Monday, May 6, 2013

BAFANABAFANA KUUMANA NA JAMHURI YA AFRIKA YA KATI JUNE 9.


TIMU ya taifa ya Afrika Kusini maarufu kama Bafana Bafana inatarajia kucheza mchezo wake wa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2014 dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati-CAR katika uwanja huru jijini Yaounde, Cameroon June 9 mwaka huu. 
Hatua hiyo imekuja kufuatia Chama cha Soka nchini Afrika Kusini-Safa ambao waliomba Shirikisho la Soka Duniani-FIFA na lile la Afrika-CAF kubadilishiwa uwanja katika mchezo wao wa marudiano kutokana na vurugu za kisiasa huko CAR.
Wanajeshi wapatao 13 wa Afrika Kusini walifariki kufuatia mapigano katika mji mkuu wan chi hiyo Bangui miezi iliyopita huku idadi hiyo ikiongezeka na kufikia 14 baada ya mwanajeshi mmoja aliyejeruhiwa naye kufariki mwezi uliopita. 
Kocha wa Bafana Bafana aliusifu uamuzi huo wa FIFA na CAF kubadilisha uwanja haswa kutokana na tukio la kuuwawa kwa wapendwa wao katika kipindi kifupi kwenye eneo hilo.

Uli Hoeness rais wa klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani anajipanga kutangaza kujiuzulu leo kwa muda baada ya mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mpaka hapo uchunguzi wa suala lake la ukwepaji kodi litakapomalizika. Hoeness mwenye umri wa miaka 61 amekuwa akishinikizwa kujiuzulu baada ya taarifa kuwa alikamatwa Machi 20 mwaka huu na baadae kuachiwa kwa dhamana ya kiasi cha euro milioni tano kama sehemu ya uchunguzi wa ukwepaji kodi. Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya Ujerumani, Hoeness anatarajiwa kutangaza uamuzi wake baadae leo katika kikao cha bodi ya maofisa wa klabu hiyo. Bayern ambayo imetinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuing’oa Barcelona kwa jumla ya mabao 7-0 katika mechi za mikondo walizokutana wanatarajiwa kumenyana na wajerumani wenzao Borussia Dortmund katika Uwanja wa Wembley Mei 25 mwaka huu.