Sunday, July 21, 2013

KIPA MARK MPYA WA CHELSEA AWEKA WAZI KUPIGANIA NAMBA NDANI YA CLUB HIYO"

Golikipa mkongwe aliyenaswa na club ya Chelsea katika kipindi cha usajili wa majira ya kiangazi, Mark Schwarzer ameibuka na kudai kuwa anapigania kupata namba katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo msimu ujao. Akihojiwa na waandishi wa habari katika ziara ya kujiandaa na msimu mpya ya klabu hiyo jijini Kuala Lumpur, Malaysia, Schwarzer amesema wakati akisajiliwa na timu hiyo alijua kwamba wana makipa bora na mpambano wa kutafuta nafasi ya kuanza utakuwa mgumu. Lakini alidai kuwa kwa juhudi na kiwango kizuri atakachoonyesha ana matumaini anaweza kupangwa katika kikosi cha kwanza timu hiyo msimu ujao. 
Meneja wa Chelsea Jose Mourinho amesema wiki iliyopita kuwa Schwarzer ataleta ushindani na hamasa kwa golikipa namba moja wa klabu hiyo Petr Cech baada ya kufanya usajili huo wa kushangaza. Schwarzer ambaye amecheza katika Ligi Kuu nchini Uingereza kwa zaidi ya miaka 15 ni mmoja ya wachezaji wachache waliocheza mechi zaidi ya 500 katika historia ya ligi hiyo.

YANGA LEO YAJITOA KIMASOMASO MBELE YA URA YA UGANDA 2-2

Club ya Yanga jioni ya leo katika Dimba la Uwanja wa Taifa  Taifa Jijini DAR kukabiliana na Timu ya inayo milikiwa na Mamlaka ya Mapato ya nchini Uganda URA kwa mchezo wa kirafiki uliomalizika kwa sare ya bao 2-2.
Sare hiyo haikuwa nyepesi, kwani mabingwa wa Tanzania Bara walilazimika kuhaha kusaka mabao ya kusawazisha hadi walipojitoa uwanjani salama dakika ya 90 kwa bao la Jerry Tegete.
Katika mchezo huo, uliochezeshwa na refa Kennedy Mapunda aliyesaidiwa na Iddi Maganga na Othman Othman, hadi mapumziko URA tayari walikuwa mbele mkwa bao 1-0.
Bao hilo lilifungwa dakika ya 42 na Litumba Yayo, ambaye jana Watoza Kodi hao wa Uganda wakiilaza Simba SC 2-1, alifunga mabao yote.
Kipindi cha kwanza URA ndio waliotawala mchezo kwa kucheza kwa kasi nzuri, uelewano mzuri na kushambulia kwa nguvu, wakati Yanga SC walionekana kukosa mipango.
Kipindi cha pili, URA walianza tena vyema na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 61, mfungaji Yayo tena akiweka rekodi ya kufunga mabao manne Taifa ndani ya siku mbili.
Kocha Mholanzi, Ernie Brandts alilazimika kufanya mabadiliko baada ya bao hilo, akiwaingiza Haruna Niyonzima kuchukua nafasi ya Said Bahanuzi wingi ya kulia, Bakari Masoud kuchukua nafasi ya Hamisi Thabit na Abdallah Mnguli ‘Messi’ kuchukua nafasi ya Shaaban Kondo.
Mabadiliko hayo yaliisaidia Yanga SC ambayo iliongeza kasi ya mashambulizi na kufanikiwa kuchomoa mabao yote, moja baada ya lingine.
Mrundi Didier Kavumbangu alianza dakika ya 66 akiunganisha krosi ya beki Juma Abdul kabla ya Tegete kusawazisha dakika ya 90 baada ya kumzidi maarifa kipa wa URA, Yassin Mugabi.
Tegete ambaye ana muda mrefu hajaifungia bao Yanga, alipagawa mno kwa kufunga bao muhimu leo na kwenda kushangilia mbele ya mashabiki kwa ishara mbili- kuomba msamaha na pili kuwaambia anaipenda Yanga kwa kuibusu nembo ya klabu iliyopo kwenye jezi sambamba na kuwapa ishara ya kuwataka watulie, mpira hauhitaji papara. 
MSHAMBULIAJI Mniegria wa Yanga, Ogbu Brendan Chukwudi aliondolewa ghafla katika kikosi cha kwanza cha Yanga baada ya kuumia wakati akipasha misuli moto kujianda kuingia mchezoni dhidi ya URA ya Uganda, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni hii.
Kocha Mholanzi, Ernie Brandts alimuondoa kabisa Chukwudi katika orodha ya wachezaji wanaoshiriki mechi ya leo na kumuanzisha Mrundi, Didier
Kikosi cha Yanga SC leo kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Ibrahim Job, Rajab Zahir 14, Salim Telela 2, Said Bahanuzi/Niyo, Hamisi Thabit 28/Bakari Masoud, Jerry Tegete, Didier Kavumbangu na Shaaban Kondo18/Abdallah Mguli.



ASHANTI UNITED YAJIPANGA KWA ZIARA YA KIGOMA

Timu ya Ashanti United iliyopanga ligi kuu msimu huu inatarajiwa kufanya ziara mkoani Kigoma, maarufu kama Brazil ya Tanzania kujiandaa na msimu, mara tu baada ya kurejea Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Kigoma inaitwa Brazil ya Tanzania kwa sababu ya kuibua nyota wengi wa soka, kuanzia enzi za akina Sunday Manara, Athumani Juma Kalomba (marehemu), Abedi Mziba, hadi sasa akia Juma Kaseja.
Ashanti itaondoka Dar es Salaam Jumanne na itakuwa Kigoma kwa takriban wiki mbili ikijifua na kucheza mechi za kujipima nguvu na timu mbalimbali za huko.
Timu hiyo iliyorejea Ligi Kuu msimu huu, imekuwa ikijifua mjini Dar es Salaam kwa takriban mwezi mzima na kucheza mechi kadhaa za kujipima nguvu.

Mechi ya mwisho ilifungwa na Azam FC mabao 5-1 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam na sasa inakwenda kurekebisha makosa Kigoma.
Ashanti inakumbukwa enzi zake ikicheza Ligi Kuu muongo uliopita kwa kuibua vipaji vya nyota wengi ambao baadaye walikuwa tegemeo la timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Miongoni mwao ni kipa Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Juma Jabu, Juma Nyosso, Said Mourad, viungo Jabir Aziz, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ na wengineo.
Timu hiyo yenye maskani yake katika soko la Ilala Boma, karibu kabisa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam inatarajiwa kuleta changamoto mpya katika Ligi Kuu, hususan dhidi ya timu kongwe, Simba na Yanga.
Pamoja na kupandishwa Ligi Kuu na vijana wadogo wenye vipaji, Ashanti imejiimarisha kwa kuongeza wakongwe kadhaa, akiwemo mshambuliaji wa zamani wa Simba na Yanga, Said Maulid ‘SMG’ aliyekuwa anacheza Angola.

WAGOSI WA KAYA WAJIPANGA NA MECHI YA KIRAFIKI VS URA YA UGANDA

TIMU ya Wagosi wa wakaya Coastal Union ya Tanga Mabingwa ya ligi kuu mnamo mwaka 1988 inataraji kushuka dimbani kucheza mechi ya Kirafiki ya Kimataifa na Mabingwa wa soka Uganda URA Jumatano wiki ijayo kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani mkoani Tanga.
Athibtisha taarifa hizo,Mwenyekiti wa timu hiyo,Hemed Aurora "Mpiganaji"alisema ni kweli mechi hiyo ipo na kinachofanyika hivi sasa ni kufanya mazungumzo ya mwisho na uongozi wa timu hiyo ili iweze kutua mkoani hapa kwa ajili ya mchezo huo.
Aurora alisema baada ya kumalizika mechi hiyo kikosi cha timu hiyo kitaondoka mkoani Tanga kuelekea Mombasa nchini Kenya kucheza mechi ya kirafiki na timu ya Bandari lengo likiwa ni kukiimarisha kikosi hicho kabla ya kuanza msimu mpya wa Ligi kuu.
Licha ya kucheza na Bandari lakini pia wapo kwenye mikakati ya kuzungumza na uongozi wa Yanga ili kuweza kucheza nao mechi ya majaribio siku ya Iddi Pili kwenye dimba hilo la Mkwakwani ambapo alisema anaamini mazungumzo hayo yatafanikiwa.

Mwenyekiti huyo amebainisha kuwa lengo la timu hiyo msimu ujao ni kuhakikisha wanafanya vizuri ili kuweza kurudisha heshima yao ya mwaka 1988 ya kuchukua ubingwa wa Ligi hiyo na kueleza hilo linawezekana kutokana na mshikamano uliopo baina ya wapenzi,wanachama na uongozi wao.
Akizungumzia maandalizi ya mechi hiyo ,Meneja wa uwanja wa CCM Mkwakwani,Mbwana Msumari alisema kwa mara ya mwisho uwanja huo kulichezwa mechi ya kimataifa mwaka 1988 kati ya African Sports na timu kutoka nchini Swithland wakati huo African Sports ni mabingwa wa Kombe la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Msumari alisema na mwaka huo huo ,Coastal Union wakacheza na Cost De Solver ya Msumbuji ambayo ilikuwa ikishiriki mashindano ya Klabu bingwa kwa hiyo anaamini mechi hiyo itakuwa na mvuto wa aina yake kutokana na historia ya timu hiyo.

NAPOLI YATANGAZA KUMSAJILI BEKI WA MADRID YA HISPANIA RAUL ALBIOL

Club ya Napoli ya nchin Italia imetangaza kumsajili beki mahiri wa klabu ya Real Madrid ya Hispania Raul Albiol. Katika taarifa iliyotumwa katika mtandao wa klabu hiyo imeeleza kuwa beki huyo wa kati mwenye umri wa miaka 27 amesajiliwa kwa mkataba wa miaka minne ambapo taarifa hiyo haikufafanua thamani halisi waliyomnunulia mchezaji huyo. 
Napoli kwasasaiajipanga kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu nchini Italia na Ligi ya Mabingwa Ulaya huku wakiwa na fedha za kutosha kutumia baada ya kumuuza mshambuliaji wa kimataifa wa Uruguay Edinson Cavani kwenda Paris Saint Germain kwa ada ya euro milioni 64. Albion ambaye ametoka katika shule ya soka ya Valencia akiwa kama mchezaji wa kiungo aliibuka katika kikosi cha kwanza cha klabu hiyo mwaka 2003 wakati huo ikifundishwa na kocha wa mpya wa Napoli Rafa Benitez kabla ya kuhamia Madrid mwaka 2009 ambako muda mwingi alitumika kama mchezaji wa akiba. Pamoja na kukosa namba klabuni kwake alifanikiwa kupata nafasi katika kikosi cha timu ya taifa ya Hispania katika michuano ya Kombe la Dunia 2010 na michuano ya Ulaya mwaka jana.

CAF YATEU MUAMUZI KUTOKA MADAGASCAR KUCHEZESHA MECHI KATI YA TANZANIA VS UGANDA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Madagascar kuchezesha mechi kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Uganda (The Cranes) itakayochezwa Jumamosi (Julai 27 mwaka huu) Uwanja wa Mandela ulioko Namboole nje kidogo ya Jiji la Kampala. Waamuzi wataongozwa na Kanoso Abdoul Ohabee wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Andirvoavonjy Pierre Jean Eric. Mwamuzi msaidizi namba mbili ni Jinoro Velomanana Ferdinand huku Andriamiharisoa Hubert Marie Bruno akiwa mwamuzi wa mezani (fourth official). Kamishna wa mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya mwisho kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) ni Ismail Kamal kutoka Ethiopia. Mechi hiyo namba 38 itachezwa kuanzia saa 10 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki. Taifa Stars ilipoteza mechi ya kwanza iliyochezwa Julai 13 mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa bao 1-0. Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iko kambini jijini Mwanza ikijiandaa kwa mechi hiyo itakayoamua ni timu ipi kati ya hizo mbili itacheza Fainali za CHAN mwakani nchini Afrika Kusini.