi leo hakuna Nchi hata moja ya Afrika
iliyoweza kutinga Nusu Fainali za Kombe la Dunia na katika Fainali za
Kombe la Dunia za Mwaka 2010 huko Nchini Afrika Kusini, Ghana ilikosa
kidogo kuwa Nchi ya kwanza kuingia Nusu Fainali ilipofanyiwa ukatili na
Luis Suarez pamoja na Uruguay yake.
Kanu,
aliewahi kuzichezea Klabu za Portsmouth, Arsenal, Inter Milan na Ajax,
anaamini Nigeria, ambao ndio Mabingwa wa Afrika, wanayo Timu imara na
Benchi la Makocha mahiri ambalo linaweza kuiwezesha Nchi hiyo kufuzu
kwenda Brazil na kuonyesha maajabu.
Kanu,
mwenye Miaka 37, alisema: “Ni wazi tutafika Fainali za Kombe la Dunia
Mwakani na tunataka kutwaa Kombe kwa ajili ya Afrika. Bado tuna Mechi na
Malawi na tuko tayari na tutafanya kila tuwezalo.”
Baada
ya kutwaa Ubingwa wa Afrika Mwezi Januari, Nigeria waliiwakilisha
Afrika kwenye Mashindano ya FIFA ya Kombe la Mabara huko Brazil Mwezi
Juni lakini waliishia hatua ya Makundi tu waliposhindwa kufuzu toka
Kundi lao lililokuwa na Timu za Spain, Uruguay na Tahiti.
Ili kufika Fainali za Kombe la Dunia
huko Brazil Mwaka 2014, Nigeria wanahitaji kutofungwa Mechi ya Nyumbani
ya mwisho ya Kundi lao dhidi ya Malawi hapo Septemba 7 na kisha kuifunga
Timu watakayopangiwa kwenye Raundi ya Mwisho ya Mtoano ambapo
zitachezwa Mechi mbili za Nyumbani na Ugenini.
Wakati
huo huo, hapo Jana huko Moses Mabhida Stadium Nchini Afrika Kusini,
Nigeria waliwafunga Afrika Kusini Bao 2-0 na kutwaa Taji la Nelson
Mandela Challenge huku Bao zote zikifungwa Kipindi cha Pili na Uche
Nwofor alietokea Benchi.