Thursday, May 23, 2013

CITY YAKANUSHA KUWAWINDA FALCAO NA NEYMAR

NEYMAR_THE_BRAZILIAN
MKURUGENZI MKUU wa Manchester City chief Ferran Soriano amekanusha taarifa kuwa wanahaha kuwasaini Masupastaa Radamel Falcao na Neymar.
Hivi karibuni kumezagaa ripoti kuwa Man City ni miongoni mwa Klabu zinazokimbiza saini za Straika wa Atletico Madrid, Radamel Falcao, na yule wa Santos ya Brazil, Neymar.
Falcao anawindwa na msululu wa Klabu zikiwemo Chelsea, Monaco na Real Madrid baada ya kung’ara sana kwa kuifungia Atletico Mabao muhimu kwa Misimu kadhaa.
Nae Neymar, anaewindwa na Klabu kubwa Barani Ulaya, anatarajiwa kuihama Brazil baada ya Nchi hiyo kuwa Mwenyeji wa Kombe la Dunia Mwaka 2014.
Hata hivyo, Soriano amekanusha kwa kutamka: “Neymar na Falcao? Habari hizo ni uongo, hawajawahi kuwa kwenye ajenda yetu!”
Vile vile, Soriano aliponda habari kuwa wanataka kumuuza Straika wao mahiri Serio Aguero, mwenye Miaka 24, huku Real Madrid ikitajwa kuwa ndio atatua.
Soriano amesisitiza: “Hatujawahi kufikiria kumuuza Aguero. El Kun ana furaha kubaki kwetu Mwaka huu!”

MESSI AFURAHIA KUVAA JEZI NAMBA 10 AKIWA KATIKA TIMU HIYO.

MSHAMBULIAJI nyota maarufu dunia wa klabu ya Barcelona Lionel Messi amesema anajisikia raha na heshima kubwa kuvaa jezi namba 10 akiwa katika klabu hiyo na kufuata nyayo za Ronaldinho na nyota wengine waliokuwa wakivaa jezi hiyo. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina alirithi namba ya jezi ya Ronaldinho wakati nyota huyo wa Brazil alipoondoka Barcelona kwenda AC Milan katika kipindi cha majira ya kiangazi mwaka 2008 na kudai kuwa ilikuwa na maana kubwa kwake wakati anaanza kuivaa. Messi amesema wakati anapewa jezi hiyo namba 10 alijisikia furaha kwa ni jezi ambayo imekuwa ikivaliwa na wachezaji waliofanya mambo makubwa katika klabu hiyo. Nyota huyo pia alielezea nia yake ya kutaka kuiongoza timu ya taifa ya nchi yake kunyakuwa Kombe la Dunia huku akitaka mataji zaidi katika klabu yake ya Barcelona.

MOURINHO PAMOJA NA RONALDO WAFUNGIWA MECHI 2.

Kocha wa Real madrid Jose Mourinho pamoja na nyota wa klabu hiyo Cristiano Ronaldo wamefungiwa mechi mbili za michuano ya Kombe la Mfalme baada ya kutolewa nje katika fainali dhidi ya Atletico Madrid. Mourinho mwenye umri wa miaka 50 alitolewa nje baada ya kumshambulia mwamuzi kwa maamuzi aliyotoa adhabu ambayo hataweza kuitumikia baada ya kutangaza kuondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu huu. Ronaldo mwenye umri wa miaka 28 alipewa kadi nyekundu baada kukutwa na hatia ya kumpiga teke la uso kwa makusudi mchezaji wa Atletico, Gabi. Wote wawili Ronaldo na Mourinho watakuwepo katika michezo miwili ya mwisho ya ligi ya Madrid.

TIMU YA TAIFA YA CAMEROON YAPATA KOCHA MPYA.

Timu ya taifa ya Cameroon imefanikiwa kupata kocha mpya  Volker Finke kuwa kocha mkuu wa timu hiyo huku kibarua chake cha kwanza Mjerumani huyo ni kuhakikisha timu hiyo inafuzu michuano ya Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil. Finke anachukua nafasi ya kocha wa muda wa timu hiyo Jean-Paul Akono ambaye aliwekwa hapo kuziba nafasi ya Denis Lavagne Septemba mwaka jana baada ya Mfaransa huyo kushindwa kuisaidia timu hiyo kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika 2012 na 2013. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 65 aliwahi kuifundisha klabu ya SC Freiburg kuanzia mwak 1991 mpaka 2007 na atakuwa anafundisha kikosi cha timu ya taifa kwa mara ya kwanza baada ya kutemwa na timu ya Urawa Red Diamonds ya Japan na timu ya Cologne ya nchini kwake. Katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia, Cameroon wako kileleni mwa kundi I wakiwa na alama sita katika mechi tatu walizocheza wakifuatiwa na Libya wenye alama tano, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo-DRC alama nne na Togo alama moja. Kazi yake ya kwanza Finke itakuwa ni kukiongoza kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Ukraine utakaochezwa jijini Kiev Juni 2 mwaka huu kabla ya kuhamishia nguvu zao katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Togo Juni 9, DRC Juni 16 na Libya Septemba 6 mwaka huu

CLUB YA SANTOS YAKATAA OFA YA PILI YA BARCA

MAKAMU wa rais wa klabu ya Santos ya Brazil, Odilio Rodrigues amedai kwamba wamekataa ofa ya klabu ya Barcelona ya Hispania kutaka kumsajili mshambuliaji wao nyota Neymar kwa mara ya pili. Katika siku za hivi karibuni Barcelona ndiyo pekee wameonyesha nia ya kumhitaji mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Brazil na kuripoti kuwa walitaka kuwapa Santos euro milioni 20 ili waweze kumiliki haki za mchezaji huyo kwa asilimia 55. Wakati mahasimu wao nao Real madrid wakiongeza mbio ya kumfukuzia mshambuliaji huyo, Barcelona walitoa kiasi hicho ili waweze kumaliza suala hilo lakini Rodrigues amesisitiza kuwa hawana haraka ya kumuuza Neymar kwa kiasi kidogo kuliko wanachotaka. Rodrigues alithibitisha kuwa ni kweli walipata ofa ya Barcelona kwa mara ya pili lakini waliikataa kwasababu hawakufikia kiwango walichokuwa wakikihitaji. Neymar katika siku karibu ameweka wazi nia yake ya kubakia Santos mpaka baada ya michuano ya Kombe la Dunia 2014, ingawa uhamisho wa kwenda barani Ulaya katika kipindi hiki cha usajili unaonekana kama unaweza kuwepo.

FA CHADAI KUWA CARROL AJITOA TIMU YA TAIFA KUTOKANA NA MAJERUHI.

CHAMA cha Soka nchini Uingereza {FA} kimedai kuwa mshambuliaji wa kimataifa wa nchi hiyo, Andy Carroll amejitoa katika timu ya taifa kutokana na kuwa majeruhi. Carroll mwenye umri wa miaka 24 amekuwa akisumbuliwa na maumivu ya kisigino baada ya kocha wa timu ya taifa Roy Hodgson kumuita katika kikosi chake ambacho kitacheza mechi mbili za kimataifa za kirafiki kati ya Ireland Mei 29 na Brazil Juni 2 katika Uwanja wa Maracana jijini Rio de Janeiro. Mshambuliaji huyo wa Liverpool amekuwa akicheza kwa mkopo katika klabu ya West Ham United msimu uliopita huku vyombo vya habari nchini Uingereza vikiripoti kuwa klabu hiyo imekubali kumchukua moja kwa moja kwa ada ya paundi milioni 15. Carroll anaungana na nahodha wa Liverpool Steven Gerrard na kiungo wa Arsenal Jack Wilshere kukosa mechi hizo za kujipima nguvu kabla ya mechi za kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2014 dhidi ya Moldova na Ukraine Septemba mwaka huu.

KOCHA WA LIVERPOOL RODGERS HANA MPANGO WA KUMUUZA SUAREZ.

BOSI wa  majogoo wa jiji la londo Liverpool Brendan Rodgers amesema hana mpango wa kumuuza mshambuliaji nyota wa klabu hiyo Luis Suarez. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uruguay alikosa mechi nne za Liverpool mwishoni mwa msimu huu baada ya kufungiwa mechi 10 kwa kumng’ata beki wa Chelsea Branislav Ivanovic lakini alimaliza katika nafasi ya tatu katika orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu nchini Uingereza akiwa na mabao 23. Liverpool haijafuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya toka mwaka 2009 lakini pamoja na vilabu vikubwa kummezea mate Suarez, kocha huyo ana imani kwamba ataweza kumbakisha mchezaji huyo kwa msimu ujao. Rodgers amesema kwasasa wanajipanga kutengeneza kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao na Suarez ni sehemu ya kikosi hicho ingawa amekiri kwamba zipo baadhi ya klabu kubwa zinazomtaka.

GARCIA AMUOMBA RADHI MCHEZAJI NAMBA MOJA TIGER WOODS

MCHEZAJI machachali wa  mchezo wa gofu, Sergio Garcia ameomba radhi kwa kauli yake ambayo inaweza kuonekana kama ya kibaguzi kwenda kwa nyota wa mchezo huo anayeshika namba moja kwa ubora Tiger Woods. Garcia mwenye umri wa miaka 33 aliulizwa kama ataweza kula chakula cha jioni na Woods ili kuzungumzia tofauti zao za hivi karibuni na mchezaji huyo kutania kuwa atamuandalia kuku wa kukaanga nyota huyo. Kuku wa kukaanga ni chakula kinachohusishwa na watu weusi huko Marekani haswa wale wanaotoka kusini mwa nchi hiyo. Garcia aliomba radhi kwa kauli hiyo kama imeeleweka vibaya akidai kuwa hakumaanisha chochote kuhusu ubaguzi wa rangi kwa nyota huyo ambao ambaye asili yake ni mweusi.

MURRAY AJITOA MICHUANO YA WAZI UFARANSA:

MCHEZAJI nyota maarufu wa tenisi kutoka Uingereza Andy Murray amejitoa katika michuano ya wazi ya Ufaransa kutokana na maumivu ya mgongo yaliyopelekea kushindwa kuendelea kucheza katika michuano ya wazi ya Italia. Murray ambaye anashika namba mbili katika orodha za ubora Duniani kwa upande wa wanaume amejitoa katika michuano hiyo baada ya kushauriwa na madaktari wake na anatarajia kurejea tena uwanjani katika michuano ya Wimbledon katikati ya mwezi ujao. Nyota huyo ambaye ni bingwa wa michuano ya wazi ya Marekani amesema umekuwa ni uamuzi mgumu kufanya kwani huwa anapenda kucheza jijini Paris lakini imekuwa nje ya uwezo wake kwasababu ya ushauri wa kiafya aliopewa. Murray aliwaomba radhi waandaaji wa michuano hiyo na kuwashukuru mashabiki wake kwa kumtumia ujumbe wa kumuunga mkono na sasa kazi kubwa aliyokuwa nayo ni kuhakikisha anapona na kurejea haraka uwanjani.