Friday, May 23, 2014

TANZANIA U15 YAANZA NA SARE DHIDI YA AYG

Tanzania imeanza Michezo ya Afrika kwa Vijana (AYG) inayofanyika nchini Botswana kwa kutoka sare ya bao 1-1 na Mali kwa upande wa mpira wa miguu kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 katika mechi iliyochezwa leo (Mei 22 mwaka huu).
tanzania-tour-guide-flagMechi hiyo ilichezwa Uwanja wa SSKB jijini Gaborone ambapo Tanzania ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 52 mfungaji akiwa Amani Ali. Hata hivyo, Mali walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 61.
Tanzania itacheza mechi yake ya pili kesho (Mei 23 mwaka huu) kwa kuwakabili wenyeji Botswana kwenye uwanja huo huo kuanzia saa 8 kamili mchana kwa saa za Tanzania. Mechi hizo zinaoneshwa moja kwa moja na kituo cha SuperSport.
Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo, Tanzania itacheza mechi nyingine Mei 25 mwaka huu dhidi ya Swaziland, itakuwa tena uwanjani Mei 27 mwaka huu kuikabili Nigeria wakati mechi ya mwisho itakuwa Mei 29 mwaka huu dhidi ya Afrika Kusini.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Uongozi wa Klabu ya Young Africans umeshangazwa na taarifa zilizoandikwa kwenye mojawapo ya vyombo vya habari juu ya Wanachama wa Tawi la Tandale kusema hawatambui kufutwa kwa Tawi lao ni za Ubabaishaji.
 
Mnamo Mei 04, 2014 Mwenyekiti wa Klabu ya Young Africans Bw Yusuf Manji alitangaza kulifuta Tawi la Tandale kutokana na kua chanzo cha migogoro ndani ya klabu kwa kipindi cha mrefu, ili hali likiwa halina hadhi ya kuwa Tawi Kamili.
 
Kufutwa kwa Tawi la Tandale kunatokana na kutotimiza idadi ya wanachama mia moja (100)  kama inavyojieleza kwenye Katiba ya Yanga SC, Ibara ya 6, kipengele cha 4 "Kutakuwa na uundaji wa matawi katika maeneo mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi. Kiwango cha chini ya idadi ya wanachama ambao wanaweza kunda tawi kisipungue watu mia moja (100)".
 
Ibara ya 13, kipengele cha 2 kinasema " Kutolipa ada zake za uanachama kwa muda wa miezi sita mfululizo bila ya sababu maalum inayokubalika na Kamati ya Utendaji"
 
Baadhi ya Wanachama walijifuta uanchama wao kutokana na kushindwa kulipia ada zao za uanachana kwa kipindi cha zaidi ya miezi sita, kama inavyojieleza kwenye Katiba kwamba mwanachama asipolipia ada yake zaidi ya miezi sita moja kwa moja anajifuta uanachama wake.
 
Hivyo Uongozi wa klabu ya Yanga SC unaomba Umma na Wanachama wake Duniani kote watambue kuwa Tawi la Tandale lilifutwa kwa kutokana na kutokidhi vigezo, huku wanachama wake wengine watano wakijifuta uanachama kwa kushindwa kulipia ada zao kwa kipindi cha zaidi ya miezi sita.
 
Mwisho wanachama wa klabu ya Yanga SC wanaombwa kulipia ada zao za uanchama mapema kabla ya muda wao kumalizika ili waweze kushiriki mkutano mkuu wa marekebisho ya Katiba utakaofanyika kwenye Ukumbi wa Bwalo la Polisi - Oysterbay Juni Mosi 2014.

Beno Njovu
Katibu Mkuu - Yanga SC
Mei 23, 2014