Thursday, July 11, 2013

DROGBA ATANGAZA KUJENGA HOSPITAL 5 ZA KINA MAMA NA WATOTO"NCHINI IVORY" COAST


Didier Drogba mshambuliaji nyota wa zamani wa Chelsea ametangaza kuwa atajenga Hospitali 5 ili kuwasaidia wakina Mama na Watoto huko Nchini Ivory Coast kwa gharama ya Dola Milioni 5.
Uamuzi huu umetangazwa huko Mjini Abidjan na Katibu wa Didier Drogba Foundation, Guy Roland Tanoh, ambae amesema itajengwa Hospitali moja katika Miji mitano ya Ivory Coast ambayo ni Abidjan, Yamoussoukro, Man, Korhogo na San Pedro.
Kwenye Tafrija huko London tulichangisha na kukusanya Dola Milioni 4 na zilizobaki si tatizo ili kukamilisha Mradi huu ambao uko moyoni kabisa mwa Drogba.”
Tanoh pia ametoboa pia kuwa Taasisi hiyo ya Drogba imeshatoa misaada kwa Watoto yatima na wale ambao wapo kwenye mazingira magumu.
Taasisi ya Didier Drogba ilianzishwa Mwaka 2007 na ilipanga kujenga Hospitali yenye gharama ya Pauni Milioni 3 lakini hadi leo ilikuwa haijajengwa na Tanoh hakufafanua kama Hospitali hiyo ni moja ya hizo tano zitakazojengwa.
Wakati huo, Drogba, mwenye Miaka 35 hivi sasa na ambae anachezea Klabu ya Turkey Galatasaray, alisema ujenzi wa Hospitali hiyo utatokana na malipo ya Picha na Matangazo yake na Kampuni ya Pepsi.

TIMU YA AFRICAN LYON ILIYOSHUKA DARAJA YAPATA HASARA YA SH.180.3

TIMU ya soka ya African Lyon ya jijini Dar es Salaam imetangaza hasara ya sh. milioni 180.3 kutokana na ushiriki wake katika msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Lyon ni miongoni mwa timu tatu zilizoshuka daraja kutoka katuika ligi hiyo kubwa ya soka nchini, nyingine ni Toto African na Polisi Moro.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Meneja wa Fedha wa Lyon, Ibrahim Salim, alisema timu yao imetumia zaidi ya sh. 388,614,500 kwa ajili ya maandalizi hadi michezo yake.
Salim amesema katika makusanya na matumizi yao, walilazimika kutumia kiasi cha sh. milioni 268.09 katika mzunguko wa kwanza, kabla ya kutumia sh. 123.6.
"Katika matumizi yote haya, fedha ambayo tumeiingiza kama klabu kupitia viingilio na vyanzo vingine ni sh. milioni 207.6, na hapo ndipo unapopata tofauti ya sh. milioni 180.3, ambayo ni hasara," Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Lyon, Rahim Kangezi, alisema soka ya Tanzania inaendeshwa kwa hasara huku wenye dhamana ya kusaidia wakiwa hawatendi haki kwa baadhi ya vipengele.
Kangezi alisema timu yake imeingia katika hasara ya sh. milioni 180.3 kutokana na uendeshaji, lakini bado wameshuka daraja, huku akisisitiza kuwa hakuna anayeshutumiwa kwa kushuka kwa timu hiyo"Unaweza kuona changamoto ambayo tunakumbana nayo katika uendeshaji wa taasisi kamam a hizi, tunapopiga kelele kwa wadhamini kutuwahishia fedha tunamaanisha."Angalieni mfano mdogo kwa fedha za wadhamini (Vodacom), ambazo awamu ya mwisho zimetufikia Mei mwaka huu, tukiwa tumebakiza mechi moja ya Ligi Kuu, sasa zingetusaidia katika nini? Alihoji mmiliki huyo.
Akizungumzia kuhusu uendeshwaji wa Ligi Kuu na changamoto walizokutana nazo, Kangezi alisema bado hakujakuwa na usimamizi mzuri katika kuhakikisha kuwa ligi hiyo inakuwa bora.
Katika hatua nyingine, Kangezi amesema timu yake inajivunia mafanikio waliyochangia kusogeza maendeleo ya soka nchini kutokana na kutoa nafasi kwa Mrisho Ngassa kwenda kujaribu soka ya kulipwa na kucheza katika kikosi cha Seattke Soundowns dhidi ya Manchester United.
"Tulifanikiwa pia kuileta timu kubwa ya Ligi Kuu ya Brazil (Atletico Parenese) kwa ziara ya kimichezo nchini, tulitoa wachezaji watano kwa ajili ya kujaribu soka ya kulipwa sambamba na kufanya semina mbili juu ya uongozi wa michezo," aliongeza.

UGANDA CRANES YAWASILI KUIKABILI STARS MICHUANO YA CHAN KWA WANANDINGA WA NDANI"

Timu ya Taifa ya Uganda (The Cranes) imewasili Dar es Salaam leo tayari kwa mechi ya kwanza ya mchujo kusaka tiketi ya Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi ya Ndani (CHAN) kati yake na Tanzania (Taifa Stars) itakTFF_LOGO12ayochezwa Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
The Cranes inayofundishwa na Mserbia Sredojvic Micho imetua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 5.30 asubuhi kwa ndege ya Air Uganda, na imefikia hoteli ya Sapphire.
Timu hiyo leo (Julai 11 mwaka huu) itafanya mazoezi saa 9 alasiri kwenye Uwanja wa Karume, wakati kesho saa 9 alasiri itafanya mazoezi Uwanja wa Taifa, kabla ya kuipisha Taifa Stars itakayoanza mazoezi saa 10 kamili jioni.
Taifa Stars inayofundishwa na Mdenmark Kim Poulsen, na kudhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, leo kwa mujibu wa program yake haitakuwa na mazoezi.
Wachezaji wanaounda The Cranes ni makipa Ismail Watenga, Kimera Ali na Muwonge Hamza. Mabeki ni Guma Dennis, Kasaaga Richard, Kawooya Fahad, Kisalita Ayub, Magombe Hakim, Malinga Richard, Mukisa Yusuf, Savio Kabugo na Wadada Nicholas.
Viungo ni Ali Feni, Birungi Michael, Frank Kalanda, Hassan Wasswa, Kyeyune Said, Majwega Brian, Mpande Joseph, Muganga Ronald, Ntege Ivan, Owen Kasule, wakati washambuliaji ni Edema Patrick, Herman Wasswa na Tonny Odur.
TENGA KUZUNGUMZA NA WAANDISHI KESHO
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga atakuwa na mkutano na waandishi wa habari. Mkutano huo utafanyika kesho (Julai 12 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwenye hoteli ya Tansoma.
Kutokana na mkutano huo, sasa mkutano kati ya makocha wa Taifa Stars na The Cranes uliokuwa ufanyike saa 5 asubuhi ofisi za TFF nao umehamishiwa hoteli ya Tansoma. Mkutano huo pia utahusisha manahodha wa timu zote mbili.
WAJUMBE MKUTANO MKUU MAALUMU KUWASILI KESHO
Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) utakaofanyika Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) wanawasili jijini Dar es Salaam kesho (Julai 12 mwaka huu).
Mkutano huo wa marekebisho ya Katiba utakuwa chini ya uenyekiti wa Rais wa TFF, Leodegar Tenga na utafanyika ukumbi wa NSSF Waterfront kuanzia saa 3 kamili asubuhi. Wajumbe wote wa mkutano huo watafikia hoteli ya Travertine.
Pia mkutano huo utahudhuriwa na wageni mbalimbali waalikwa wakiwemo kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA).
MECHI YA STAND, KIMONDO NAYO KUPIGWA JUMAPILI
Mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kati ya Stand United FC ya Shinyanga na Kimondo SC ya Mbeya iliyokuwa ichezwe Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) imesogezwa mbele kwa siku moja.
Timu hizo sasa zitacheza Jumapili (Julai 14 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Kimondo ilishinda bao 1-0 mechi ya kwanza iliyochezwa Julai 6 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Mechi nyingine ya ligi hiyo itakuwa kati ya Friends Rangers ya Dar es Salaam na Polisi Jamii ya Mara, na itafanyika kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Mwamuzi wa mechi hiyo ni Hans Mabena kutoka Tanga.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)