Monday, May 20, 2013

MOURINHO HATARINI KUNG"OKA HUKU ANCELOTTI KUGOMEWA KUONDOKA".


RAIS wa club ya Paris St-Germain amemthibitishia meneja wa timu hiyo CarloAncelotti hataruhusiwa kuihama Klabu hiyo kwenda Real Madrid huko Jijini Madrid huku Uongozi wa Real madrid upo katika mipango ya kumtimua Jose Mourinho huku wakiwa na Mechi mbili za La Liga kumalizia Msimu.
Inaaminika leo Bodi ya Real Madrid inafanya Kikao na inategemewa kutoa tamko la kumtimua Jose Mourinho na hatua hii inakuja hasa baada ya Ijumaa kunyukwa kwenye Fainali ya Copa del Rey Bao 2-1 na Atletico Madrid na kuhakikisha Msimu huu wanamaliza bila Taji kubwa ukiondolea mbali Super Cup.
Jumamosi ijayo Real Madrid wanapepetana na Real Sociedad katika Mechi ya La Liga ya kukamilisha Ratiba tu kwa vile wao wameshakamata Nafasi ya Pili na Bingwa tayari ni Mahasimu wao FC Barcelona ambao wamewavua Ubingwa.
tetesi zilizopo  Jose Mourinho yuko mbioni kurudi Klabu yake ya zamani Chelsea.
Na huko Paris, Rais wa PSG kutoka Nchini Qatar, Nasser al-Khelaifi, amemkatalia Carlo Ancelotti kuondoka Klabu hiyo baada ya Meneja huyo kuomba kufanya hivyo.
Ancelotti, Miaka 53, amesema: “Nimeomba kuondoka na  hivyo nasubiri jibu!”
Nae Rais Nasser al-Khelaifi amejibu: “Ameomba kuondoka kwenda Real. Haiwezekani kwa vile bado ana Mkataba wa Mwaka mmoja, hivyo huo ni uamuzi wetu
ANCELOTTI-Mafanikio:
Juventus: Intertoto Cup 1999
AC Milan: Coppa Italia 2003, UCL 2003 & 2007, UEFA SUPER CUP 200 & 2007; Serie A 2004; Supercoppa Italiana 2004; Fifa Club World Cup 2007
Chelsea: Ngao ya Jamii 2009; BPL 2010; FA CUP 2010
PSG: Ligue 1 2013

MOYES AANZA RASMI HIMAYA YAKE KATIKA CLUB YA MAN UNITED.


ALIYEKUWA kocha wa EVERTON DAVID MOYES leo ameanza rasmi  himaya yake kwa Mabingwa wa England Manchester United tangu kustaafu Sir Alex Ferguson wakati alipokwenda Carrington, Kituo cha Mazoezi cha Mabingwa hao, kwa mara ya kwanza kukutana na Wachezaji na Wafanyakazi wote.
Ingawa anatakiwa kuanza kazi rasmi hapo Julai 1, Moyes ameamua kuanza mapema ili kurahisisha Kipindi hiki cha Mpito ambacho Man United inashuhudia mabadiliko ya Uongozi kwa mara ya kwanza tangu Mwaka 1986 Sir Alex Ferguson alipotwaa madaraka.
Akiongea Jana mara baada ya Mechi yake ya mwisho akiwa na Everton walipofungwa 2-1 na Chelsea, Moyes alisema: “Nadhani kwa Wiki mbili zijazo ntakuwa na kazi mbili. Ntakuwa pia Siku nyingine nakwenda Finch Park [Kituo cha Mazoezi cha Everton] kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa kwa Meneja mpya.”
Moyes, ambae alidumu Everton Miaka 11, anarithi himaya ya Sir Alex Ferguson ya mafanikio makubwa ya kutwaa Vikombe 38 katika Miaka 26 yakiwemo Mataji ya Ubingwa wa Ligi Kuu England mara 13.
Kazi kubwa ambayo itabidi aanze nayo ni kuamua hatima ya Straika Wayne Rooney ambae Sir Alex Ferguson alitoboa hivi karibuni kuwa ameomba kuihama Man United.
Hii ni mara ya Pili ndani ya Miaka mitatu kwa Rooney kuomba Uhamisho na hili itabidi litafutiwe ufumbuzi na Moyes ambae ndie Mtu aliemkuza Rooney alipokuwa Everton na kumpandisha kucheza Timu ya Kwanza akiwa na Miaka 16 tu.
Lakini, Rooney alikorofishana na Moyes mara baada ya kuihama Everton na kwenda Man United wakati Straika huyo alipoandika kwenye Kitabu chake kashfa dhidi ya Moyes ambae alishitaki na kushinda Kesi na kulipwa Fidia.
Hata hivyo, Mwaka 2010, Rooney alimtaka radhi Moyes ambae alimsamehe wakati huo huo.
Hata hivyo Wachambuzi wanahisi kuondoka kwa Rooney wakati huu hakutazua athari yeyote kwa Mabingwa Man United kwani wanae Mfungaji Bora wa England, Robin Van Persie, aliefunga Bao 26 katika Msimu wake wa kwanza na Man United na kutwaa Buti ya Dhahabu.
Pia, Moyes anatarajiwa kuamua hatima za Wasaidizi wa Ferguson, Makocha Mike Phelan na Rene Meulensteen, ingawa mwenyewe ameshadokeza hakutakuwa na mabadiliko makubwa lakini inaaminika aliekuwa Msaidizi wa Moyes huko Everton, Steve Round, Kocha Jimmy Lumsden na Mchezaji wa zamani wa Man United, Phil Neville, watakuwa nae kwenye Benchi la Ufundi la Mabingwa hao.

NICOLA KUCHEZESHA CHAMPIONS LEAGUE MEI 25

SHIRIKISHO la Soka barani Ulaya, UEFA limemtangaza Nicola Rizzoli wa Italia kuwa mwamuzi katika mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Bayern Munich na Borussia Dortmund itakayochezwa Jumamosi ijayo katika Uwanja wa Wembley jijini London Uingereza. Hiyo itakuwa mechi ya tano ya michuano hiyo kwa Rizzoli msimu huu na mechi ya 27 kwa jumla toka ateuliwe kuchezesha michuano hiyo kwa mara ya kwanza huku mchezo wake wa mwisho ukiwa ni wa Malaga dhidi ya Porto katika hatua ya timu 16 bora Machi mwaka huu. Rizzoli mwenye umri wa miaka 41 ambaye amekuwa mwamuzi wa kimataifa toka mwaka 2007, amewahi pia kuchezesha fainali ya michuano ya Europa League mwaka 2010 kati ya Fulham na Atletico Madrid. Katika fainali ya Wembley Rizzoli atakuwa akisaidiwa na Muitaliano mwenzake Renato Faverani na Andrea Stefani huku wengine wakiwa ni Damir Skomina kutoka Slovakia na wengine wawili kutoka Italia ambao ni Gianluca Rocchi na Paolo Tagliavento.

WENGER AKIRI FURAHA WALIONAYO WACHEZAJI

Bosi wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amekiri kuwa amefurahi timu yake hiyo kuwaaibisha wale waliyoiponda baada ya kujihakikishia nafasi yao ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Newcastle United jana. Nafasi ya Arsenal kumalizika katika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu ya Uingereza ulikuwa ukipondwa na wachambuzi wa soka wakati walipokuwa nyuma ya mahasimu wao Tottenham Hotspurs kwa alama saba huku kukiwa kumebakia mechi 10. Lakini Ushindi wao dhidi ya Newcastle jana, kwa bao lililofungwa na Laurent Koscielny, limewahakikishia kumaliza katika nafasi ya nne wakiwapita kwa alama moja moja mahasimu wao wa London Tottenham na kupata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya 16 mfululizo. Wenger amesema wamepitia magumu mengi msimu huu lakini anashukuru wachezaji wake walitengeneza ari ya ushindi mwishoni mwa msimu kitu ambacho kwa kiasi kikubwa kimechangia kumaliza wakiwa katika nafasi nne za juu.

NGASSA HUYOO ATIMKIA JANGWANI TENA MARA NYINGINE


Uongozi wa mabingwa wa ligi kuu soka ya Vodacom Tanzania Bara Dar Es Salaam Young African imemtambulisha rasmi mshambuliaji MRISHO HALFAN NGASA kuwa mchezaji wao kwa ajili wa msimu ujao wa ligi hiyo. NGASA alikuwa anacheza kwa mkopo kwa wapinzani wa jadi wa Yanga , Simba akitokea katika Klabu ya Azam ya Jijini Dar Es Salaam. Akimtambulisha rasmi mbele ya Waandishi wa Habari hii leo Makao Makuu ya Klabu hiyo Katibu wa Yanga LAWRANCE MWALUSAKO amesema wamefikia hatua hiyo baada ya kufanya mazungumza na mshambuliaji na kuamua kurejea katika Klabu yake hiyo ya zamani. MWALUSAKO amesema NGASA ambaye amekiri kuwa na mahaba ya dhati na Klabu hiyo ameingia mkataba wa miaka miwili. Akizungumza baada ya kutambulishwa rasmi NGASA amesema anamshukuru Mungu kwa kumwezesha kurejea katika Klabu yake hiyo ya zamani ambaye amesema ni kama Nyumbani kutokana na mapenzi aliyonayo. Mshambuliaji huyo pia amewataka mashabiki wake kuendelea kumuunga mkono na anaimani kuwa atafanya vizuri katika Klabu hiyo ambayo amewahi kuichezea huko nyuma.