Katika habari ambazo tumezinasa
mchezaji huyo ameigharimu Yanga SC zaidi ya Sh. Milioni 60 kwa pamoja fedha
alizopewa za usajili na ambazo klabu yake ya Mtibwa imelipwa.
Yanga SC imeamua kumsajili Javu
kuimarisha safu yake ya ushambuliaji baada ya kuona kocha Mholanzi, Ernie
Brandts hajaridhishwa na mshambuliaji kutoka Nigeria, Ogbu Brendan Chukwudi na
wakati huo huo, Hamisi Kiiza anataka dau kubwa aendelee kuichezea timu hiyo.
Kiiza amemaliza Mkataba wake Yanga SC
na ili kuongeza Mkataba mwingine, viongozi wanashindwa kufika dau lake na sasa
wanaamua kumsajili Javu.
Javu ni kati ya washambuliaji wazuri
Tanzania kwa sasa, ambaye kwa misimu mitatu amekuwa mwiba dhidi ya vigogo wa
soka nchini, Simba na Yanga zinapokutana na timu hiyo ya Manungu.
Kocha Brandts amevutiwa mno na uwezo wa Javu na kwa ujumla amefurahia ujio wake
kwenye mazoezi ya Yanga SC leo.Javu ni mchezaji mwenye uzoefu ambaye
amekuwa akiitwa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars tangu enzi za
Mbrazil, Marcio Maximo ingawa mbele ya Mdenmark, Kim Poulsen hajawahi kupata
nafasi.
Kusajiliwa kwa Javu, kunaongeza
ushindani katika safu ya ushambuliaji ya Yanga SC, kwani sasa inakuwa na watu
wanne, wengine ni Jerry Tegete, Didier Kavumbangu, Shaaban Kondo, wakati huo
huo hatima ya Mnigeria Chukwudi na Kiiza haijajulikana kama wataachwa au
watasajiliwa.
Kwa majira haya ya joto, huyo anakuwa
mchezaji wa pili wa Mtibwa kusajiliwa Yanga baada ya beki, Rajab Zahir.
Kwa Mtibwa Sugar ni pigo, kwani katika
kikosi chao cha kwanza, huyo anakuwa mchezaji wa tatu kuondoka baada ya Issa
Rashid ‘Baba Ubaya’ aliyesajiliwa Simba SC na Shaaban Kisiga aliyejiondoa
kwenye timu, baada ya kutofautiana na kocha Mecky Mexime.
Wakati huo huo, kiungo Rashid Gumbo
anaonekana kutikisa kiberiti baada ya kung’ara akiichezea kwa mkopo timu hiyo
akitokea Yanga SC. Gumbo amemaliza Mkataba wake Yanga na sasa ili kuendelea
kuichezea Mtibwa, lazima wakae naye mezani.Kama ilivyo kawaida kwa Mtibwa ni si
jambo la kushangaza kuuza nyota wake kama Arsenal ya England, hali ambayo
imepunguza makali yake katika Ligi Kuu miaka ya karibuni, kwani kila nyota
anayeibuka anauzwa. Mtibwa iliibuka vizuri katika soka ya Tanzania ikitwaa
ubingwa wa Bara mara mbili mfululizo, 1999 na 2000, miaka mitatu tu tangu ianze
kucheza Ligi Kuu.
|