Thursday, July 25, 2013

JAVU ASAINI JANGWANI KUIMARISHA SAFU YA USHAMBULIAJI YA YANGA

Mshambuliaji nyota wa Club ya  Mtibwa Sugar ya Morogoro, Hussein Javu amesaini Mkataba wa miaka miwili kujiunga na Mabi
ngwa hao wa ligi kuu msimu uliopita Yanga SC ambapo hii leo asubuhi ameanza mazoezi kwenye Uwanja wa Sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga SC, Abdallah Bin Kleb amesema kwamba wamemalizana na Javu pamoja na klabu yake, Mtibwa na sasa huyo ni mchezaji mpya wa Jangwani.

Katika habari ambazo tumezinasa mchezaji huyo ameigharimu Yanga SC zaidi ya Sh. Milioni 60 kwa pamoja fedha alizopewa za usajili na ambazo klabu yake ya Mtibwa imelipwa.
Yanga SC imeamua kumsajili Javu kuimarisha safu yake ya ushambuliaji baada ya kuona kocha Mholanzi, Ernie Brandts hajaridhishwa na mshambuliaji kutoka Nigeria, Ogbu Brendan Chukwudi na wakati huo huo, Hamisi Kiiza anataka dau kubwa aendelee kuichezea timu hiyo.
Kiiza amemaliza Mkataba wake Yanga SC na ili kuongeza Mkataba mwingine, viongozi wanashindwa kufika dau lake na sasa wanaamua kumsajili Javu.
Javu ni kati ya washambuliaji wazuri Tanzania kwa sasa, ambaye kwa misimu mitatu amekuwa mwiba dhidi ya vigogo wa soka nchini, Simba na Yanga zinapokutana na timu hiyo ya Manungu. 
Kocha Brandts amevutiwa mno na uwezo wa Javu na kwa ujumla amefurahia ujio wake kwenye mazoezi ya Yanga SC leo.Javu ni mchezaji mwenye uzoefu ambaye amekuwa akiitwa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars tangu enzi za Mbrazil, Marcio Maximo ingawa mbele ya Mdenmark, Kim Poulsen hajawahi kupata nafasi.  
Kusajiliwa kwa Javu, kunaongeza ushindani katika safu ya ushambuliaji ya Yanga SC, kwani sasa inakuwa na watu wanne, wengine ni Jerry Tegete, Didier Kavumbangu, Shaaban Kondo, wakati huo huo hatima ya Mnigeria Chukwudi na Kiiza haijajulikana kama wataachwa au watasajiliwa.
Kwa majira haya ya joto, huyo anakuwa mchezaji wa pili wa Mtibwa kusajiliwa Yanga baada ya beki, Rajab Zahir.
Kwa Mtibwa Sugar ni pigo, kwani katika kikosi chao cha kwanza, huyo anakuwa mchezaji wa tatu kuondoka baada ya Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ aliyesajiliwa Simba SC na Shaaban Kisiga aliyejiondoa kwenye timu, baada ya kutofautiana na kocha Mecky Mexime.  
Wakati huo huo, kiungo Rashid Gumbo anaonekana kutikisa kiberiti baada ya kung’ara akiichezea kwa mkopo timu hiyo akitokea Yanga SC. Gumbo amemaliza Mkataba wake Yanga na sasa ili kuendelea kuichezea Mtibwa, lazima wakae naye mezani.Kama ilivyo kawaida kwa Mtibwa ni si jambo la kushangaza kuuza nyota wake kama Arsenal ya England, hali ambayo imepunguza makali yake katika Ligi Kuu miaka ya karibuni, kwani kila nyota anayeibuka anauzwa. Mtibwa iliibuka vizuri katika soka ya Tanzania ikitwaa ubingwa wa Bara mara mbili mfululizo, 1999 na 2000, miaka mitatu tu tangu ianze kucheza Ligi Kuu.