Uongozi wa
klabu ya Young Africans unapenda kuwajulisha wanachama wake, wapenzi wa
soka na wadau kwa ujumla kuwa taarifa za kuhama kwa wachezai wake
Didier Kavumbagu na Frank Domayo kwenda kujiunga na Azam FC
zisiwakatishe tamaa, ni mapenzi ya wachezaj wenyewe kwani
walishakubaliana na uongozi kila kitu juu ya kuendelea kuitumikia Yanga
kabla ya siku mbili hizi kuonekana wakiwa wamejiunga na wana ramba
ramba.
Yanga tayari ina wachezaji watatu
wenye mikataba inayoendelea na kama kanuni za VPL kwa wachezai wa
kimataifa kuwa watatu zitatumika wachezaji Haruna Niyonzima, Hamisi
Kizza na Emmanuel Okwi ndio watakaoendelea, hivyo uongozi uliomba
mwongozo kwa TFF juu ya taratibu zitakazotumika kwa msimu ujao kabla ya
kuwasainisha Kavumbagu na Twite.
Didier
Kavumbagu na Mbuyu Twite ambao mikataba yao ilikuwa mwishoni waliongea
na uongozi tangu mapema mwaka jana mwezi wa Septemba juu ya kuweka
sahihi zao na kuendelea kuitumikia Yanga na kukubaliana mambo yote ya
msingi kikubwa kilichokuwa kinasubiriwa ni maamuzi ya TFF juu ya usajili
wa wachezaji wa kigeni msimu mpya wa 2014/2015 kwani Azimio la Bagamoyo
linapaswa kuanza kutekelezwa msimu huu.
Uongozi
wa Yanga uliandikia TFF barua mapema kuomba kupewa mwongozo wa kanuni
zitakazotumika kwenye usajli kwa wachezaji wa kimataifa kwa msimu mpya
kufuatia Azimio la Bagamoyo kuelekeza msimu huu kila timu inapasa kuwa
na wachezaji watatu wa kigeni, mpaka sasa uongozi wa Yanga haujapata
majibu juu ya utaratibu utakaotumika kwenye msimu wa Ligi Kuu ijayo.
Kuhusu Frank Domayo aliyeripotiwa jana
kujiunga na Azam FC pia alikuwa katika makubalianoya kuongeza mkataa
tangu mwezi Julai 2013, alikubaliana na uongozi juu ya mambo yote ya
msingi na kilichobakia ilikuwa ni kuweka sahihi kwenye mkataba mpya,
lakini Domayo alisema hawezi kusaini mpaka siku atakapokuja mjomba wake
ambaye ndie wakala wake na ahadi hiyo iliendelea kwa muda wa mwaka mzima
kabla ya jana kusikia ameshasaini timu nyngine.
Habari hizi
zimewashitua wapenzi, wanachama na washabiki wa Young Africans lakini
ukweli ni kuwa wachezaji wenyewe walisindwa kuwa wakweli kwa viongozi na
mwisho wa siku walikua na mipango yao ya kuondoka, hivyo uongozi
ulijtahid kadri ya uwezo wake lakini wachezaji wanaonekana hawakua
tayari kuendelea kuichezea Yanga SC.
Taarifa kamili kuhusu mipango
ya timu kwa msimu ujao pamoja na ripoti ya kocha mkuu Hans pamoja na
benchi lake la Ufundi zitatolewa hivi karibuni baada ya benchi la ufundi
na uongozi kukaa kwa pamoja na kuafikiana mipango ya msimu ujao.
Aidha
uongozi wa Yanga SC unawaomba wanachama wake, wapenzi na washabiki
wasiwe na wasi wasi juu ya kuondoka kwa wachezaji hao kwani Yanga bado
ina nafasi wachezaji wengi wenye vipaji na itaendelea kuboresha kikosi
chake kwa kuzingatia maelekezo ya kocha mkuu Hans katika usajli wa msimu
ujao.