Tuesday, April 16, 2013

KAMATI  MAALUM YAUNDWA KUHUSU TAIFA STAR "

SERIKALI kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo imeunda kamati maalumu kwa ajili ya kuisaidia timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ili iweze kufanya vizuri kwenye michezo yake iliyobakia ya kufuzu michuano ya Kombe la dunia 2014. Hivi karibuni Stars ilifanikiwa kuitandika Morocco mabao 3-1 hivyo kufanikiwa kujiweka katika nafasi nzuri kwenye kundi C walilopo wakiwa na timu zingine za Ivory Coast na Gambia. Msimamo wa kundi hilo mpaka sasa Stars wako katika nafasi ya pili wakiwa na point sita, nyuma ya vinara Ivory Coast wanaoongoza kwa alama saba na Morocco ni ya tatu wakiwa na alama mbili wakati Gambia wao wanashikilia mkia wakiwa na alama moja. Kutokana na matokeo hayo wizara kupitia waziri wake Fenela Mukangara wameipongeza timu hiyo kwa kuweka matumaini hai ya kufuzu michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika nchini Brazil 2014. na kwa kuzingatia hilo wizara imeamua kuunda kamati maalumu kwa ajili ya kuongeza hamasa ya ushindi kwa Stars ili iweze kuweka historia kwa kushiriki michuano ya Brazil. Jukumu la msingi la Kamati iliyoundwa ni kuhakikisha Taifa Stars inawezeshwa na kuandaliwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuunda kikundi cha kuishangilia timu ya Taifa ndani na nje ya nchi.star kwa sasa katika viwango vya fifa ipo katika nafasi ya 116

Wajumbe wa Kamati ya Taifa Stars Stars itakayoongozwa na Mhe. Mohamed Dewji ni hawa wafuatao:-


Mhe Mohamed Dewji - Mbunge
Bi. Teddy Mapunda - Montage
Dkt. Ramadhani Dau - Mkurugenzi Mtendaji NSSF
Bw. Dioniz Malinzi - Mwenyekiti BMT
Bw. Abji Shabir - New Africa Hotel
Bw. George Kavishe - TBL
Mhe. Mohamed Raza - Zanzibar
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Bw. Joseph Kusaga - Clouds
Mhe. Kapt. John Komba - Mbunge
Mhe. Zitto Kabwe - Mbunge
Kamati hiyo iliyoteuliwa leo, inatakiwa kuanza kazi kazi mara moja. Hadidu za rejea zitakazowaongoza kutekeleza majukumu yao chini ya Kamati hii watazipata kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo. Kamati itashirikisha wadau mbalimbali kadri itakavyoona inafaa. Serikali inaahidi kutoa ushirikiano utakaohitajika katika kuhakikisha Kamati hii inafanya kazi vizuri ili kuiwezesha Taifa Stars kushinda Mechi zote zilizombele yetu.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TFF_LOGO12Aprili 16, 2013
RAMBIRAMBI MSIBA WA MEJA JENERALI MAKAME RASHID
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko za kifo cha Mkuu wa zamani wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Makame Rashid kilichotokea juzi (Aprili 14 mwaka huu) kutokana na maradhi jijini Dar es Salaam.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kutokana na mchango aliotoa Meja Jenerali Makame Rashid ikiwemo kuwa mlezi wa timu ya Ruvu Stars wakati huo akiwa Kamanda (CO) wa Kikosi cha Ruvu JKT.
Pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mdhamini (Trustee) wa TFF wakati huo ikiitwa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) na wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya katika miaka ya themanini alikuwa sehemu ya mafanikio kwa timu ya Tukuyu Stars ya Mbeya iliyotwaa ubingwa wa Tanzania Bara mwaka 1987 ikiwa ndiyo kwanza imepanda kucheza Ligi Kuu wakati huo ikiitwa Ligi Daraja la Kwanza.
TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Meja Jenerali Makame Rashid, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Maziko yanatarajiwa kufanyika leo (Aprili 16 mwaka huu) nyumbani kwao mkoani Mtwara. Mungu aiweke roho ya marehemu Sembwana mahali pema peponi. Amina
VPL KUTIMUA VUMBI VIWANJA VITATU
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Aprili 17 mwaka huu) kwenye viwanja vitatu huku vinara wa ligi hiyo Yanga wakifukuzia ubingwa huo jijini Tanga.
Yanga inayoongoza ligi ikiwa na pointi 52 itakuwa mgeni wa Mgambo Shooting katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Athuman Lazi kutoka Morogoro kwenye Uwanja wa Mkwakwani. Waamuzi wasaidizi wa mechi hiyo ni Michael Mkongwa wa Iringa na Godfrey Kihwili wa Arusha wakati Kamishna wa mechi hiyo ni Godbless Kimaro kutoka Moshi.
Kagera Sugar na Toto Africans zitaumana kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba katika mechi namba 164 itakayokuwa chini ya mwamuzi Martin Saanya wa Morogoro.
Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro, na wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 4,000 utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mtibwa Sugar yenye pointi 33 na Oljoro JKT yenye pointi 28.
Israel Nkongo kutoka Dar es Salaam ndiye atakayechezesha mechi hiyo akisaidiwa na Hamis Chang’walu (Dar es Salaam) na John Kanyenye (Mbeya). Kamishna wa mechi hiyo ni Ramadhan Mahano kutoka Iringa.
AS FAR KUWASILI KESHO KUIKABILI AZAM
Wapinzani wa Azam katika michuano ya Kombe la Shirikisho, AS FAR Rabat ya Morocco wanatarajiwa kutua nchini kesho (Aprili 17 mwaka huu) saa 7 mchana kwa ndege ya Emirates.
Msafara wa timu hiyo wenye watu 28 utafikia hoteli ya Sapphire iliyoko maeneo ya Kariakoo, Dar es Salaam tayari kwa mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili itakayochezwa Jumamosi (Aprili 20 mwaka huu) saa 10 kamili jioni Uwanja wa Taifa.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)