Wednesday, September 3, 2014

AZAM FC KIBOKO, AISHI MANULA AITWA TAIFA STARS AZAM KUWA NA WACHEZAJI 10 TAIFA

Mlinda mlango Chipukizi wa Azam FC AISHI MANULA ameongezwa katika kikosi cha wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' inayojiandaa kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Burundi tarehe 7 September 2014. Sasa Azam FC ina jumla ya wachezaji 10 katika kikosi cha Stars ambao ni

1.MWADINI ALI
2. SHOMARI KAPOMBE 
3. ERASTO NYONI 
4. SAID MORAD 
5. AGGREY MORIS 
6. HAMIS MCHA 
7. HIMIDI MAO 
8. SALUM ABUBAKAR 
9. JOHN BOCCO 
10. AISHI MANULA 


NMB YAIPA SHAVU MKATABA WA KUIDHAMINI AZAM FC MIAKA MIWILI

BENKI ya NMB imejitia kitanzi mkataba wa udhamini wa miaka miwili na mabingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara, Azam fc, utaohusisha gharama za usafiri na baadhi ya nyingine za uendeshaji wa timu.
Mwenyekiti wa Azam fc, Said Muhammad Said amewaambia waandishi wa habari leo makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo, Azam Complex, Mbande, Chamazi, nje ya jiji la Dar es salaam kuwa mkataba huo utaanza utekelezaji mara moja.
“Tumeupokea kwa furaha mkataba huu na tunapenda kuwashukuru NMB kwa kuungana nasi”. Alisema Said.
Naye katibu mkuu wa Azam fc, Nassor Iddrisa ‘Father’ alifafanua kuwa NMB watanufaika na mkataba huo kwa kutangaza nembo yao katika jezi za Azam fc, mabasi ya Azam fc na kuweka mabango katika uwanja wa Azam Complex.
Pia Azam watavaa jezi zenye nembo ya NMB kuanzia mazoezini na katika mechi za ligi kuu na mashindano ya kimataifa.
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa NMB, Mark Weissing amesema mafanikio ya Azam fc ndio chachu ya kuingia ushirikiano na timu hiyo.
Azam fc inakuwa timu ya pili kuingia mkataba na taasisi ya kifedha nchini ambapo timu ya kwanza ni Simba ambayo iliingia mkataba na NMB mwaka 2004, lakini 2004 walitemana.
Pia NMB iliwahi kuidhamini timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa stars kati ya mwaka 2007 na 2010 ikiwa chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo ambaye kwasasa ni kocha mkuu wa Yanga sc.
Wakati wa utiaji saini wa mkataba baina ya Azam fc na NMB, watu wengi walikuwa na hamu ya kujua una thamani gani.

Hata hivyo viongozi wa Azam fc waligoma kutaja thamani ya mkataba huo, lakini taarifa za uhakika zinasema mkataba huo unakadiriwa kuwa na thamani ya shilingi za Kitanzania Bilioni 1.
Imeelezwa kuwa kwa kila mwaka Azam fc watanufaika na shilingi milioni 500 za Kitanzania kutoka NMB.
Tangu imeanzishwa mwaka 2004 ba kupanda ligi kuu 2008, Azam fc inapata mdhamini kwa mara ya kwanza .
Azam fc inakuwa miongoni mwa timu chache za Tanzania zinazonufaika na udhamini.
Simba na Yanga ndio timu pekee zilizokuwa zinanufaika na udhamini, kwa miaka mingi, lakini siku za karibuni Mbeya City walivuna milioni 360 kutoka kwa Binslum.
Udhamini ni moja ya vyanzo vya mapato kwa klabu za mpira wa miguu, lakini imekuwa changamoto kwa timu mbalimbali kufikia mafanikio ya kupata wadhamini.
Siku zote mdhamini anawekeza sehemu anayoweza kunufaika, hivyo sio rahisi kuweka fedha kwenye timu yenye kiwango kibovu.
Kilio cha kukosa udhamini kwa timu za ligi kuu kinasikika kila kukicha, lakini zimeshindwa kutegua mtego huo tofauti na Azam fc na Mbeya City.
Hakuna haja ya kulia kwa kukosa udhamini, ukiucheza mpira kwa nafasi uliyopata na kufanikiwa kama Mbeya City, Azam fc, Yanga, na Simba, mabilioni na mamilioni yatakuja yenyewe.
Mafanikio ya Azam fc yamewafanya walambe mabilioni kutoka NMB, na timu nyingine zinatakiwa kujipanga kwa kutafuta mafanikio uwanjani zaidi ya kulia kila wakati.

GOR MAHIA WATUA KESHO KUMPIMA PATRICK PHIRI NA SIMBA YAKE

WEKUNDU wa Msimbazi wanatarajia kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya mabingwa wa ligi kuu nchini Kenya, Gor Mahia siku ya jumamosi katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Geofrey Nyange ‘Kaburu’, makamu wa Rais wa Simba sc, amewaambia waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuwa kikosi cha Gor Mahia kitawasili kesho uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam kikitokea Nairobi kwa kutumia ndege ya shirika la Kenya.
Kaburu aliongeza kuwa nacho kikosi cha Simba kitawasili siku hiyo hiyo kikitokea Zanzibar kilipoweka kambi ya kujiwinda na ligi kuu.
Licha ya kukipiga na Simba, Gor Mahia imeomba kucheza mechi mbili, hivyo siku ya jumapili watakuwa na mechi nyingine ya kirariki wakati kikosi cha Patrick Phiri kitarejea Zanzibar kuendelea kumalizia program zake za maandalizi kabla ya ligi kuanza septemba 20 mwaka huu.
Awali Simba walipanga kuchuana na Mtibwa Sugar, lakini kocha Phiri akapendekeza kutafutiwa mechi ngumu ya kimataifa ili kuangalia namna kikosi chake kilivyoimarika.
Mechi ya jumamosi itakuwa fursa nzuri kwa mashabiki wa Simba kuwaona wachezaji wao akiwemo mshambuliaji hatari aliyerejea Msimbazi, Mganda Emmanuel Anord Okwi ambaye atavalia jezi yake namba 25 aliyokuwa anaitumia kabla ya kutimkia Etoile Du Sahel ya Tunisia.
Kaburu alisema viingilio katika mechi hiyo ni shilingi elfu 5 (5,000) kwa viti vya kijana, viti vya rangi ya chungwa ni shilingi 10,000, VIP C na B itakuwa shilingi 2,000 wakati VIP A itakuwa shilingi elfu 30,000.
Tiketi kwa ajili ya mchezo huo zitaanza kuuzwa siku ya mechi kuanzia majira ya saa 4:00 asubuhi.
Simba wataanza kampeni za kusaka ubingwa wa ligi kuu bara septemba 21 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam dhidi ya Coastal Union

MECHI YA NGAO YA JAMII BAINA YA YANGA NA AZAM FC WASOGEZWA MBELE

MECHI ya Ngao ya Jamii kuashiria kufunguliwa kwa pazia la ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2013/2014 baina ya mabingwa Azam fc na makamu bingwa, Dar Young Africans sasa utapigwa uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam septemba 14 badala ya septemba 13 mwaka huu kama ilivyopanga.

Shirikisho la soka Tanzania limeamua kuusogeza kwa siku moja mchezo huo uliotakiwa kupigwa jumamosi na sasa kupigwa jumapili kwa lengo la kuwapa fursa mashabiki wengi kuuona.
TFF  imesema jumapili ni siku tulivu kuliko jumamosi na mchezo wa mwaka huu utaambatana na shughuli za kijamii ikiwemo uchangiaji wa damu.
Pia sehemu ya mapato ya mchezo huo yatapelekwa katika shughuli ya kijamii iliyochaguliwa.
Mechi hiyo itapigwa ikiwa ni wiki moja kabla ya kuanza kwa ligi kuu septemba 20 mwaka huu ambapo Yanga wataanzia ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar katika dimba la Jamhuri mkoani Morogoro.
Mnyama Simba atakuwa uwanja wa Taifa siku moja baada ya kufunguliwa kwa ligi kuu (septemba 21 mwaka huuu) dhidi ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union.
Azam fc watakuwa nyumbani Azam Conmplex kuchuana na Polisi Morogoro