Monday, May 6, 2013

KMKM YAWEKA HISTORIA KUTWAA UBINGWA WA ZANZIBAR

Ligi kuu ya Zanzibar Grand Malt msimu wa 2012/2013 imemalizika rasmi mwishoni mwa wiki ambapo timu ya KMKM imefanikiwa kuwa bingwa mpya huku timu ya Chuoni ikitwaa nafasi ya pili.
mabingwa watetezi wa ligi hiyo Super Falcon imepatwa na balaa na kushindwa kuhimili mikikimikiki na hatimaye kushuka daraja.
kutokana na kufanikiwa kutwaa ubingwa KMKM ndiyo itaiwakilisha Zanzibar katika Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Chuoni watajitupa katika michuano ya Kombe la Shirikisho.
Kmkm imefanikiwa kutwaa kombe, medali ya dhahabu kwa timu nzima pamoja na fedha taslimu Sh milioni 10, huku mshindi wa pili Chuoni akipata Sh milioni 5 pamoja na medali ya fedha kwa kila mchezaji.
Golikipa bora bora alikuwa ni Khamis Uzidi wa Zimamoto ambaye alikabidhiwa kikombe pamoja na fedha taslimu Sh 500,000 huku mfungaji bora wa ligi hiyo, Juma Mohd Juma wa Chuoni akijipatia Sh milioni 1 na kikombe.
Mchezaji bora wa Grand Malt premier League ni Abdullah Juma wa Jamhuri ya Pemba aliyekabidhiwa Sh milioni 1 taslimu pamoja na kikombe.
Mbali na hilo wadhamini wa ligi hiyo ilitoa zawadi kwa timu za madaraja mengine ambayo mshindi wa kwanza na wa pili katika Ligi Daraja la Kwanza ambazo ni Miembeni na Polisi zilikabidhiwa seti ya jezi na vikombe.
Zawadi hizo zilitolewa kwa mshindi wa kwanza na wapili wa Ligi Daraja la Pili ambazo ni Kimbunga na Bweleo fc.

BAFANABAFANA KUUMANA NA JAMHURI YA AFRIKA YA KATI JUNE 9.


TIMU ya taifa ya Afrika Kusini maarufu kama Bafana Bafana inatarajia kucheza mchezo wake wa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2014 dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati-CAR katika uwanja huru jijini Yaounde, Cameroon June 9 mwaka huu. 
Hatua hiyo imekuja kufuatia Chama cha Soka nchini Afrika Kusini-Safa ambao waliomba Shirikisho la Soka Duniani-FIFA na lile la Afrika-CAF kubadilishiwa uwanja katika mchezo wao wa marudiano kutokana na vurugu za kisiasa huko CAR.
Wanajeshi wapatao 13 wa Afrika Kusini walifariki kufuatia mapigano katika mji mkuu wan chi hiyo Bangui miezi iliyopita huku idadi hiyo ikiongezeka na kufikia 14 baada ya mwanajeshi mmoja aliyejeruhiwa naye kufariki mwezi uliopita. 
Kocha wa Bafana Bafana aliusifu uamuzi huo wa FIFA na CAF kubadilisha uwanja haswa kutokana na tukio la kuuwawa kwa wapendwa wao katika kipindi kifupi kwenye eneo hilo.

Uli Hoeness rais wa klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani anajipanga kutangaza kujiuzulu leo kwa muda baada ya mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mpaka hapo uchunguzi wa suala lake la ukwepaji kodi litakapomalizika. Hoeness mwenye umri wa miaka 61 amekuwa akishinikizwa kujiuzulu baada ya taarifa kuwa alikamatwa Machi 20 mwaka huu na baadae kuachiwa kwa dhamana ya kiasi cha euro milioni tano kama sehemu ya uchunguzi wa ukwepaji kodi. Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya Ujerumani, Hoeness anatarajiwa kutangaza uamuzi wake baadae leo katika kikao cha bodi ya maofisa wa klabu hiyo. Bayern ambayo imetinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuing’oa Barcelona kwa jumla ya mabao 7-0 katika mechi za mikondo walizokutana wanatarajiwa kumenyana na wajerumani wenzao Borussia Dortmund katika Uwanja wa Wembley Mei 25 mwaka huu.

RCL MCHAKATO WA UPANGAJI KUCHUKUA NAFASI KESHO"

MCHAKATO wa  upangaji wa ratiba ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) uliokuwa ufanyike juzi (Mei 3 mwaka huu), sasa utafanyika kesho Jumanne (Mei 7 mwaka huu) na ligi hiyo itaanza Mei 12 mwaka huu kama ilivyopangwa.
Uamuzi huo umefanya na Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliyokutana jana (Mei 5 mwaka huu) kujadili maandalizi ya ligi hiyo, yakiwemo maombi ya baadhi ya mikoa ambayo haijamaliza yao kutaka RCL isogezwe mbele.
Kamati ya Mashindano chini ya Uenyekiti wa Blassy Kiondo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF ilipitia maombi hayo na kuangalia athari ambazo zinaweza kujitokeza huko mbele iwapo RCL itasogezwa mbele.
Baadhi ya athari iwapo RCL itasogezwa mbele ni timu zitakazopanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kutopata muda wa kufanya usajili wa wachezaji kwa msimu mpya.

Hivyo draw hiyo itakayofanyika saa 6 mchana itahusisha mikoa ambayo tayari imemaliza ligi na kuwasilisha majina ya mabingwa wao. 
ni Abajalo SC (Dar es Salaam 2), Biharamulo FC (Kagera), Flamingo SC (Arusha), Friends Rangers (Dar es Salaam 3), Katavi Warriors (Katavi), Kiluvya United (Pwani), Kimondo FC (Mbeya) na Machava FC (Kilimanjaro).
Mingine ni Magic Pressure FC (Singida), Mbinga United (Ruvuma), Mji Njombe (Njombe), Polisi Jamii Bunda FC (Mara), Red Coast FC (Dar es Salaam 1), Rukwa United (Rukwa), Saigon FC (Kigoma), TECKFOLT FC ya Kilombero ambayo ni Shule ya Sekondari (Morogoro) na UDC FC ya Ukerewe (Mwanza).
Ada ya ushiriki ni sh. 100,000 wakati usajili wa wachezaji wa timu hizo ni uleule uliofanyika katika Ligi ya Mkoa na unatakiwa kuwasilishwa TFF kwa ajili ya uthibitisho.

TFF inapenda kusisitiza kuwa hakuna usajili mpya wa wachezaji kwa ajili ya ligi hiyo. Mikoa ambayo bado haijawasilisha mabingwa wake ni Dodoma, Geita, Iringa, Lindi, Manyara, Mtwara, Shinyanga, Simiyu, Tabora na Tanga.

KAGAME SASA NI WAKATI WA DARFUR NA KORDOFAN YA KUSINI.

KATIBU Mkuu wa Baraza la Michezo kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati-CECAFA, Nicholas Musonye amesema wameteua miji Darfur na Kordofan ya Kusini nchini Sudan kuwa wenyeji wa michuano ya vilabu inayoandaliwa na baraza hilo. Musonye amesema michuano hiyo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi kati ya June 18 na Julai 2 mwaka huu. Aliendelea kusema kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya kufanya ziara ya kukagua miundo mbinu pamoja na usalama katika miji hiyo ambayo imekabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa kipindi kirefu sasa. Amesema viwanja walivyochagua ni Uwanja wa El Fasher uliopo jijini Darfur na uwanja mwingine mdogo wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 20,000 uliopo Kordofan ya Kusini. Vilabu 13 vimeshathibitisha kushiriki michuano hiyo wakiwemo Yanga ya Tanzania ambao ndio mabingwa watetezi wa michuano hiyo.