Wednesday, July 10, 2013

CAF YABADILI MWAMUZI MECHI YA STARS

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limefanya mabadiliko ya mwamuzi wa mechi ya mchujo kusaka tiketi ya Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi ya Ndani (CHAN) kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Uganda (The Cranes) itakayochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwamuzi aliyeondolewa kutokana na sababu za kiufundini Jean Claude Birumushahu aliyekuwa mwamuzi msaidizi namba moja. Nafasi yake sasa inachukuliwa na Herve Kakunze pia kutoka Burundi.
CAF imemuondoa mwamuzi huyo baada ya kufeli katika mtihani wa waamuzi (Cooper Test) kwa waamuzi wa Burundi wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) uliofanyika nchini humo siku tatu zilizopita.
Waamuzi hao na Kamishna wa mechi hiyo Gebreyesus Tesfaye kutoka Eritrea wanatarajiwa kuwasili nchini kesho (Julai 11 mwaka huu) kwa ndege za Kenya Airways na EgyptAir kwa muda tofauti.
Nayo Uganda Cranes inatarajiwa kuwasili nchini kesho (Julai 11 mwaka huu) na itafikia hoteli ya Sapphire. Shirikisho la Mpira wa Miguu Uganda (FUFA) bado halijatuma taarifa rasmi juu ya ujio wa timu hiyo.
Wakati huo huo, makocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen na wa Uganda, Milutin Micho pamoja na manahodha wao watakuwa na mkutano na Waandishi wa Habari utakaofanyika keshokutwa (Julai 12 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF kuzungumzia mechi ya Jumamosi.
FRIENDS, POLISI KUCHEZA MECHI YA RCL JUMAPILI
Mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kati ya Friends Rangers ya Dar es Salaam na Polisi Jamii ya Mara iliyokuwa ichezwe Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) imesogezwa mbele kwa siku moja.
Timu hizo sasa zitacheza Jumapili (Julai 14 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi. Polisi Jamii ilishinda bao 1-0 mechi ya kwanza iliyochezwa Julai 6 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.
Refa Hans Mabena kutoka Tanga ndiye atakayechezesha mechi akisaidiwa na E. Mkumbukwa na Hajj Mwalukuta wote kutoka Tanga. Mwamuzi wa akiba (fourth official) ni Kessy Ngao wa Dar es Salaam.
Mechi kati ya Stand United FC ya Shinyanga na Kimondo SC ya Mbeya itachezwa Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Mwamuzi atakuwa Daniel Warioba kutoka Mwanza. Kimondo SC ilishinda mechi ya kwanza bao 1-0.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

BLANC KOCHA MPYA WA PSG AANZA KWA KIPIGO CHA BAO 3-1

Kocha mpya wa klabu ya Paris Saint-Germain-PSG, Laurent Blanc ameanza vibaya kibarua chake baada ya mchezo wake wa kwanza wa kirafiki kujiandaa na msimu wa ligi kumalizika kwa mabingwa hao wa soka nchini Ufaransa kupokea kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa timu ya Sturm Graz ya Austria. Wenyeji ndio waliotangulia kushinda bao la kwanza dakika ya 26 kupitia kwa mchezaji Robert Beric akiyatumia vyema makosa ya beki kinda wa PSG Antoine Conte kabla ya Marco Djuricin kuongeza bao la pili dakika mbili baadae. Sturm ambao walionekana kuwa fiti zaidi baada ya kuanza mazoezi wiki mbili kabla ya PSG waliongeza bao la tatu katika dakika ya 76 kupitia kwa Nikola Vujadinovic wakati PSG walipata bao lao la kufutia machozi kupitia kwa Hervin Ongenda dakika tano kabla mpira haujamalizika. PSG wataendelea na maandalizi yao kwa ajili ya kujiwinda na msimu mpya kwa mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya Rapid Vienna Ijumaa.

CHALSEA YAMSAJILI KIPA WA KIMATAIFA WA AUSTRALIA "MARK"

KLABU ya Chelsea ya Uingereza, imefanikiwa kunasa saini ya golikipa wa kimataifa wa Australia Mark Schwarzer kwa usajili huru mpaka mwishoni mwa michuano ya Kombe la Dunia mwakani. Schwarzer mwenye umri wa miaka 40, amecheza soka kwa muda wa miaka 15 nchini Uingereza katika vilabu vya Bradford City, Middlesbrough na Fulham. Msimu uliopita golikipa huyo alitajwa kuwa mchezaji wa kwanza kutoka nje ya Uingereza kucheza mechi 500 katika Ligi Kuu nchini humo. Akihojiwa mara baada ya kukamilisha usajili wake, Schwarzer amesema ni heshima kubwa kwake kuiwakilisha klabu yenye hadi ya juu duniani kama Chelsea na anamatumaini ya kufanya vyema akiwa hapo.

DOS SANTOS AKAMILISHA USAJILI KATIKA CLUB YA VILLAREAL"

Kiungo nyota wa kimataifa wa Mexico, Giovani Dos Santos amekamilisha usajili wake wa kujiunga na klabu Villareal ambayo imepanda ligi msimu huu akitokea klabu ya Real Mallorca zote za Hispania. Dos Santos mwenye umri wa miaka 24 ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Mexico kilichonyakuwa medali ya dhahabu katika michuano ya olimpiki jijini London mwaka jana, amesaini mkataba wa miaka minne na klabu hiyo. Kiungo huyo mshabuliaji aliibukia katika shule ya watoto ya Barcelona kabla ya kwenda katika klabu ya Tottenham Hotspurs mwaka 2008 kwa uhamisho wa euro milioni sita. Hata hivyo Dos Santos alishindwa kung’aa sana katika kikosi cha kwanza na kujikuta akipelekwa kwa mkopo katika timu ya daraja la pili ya Ipswich Town na baadae kwenda Galatasaray ya Uturuki na Racing Santander.

WANNE KUTOKA BAYEN MUNICH NAO KATIKA ORODHA YA FIFA

Club ya Bayern Munich ya ujerumani imefanikiwa kutoa wachezaji wa nne walioteuliwa katika orodha ya wachezaji 10 na Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA kugombea tuzo ya mchezaji bora wa bara hilo kwa msimu wa 2012-2013. Wachezaji hao ni Franck Ribery, Thomas Mueller, Arjen Robben na Bastian Schwainsteiger ambao wote walikuwemo katika kikosi cha Bayern ambacho kilifanikiwa kunyakuwa mataji matatu msimu uliopita. Mbali na hao wengine waliotajwa katika orodha hiyo ni mchezaji bora wa mwaka katika Ligi Kuu nchini Uingereza, Gareth Bale pamoja na mfungaji bora wa ligi hiyo Robin van Persie huku Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wakiwa wachezaji pekee kutoka La Liga ya nchini Hispania kwenye orodha hiyo. Hii itakuwa ni mara ya tatu kufanyika sherehe za tuzo hizo ambapo mwaka 2011 Messi ndiye aliyeshinda huku mchezaji mwenzake wa Barcelona Andres Iniesta akishinda tuzo hiyo mwaka jana. Wachezaji wengine ni Mshambuliaji nyota wa klabu ya Paris Saint-Germain-PSG, Zlatan Ibrahimovic na Robert Lewandowski anayekipiga Borussia Dortmund ambapo orodha ya mwisho ya wachezaji watatu itatajwa Agosti 6 kabla ya sherehe za kumjua mshindi ambazo zitafanyika wakati wa upangaji wa ratiba ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Agosti 29 mwaka huu jijini Monaco.