Tuesday, December 2, 2014

MANDAWA MCHEZAJI BORA WA VPL NOVEMBA

Mshambuliaji wa timu ya Kagera Sugar ya mkoani Kagera amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kwa mwezi Novemba mwaka huu ambapo atazawadiwa kitita cha sh. milioni moja.
Mandawa ambaye kwa mwezi huo alichuana kwa karibu na mshambuliaji Fulgence Maganda wa Mgambo Shooting ya Tanga na nahodha wa Simba, Joseph Owino atakabidhiwa zawadi yake na wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya Vodacom.

Hafla ya kukabidhi zawadi hiyo inatarajiwa kufanyika wakati wa mechi ya raundi ya nane ya ligi hiyo kati ya Simba na Kagera Sugar itakayochezwa Desemba 26 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
KOZI YA UKUFUNZI WA UTAWALA YA FIFA SASA MACHI.
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limesogeza mbele kozi ya ukufunzi ya utawala wa mpira wa miguu iliyokuwa ifanyika Desemba mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa FIFA, kozi hiyo sasa itafanyika Machi mwakani katika tarehe itakayotangazwa baadaye.

TFF imepokea maombi ya zaidi ya washiriki 40 kwa ajili ya kozi hiyo itakayoshirikisha washiriki 30. Kutokana na maombi kuzidi idadi ya nafasi zilizopo, FIFA itafanya mchujo wa washiriki.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

MIKOA MITANO YATAKIWA KUWASILISHA USAJILI COPA 2014

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeitaka mikoa mitano kuwasilisha usajili wa wachezaji wake kwa ajili ya mashindano ya Taifa ya Copa Coca-Cola 2014 kabla ya Desemba 5 mwaka huu.

Mikoa hiyo ambayo haijawasilisha usajili wake hadi sasa kwa ajili ya michuano hiyo inayoanza Desemba 13 mwaka huu jijini Dar es Salaam ni Arusha, Dodoma, Katavi, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Mjini Magharibi na Simiyu.

Kwa mujibu wa Kamati ya Mashindano ya michuano hiyo, mkoa ambao hautawasilisha usajili wake kwa ajili ya uhakiki wa umri wa wachezaji utakaonza Desemba 10 mwaka huu utaondolewa katika fainali hizo zitakazomalizika Desemba 20 mwaka huu.

Wachezaji watakaobainika kuzidi umri hawataruhusiwa kushiriki katika michuano hiyo inayoshirikisha wachezaji wenye umri chini ya miaka 15. Kwa mujibu wa Kanuni ya 29 ya michuano kuhusu idadi ya wachezaji, kila timu inatakiwa kuwa na wachezaji wasiozidi 20 na wasiopungua 16.

Hivyo, kila timu inatakiwa kuhakikisha inakuwa na idadi hiyo ya wachezaji, kwani kikanuni wakipungua 16 itaondolewa kwenye mashindano.

Timu 16 kwa upande wa wavulana zitashiriki katika fainali hizo wakati kwa upande wa wasichana ni timu nane. Mikoa iliyoingiza timu za wasichana kwenye fainali hizo ni Arusha, Dodoma, Ilala, Kinondoni, Mbeya, Mwanza, Temeke na Zanzibar.

CAF YAWEKA HADHARANI MAJINA YA TIMU SPECHO KWA DROO KUPANGWA.

WASHIRIKI 16 wa Fanali za Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON 2015, ambazo zitachezwa huko Nchini Equatorial Guinea kuanzia Januari 17, watajua nani Wapinzani kwenye Makundi yao Leo Jumatano makundi ya Timu 4 kila moja kutajwa kwa ajili ya Droo hiyo na CAF.
Droo hiyo itafanyika Mjini Malabo Nchini Equatorial Guinea.
Timu hizo 16 zimepangwa kwenye Vyungu Vinne vya Timu 4 kila moja na kwenye Droo kila Chungu kitatoa Timu moja ili kupanga Makundi Manne.
CHUNGU 1
Equatorial Guinea, Ghana, Zambia, Burkina Faso
CHUNGU 2
Ivory Coast, Mali, Tunisia, Algeria
CHUNGU 3
Cape Verde, South Africa, Gabon, DR Congo
CHUNGU 4
Cameroon, Senegal, Guinea, Congo

POLISI MORO NA MWADUI FC ZAMTOLEA MACHO KINDA MIRAJI ADAM LA SIMBA

Timu Polisi ya Morogoro na Mwadui FC ya Shinyanga zimewasilisha barua kumuomba beki wa pembeni Miraj Adam wa Simba SC kwa mkopo baada ya kushushwa Simba B.
Polisi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania inapambana na Mwadui FC, inayopigania kupanda Ligi Kuu pia kuwania huduma za beki huyo aliyetokea timu ya vijana ya Wekundu hao wa Msimbazi.
Mwadui wanaamini wanaweza kumpata kwa urahisi beki huyo kwa sababu ya mahusiano mazuri ya kocha wao, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na klabu ya Simba SC.
Lakini Polisi nayo inaamini inaweza kumpata kwa urahisi beki huyo wa kulia, Miraj, kwa sababu inacheza Ligi Kuu kwa sasa na Morogoro si mbali sana na Dar es Salaam anakoishi mchezaji huyo.

Kwa sasa, Miraj ameshushwa kikosi cha pili baada ya mechi saba za awali za Ligi Kuu, lakini Simba SC bado haijaamua kumtoa kwa mkopo hadi hapo itakapofanikisha kusajili mchezaji mwingine wa nafasi hiyo.

VITA KALI YA BALLON D"OR MESS VS RONALDO VS NEUER JAN 12/2015.

SHIRIKISHO la Soka Duniani-FIFA limetangaza orodha ya wachezaji watatu watakaogombea tuzo ya mchezaji ya mchezaji bora wa mwaka wa dunia maarufu kama Ballon d’Or. 
Wachezaji hao watatu waliopenya katika mchujo wa wachezaji 23 ni pamoja na nyota wa kimataifa wa Ureno na klabu ya Real Madrid Cristiano Ronaldo, Lionel Messi wa Argentina na klabu ya Barvelona na Manuel Neuer kutoka Ujerumani na timu ya Bayern Munich.
Sherehe za utoaji tuzo inatarajiwa kufanyika Januari 12 mwakani huku Ronaldo akiwa ndio mshindi wa mwaka jana. Kwa upande wa wanawake walioteuliwa kugombea tuzo hiyo ni pamoja na Nadine Kessler wa Ujerumani, Marta wa Brazil na Abby Wambach kutoka Marekani. 
Kwa upande wa makocha walioteuliwa kugombea tuzo ni pamoja na Carlo Ancelotti wa Real Madrid, Joachim Loew aliyeiwezesha Ujerumani kunyakuwa Kombe la Dunia na kocha wa Atletico Madrid Diego Simeone.