Wednesday, November 5, 2014

REAL MADRID,DORTMUND ZATINGA HATUA YA 16 BORA UEFA

Michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Uefa hatua ya makundi iliendelea tena jana huku tukishuhudia klabu mbili za Borussia Dortmund na Real Madrid zikifanikiwa kutinga hatua inayofuata ya timu 16 bora. Dortmund wanaonolewa na Jurgen Klopp pamoja na kusuasua katika Bundesliga lakini katika michuano hiyo wamekuwa wakionyesha kiwango kizuri baada ya kuigaragaza Galatasaray kwa mabao 4-1 hivyo kuwa wameshinda mechi zao zote nne katika kundi D.
Madrid wao wametinga hatua hiyo baada ya kuikabili Liverpool na kuitandika bao 1-0 katika Uwanja wa Santiago Bernabeu na kufikisha alama 12 katika kundi B mbele ya FC Basel waliopo nafasi ya pili ambao nao waliichapa Ludogorets Razgrad kwa mabao 4-0.
Kwa upande mwingine ushindi wa mabao 2-0 waliopata Atletico Madrid dhidi ya Malmo umewapaisha mpaka kileleni mwa kundi A huku Olympiakos wakiwa nafasi ya pili pamoja na kutandikwa na Juventus kwa mabao 3-2. Kundi C Bayer Leverkusen wamejiimarisha kileleni baada ya kuibuka na ushindi wa ugenini wa mabao 2-1 dhidi ya Zenit Saint Petersburg, Benfica wao walifufua matumaini yao ya kusonga mbele baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Monaco. Arsenal wao wameendelea kushika nafasi ya pili nyuma ya Dortmund baada ya kushindwa kulinda ushindi wake na kujikuta wakitoa sare ya mabao 3-3 na Anderletch katika Uwanja wa Emirates.

BARAZA LA MITIHANI LA TAIFA NEKTA LATANGAZA MATOKEO YA DARASA LA 7 UFAULU WAONGEZEKA.

BARAZA la mitihani la taifa Nekta, limetangaza matokeo ya mitihani ya darasa la saba mwaka huu, ambapo kiwango cha ufaulu kimeongezeka kutoka asilimia 50 nukta sita moja ya mwaka jana hadi kufikia asilimia 56, nukta tisa, tisa mwaka huu.
Akitangaza matokeo hayo jijini Dar-es-Salaam katibu mtendaji wa Nekta Dokta Chazi Msonde amesema shule za kanda ya ziwa zinaongoza ambapo shule nane kati ya kumi bora zinatoka kanda hiyo, huku mbili zilizosalia ni kutoka mkoa wa Dar-es- Salaam na Kilimanjaro.
Watahiniwa waliofanya mitihani ya kumaliza elimu ya msingi mwaka huu walikuwa ni zaidi ya laki saba na 92, elfu sawa na asilimia 98, ya watahiniwa waliosajiliwa kufanya mitihani hiyo.

WAZIRI NYALANDU ASEMA VITENDO VYA UJANGILI VISIPODHIBITIWA TAIFA LITAANGAMIA.

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema vitendo vya ujangili dhidi ya wanyama wakiwamo tembo, mbali na kuonekana kupungua nchini, lakini kasi yake isipodhibitiwa, taifa  litaangamia.
Waziri Nyalandu ametoa tahadhari hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa kitaifa uliowashirikisha viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini na wadau wa maendeleo kuhusu kujadili namna ya kudhibiti uharibifu dhidi ya rasilimali za nchi zikiwamo wanyama na misitu, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Waziri Nyalandu,amesema  kukithiri kwa vitendo hivyo kunachangiwa na madai ya kuongezeka kwa soko haramu la rasilimali za nchi zikiwamo nyara za serikali katika nchi za Vietnam, Japan, Korea, China na Thailand.
Hata hivyo Nyalandu amewataka  watu wote wanaomiliki silaha kinyume na sheria zikiwamo silaha aina ya gobore, kuzisalimisha haraka kwa hiari, vinginevyo watakumbwa na operesheni ya nyumba kwa nyumba na kuwalazimu wahusika kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

SIMBA IPO MBIONI KUMLETA KOCHA KIM POULSEN MSIMBAZI

Simba imeamua kufanya mabadiliko tena katika benchi la ufundi na nguvu zimeelekezwa kwa Kocha Mdenishi,  Kim Poulsen.
Poulsen raia wa Denmark katika nafasi ya Mzambia Patrick Phiri ambaye timu yake imecheza mechi sita mfululizo na kutoka sare zote.Simba imeingia kwenye harakati za kumng’oa Phiri ambaye ameingoza Simba katika mechi sita tu za Ligi Kuu Bara na zote ametoka sare. Simba imefunga mabao sita, imefungwa sita na ina pointi sita.
Mdenishi Poulsen ambaye yuko kwao nchini Denmark baada ya kuzinoa timu za taifa za vijana na baadaye Taifa Stars, aliondolewa kwenye kiti chake baada ya kuingia kwa uongozi wa Jama Malinzi.Habari za uhakika kimesema kuwa Simba wamefanya mazungumzo na Poulsen na kukubaliana kila kitu na yuko tayari kucha nchini wakati wowote.
Lakini kumekuwa na suala la Phiri kidogo limekuwa likiwagawanya kwa baadhi ya wajumbe wa kamati ya utendaji kutaka apewe mechi ya mwisho ambayo itakuwa ni dhidi ya Ruvu shooting  kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, Jumapili.
Hivyo wanachosubiri huenda kikawa ni mechi ya Jumamosi na kama si mechi hiyo, basi angekuwa ameishatua,” kilifafanua chanzo.
Iwapo Simba itashikilia msimamo wake wa kumleta Poulsen, basi lazima itaendelea na rekodi yake ya kuwa tim iliyofukuza makocha wengi zaidi kwa misimu mitatu mfululizo.
Katika misimu miwili iliyopita, Simba ilifundishwa na makocha wanne tofauti, kila mmoja akifundisha nusu msimu ambao ni Abdallah Kibadeni Mputa,Patric liewing,Logarusic na huyu Patric Phiri
Source: Champion

PATRICK LIEWING KUTUA AZAM FC NOV 17 MWAKA HUU

Aliekuwa Kocha wa simba Patrick Liewig amekubaliana kila kitu na uongozi wa Azam FC na anatarajia kutua nchini Novemba 17, mwaka huu.
Azam FC imeamua kuboresha benchi lake la ufundi baada ya kuondokewa na kocha wake Vivek Nagul ambaye amepata ulaji kwao India.
Liewig raia wa Ufaransa anatarajia kutua nchini na ndege ya Shirika la Ndege la Qatar akitokea kwao Ufaransa.
Habari za uhakika kutoka kwa rafiki wa Liewig aishiye katika jiji la Paris, Ufaransa amesema kocha huyo amemhakikishia kuwa anakuja nchini.
Chanzo hicho kimeeleza, Liewig angeweza kutua nchini mapema lakini alikwama kutokana na mkewe kuwa mgonjwa.
Liewig alikuwa kocha wa Simba msimu uliopita. Lakini uongozi wa Ismail Aden Rage ukamuondoa na nafasi yake ukampa Abdallah Kibadeni ambaye hata hivyo hakudumu zaidi ya nusu msimu.

RIPOTI ZINAONYESHA KUWA TFF ILIMLIPA KIM MILLION 153

Ripoti ya ukaguzi wa mahesabu ya kampuni binafsi (jina limehifadhiwa), imeonyesha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitoa kitita cha dola 90 (Sh milioni 153) kumlipa Kocha Kim Poulsen.
TFF ililazimika kumlipa Poulsen kutokana na uamuzi wake wa kuvunja mkataba na ripoti hiyo ya ukaguzi wa fedha imeeleza hivyo.
Poulsen alikubali kuondoka baada ya kutaka kulipwa kutokana na mkataba wake lakini bado hakuna uhakika kama kweli alilipwa kiasi hicho kikubwa cha fedha kwa ajili ya kuvunja mkataba.
Nafasi ya Mdenishi huyo, imechukuliwa na Mart Nooij raia wa Uholanzi ambaye tokea aanze kuinoa Stars, pia hakuna mabadiliko makubwa ukilinganisha na yale ya Poulsen.
Mara kadhaa, TFF wamekuwa wakisisitiza kutotaka kuizungumzia mikataba kwa madai kuwa ni siri kati yao na mhusika. Hata hivyo fedha hizo nyingi kwa ajili ya kuvunja tu mkataba, zinatia hofu.
Ripoti hiyo ya ukaguzi wa mahesabu ya udhamini kati ya TFF na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), imeonyesha kuna uchakachuaji mkubwa wa fedha.
Baadhi ya matatizo ni pamoja na kununuliwa kwa magari mawili aina ya Toyota Hiace ambaye wakaguzi hawakuyaona na moja halina hata jina la TFF na badala yake linamilikiwa na mtu aitwaye Juma Shariff.
Chanzo:Saleh Jembe

NOOIJ AITA 24 STARS KUIKABILI SWAZILAND

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij ametangaza kikosi cha wachezaji 24 kwa ajili ya mechi ya kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) dhidi ya Swaziland itakayochezwa Novemba 16 mwaka huu jijini Mbabane.
 
Akizungumza Dar es Salaam, leo (Novemba 5 mwaka huu), Nooij alisema kikosi hicho kitaingia kambini Novemba 10 mwaka huu saa 6 mchana kwenye hoteli ya Accomondia, na siku hiyo hiyo jioni kitafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Gymkhana.
 
Novemba 11 mwaka huu, Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itaondoka kwenda Afrika Kusini ambapo itaweka kambi ya siku mbili kabla ya kuondoka Novemba 13 mwaka huu kwenda Swaziland.
 
Wachezaji walioitwa kwenye kikosi hicho ni makipa Aishi Manula (Azam) na Deogratias Munishi (Yanga). Mabeki ni Abubakar Mtiro (Kagera Sugar), Aggrey Morris (Azam), Emmanuel Simwanda (African Lyon), Hassan Isihaka (Simba), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Osacr Joshua (Yanga), Said Moradi (Azam), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar) na Shomari Kapombe (Azam).
 
Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Haruna Chanongo (Simba), Himid Mao (Azam), Mwinyi Kazimoto (Al Markhiya, Qatar), Said Ndemla (Simba) na Salum Abubakar (Azam).
 
Washambuliaji ni Juma Luizio (ZESCO, Zambia), Mbwana Samata (TP Mazembe, DR Congo), Mrisho Ngasa (Yanga), Simon Msuva (Yanga) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DR Congo).
 
WADAU KUBUNI JEZI MPYA YA TIMU ZA TAIFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linakaribisha wabunifu, kubuni mwonekano wa jezi mpya za timu ya Taifa kwa mechi za nyumbani na ugenini. Ubunifu ni lazima uzingatie rangi za bendera ya Taifa.
*       
Mshindi wa jezi ya nyumbani atapata sh. 1,000,000 (milioni moja), na mshindi wa jezi ya ugenini atapata pia sh. 1,000,000 (milioni moja).
 
Ubunifu utumwe kwenye anwani ya barua pepe: info@tff.or.tz au uwasilishwe kwa CD au flash zikiwa katika mfumo wa PDF katika ofisi za TFF zilizopo ghorofa ya tatu katika Jengo la PPF Tower, Mtaa wa Ohio na Garden Avenue. Mwisho wa kupokea designs ni Novemba 15, 2014.
 
Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana nasi kwa simu namba; 0713 210242 au 0714 634838.
 
MPANDA UTD, UJENZI RUKWA KUANZA SDL
Michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL) inayoshirikisha timu 24 katika makundi manne ya timu sita sita kwa mtindo wa nyumbani na ugenini inaanza kutimua vumbi Novemba 22 mwaka huu ambapo Mpanda United itakuwa mwenyeji wa Ujenzi Rukwa.
 
Mechi hiyo ya kundi A itachezwa kwenye Uwanja wa Mandela mjini Sumbawanga. Siku hiyo hiyo katika kundi hilo kutakuwa na mechi kati ya Mvuvumwa FC na CDA (Lake Tanganyika, Kigoma), na Milambo dhidi ya Singida United kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
 
Kundi B mechi za ufunguzi ni kati ya Pamba na JKT Rwamkoma kwenye Uwanja wa CCM Kirumba huku Bulyanhulu FC ikiwa mwenyeji wa AFC kwenye Uwanja wa Bulyanhulu mkoani Shinyanga.
 
Abajalo FC ya Dar es Salaam itaikaribisha Kariakoo FC ya Lindi kwenye mechi ya kundi C itakayochezwa Uwanja wa Karume. Nazo Kiluvya United na Transit Camp zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Mabatini uliopo Mlandizi mkoani Pwani.
 
Kundi D mechi tatu za ufunguzi ni kati ya Town Small Boys na Volcano FC (Uwanja wa Majimaji, Songea), Njombe Mji na Mkamba Rangers (Uwanja wa Sabasaba, Njombe), na Wenda FC dhidi ya Magereza Iringa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
 
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF