Club ya Simba SC imeupeleka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mkataba wake mpya na mshambuliaji Mrisho Khalfan Ngassa, ambao unaonyesha ataitumikia klabu hiyo na msimu ujao pia, kwa mujibu wa blogu ya bin zubeiry.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya Simba SC, kimesema; “Tumeupeleka mkataba ambao Ngassa alisaini na sisi na TFF wamegonga muhuri wa kuupokea,”.
Kikifafanua, chanzo hicho kimesema; “Sisi tuliununua mkataba wa Ngassa uliokuwa umebaki Azam FC kwa shilingi Milioni 25, kwa hivyo, haki za mchezaji huyo zote zikahamia kwetu,”. “Lakini alipokuja kwetu, tukazungumza naye, akasaini mkataba wa msimu mmoja zaidi kutoka ule mkataba wake uliobaki Azam FC na tulimpa shilingi Milioni 30.
Fedha taslimu Milioni 12 na gari aina ya verosa yenye thamani ya Sh. Milioni 18, akasaini kila sehemu na kuweka dole gumba,”kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, chanzo hicho kimesema kwa sasa Mrisho amekuwa akilalamika kwa uongozi wa Simba kwamba alidhani alipewa Milioni 12 na Verosa ili akubali kuja Simba.
Ikumbukwe awali Ngassa aligoma kupelekwa kwa mkopo Simba SC, hadi alipofanya mazungumzo na viongozi wa klabu hiyo na kufikia makubaliano ndipo akajiunga na klabu hiyo.

“Bado tunatafakari, tunaweza kurudi naye mezani, ili aitumikie klabu kwa moyo bila kinyongo, au tu tukaamua autumikie mkataba ambao tayari tumekwishausajili na TFF,”kilisema chanzo.
Siku zote, Mrisho mwenyewe amekuwa akisistiza hakusaini mkataba mwingine Simba SC akitokea Azam, bali anajua alikuja kumalizia mkataba wake wa klabu yake ya zamani.
Mrisho Ngassa alipelekwa kwa mkopo Simba baada ya kuonyesha mapenzi kwa klabu yake ya Zamani ya yanga.