1.Kama wote tunavyofahamu jana uongozi wangu
wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ulifikia
tamati kama mlivyotangaziwa na Rais wa TFF. Kwa heshima kubwa naomba kutumia
fursa hii kuwashukuru viongozi na wadau wa soka kwa ushirikiano mkubwa
nilioupata kutoka kwao wakati nikitekeleza majukumu mbalimbali ya TFF.
2. Kwa kushirikiana na viongozi wa mpira wa miguu
katika TFF na mikoa yote Tanzania Bara, pamoja na wadau wa soka, nimepata fursa
kulitumikia soka la nchi yetu kwa nafasi mbalimbali. Kwa pamoja tumetekeleza
majukumu ya ujenzi wa misingi ya uongozi bora katika TFF na wanachama wake.
3.Naishukuru Kamati ya Utendaji ya TFF:
(i)kwa kuniteua kuwa mjumbe wa Kamati ya Nidhamu
ya TFF, (Jan 2005 - Jan 2007). Nawashukuru pia wajumbe wa Kamati hiyo chini ya
Mhe. Said El-Maamry kwa kunichagua kuwa Katibu wa Kamati hiyo. Ushirikiano
mlionipatia ulioniwezesha kulitumikia taifa katika soka na kwa pamoja kurejesha
nidhamu kwa kiwango kikubwa. (ii)kwa kuniteua kuwa mjumbe wa Kamati Maalumu,
iliyochunguza mkasa wa timu yetu ya Taifa ya wachezaji wa umri chini ya miaka
17 (Serengeti Boys) mwezi Juni 2005. Nawashukuru wajumbe wa kamati hiyo
chini ya Dr. Hamad Ndee Mkuu wa Idara ya Michezo ya Chuo kikuu cha Dar es
salaam, kwa kunichagua kuwa Katibu wa kamati hiyo iliyoandaa taratibu za
mashindano ya vijana ambazo ni msingi wa mashindano ya vijana wa
umri chini ya miaka 17 hapa nchini.
(iii)kwa kuniteua kuwa Mjumbe wa Kamati Maalumu
iliyotayarisha Programu ya kuendeleza Timu ya Taifa kwa kipindi cha miezi 15
(April 2006 hadi Juni 2007). Progamu iliyochangia Tanzania kiinua kiwango cha
ubora wa soka kutoka nafasi ya 165 duniani mwezi Februari 2006 hadi nafasi ya
89 mwezi Desemba 2007.
(iv)kwa kunipa fursa ya kuwa mjumbe wa Kamati
Maalumu ya kuboresha mapato ya TFF mwaka 2009. Nikiwa mjumbe na Katibu wa
Kamati hiyo nilipata ushurikiano mkubwa kutoka kwa wadau wa soka nchini
na nje ya nchi. Nina imani kuwa TFF itakamilisha utekelezaji wa
mapendekezo ya Kamati na ya wadau wa soka ikiwa ni pamoja na kuanza kutumia
tiketi za elektroniki.
(v)kwa kuniteua kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa
vipindi viwili; Februari 2009 - Machi 2011 na kuniteua tena kuiongoza
Kamati hiyo kwa kipindi cha pili Machi 2011 hadi jana tarehe 18 Julai 2013.
Naishukuru Kamati ya Utendaji ya TFF kwa imani kubwa iliyoonyesha kwangu na
wanakamati wenzangu.
4.Nawashukuru wajumbe wote wa wa Mkutano Mkuu
wa TFF, kwa ushirikiano mkubwa mliotoa kwangu na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa
kushiriki kwa amani na utulivu na kuzingatia Katiba za vyama vyenu, Katiba ya
TFF na Kanuni za Uchaguzi na hivyo kufanikisha zoezi la chaguzi za viongozi
katika wilaya zote na Mikoa yote ya Tanzania Bara na hivyo kuwezesha kuwa na
wajumbe wa Mkutano Mkuu, ambao katika kikao chake cha kwanza baada ya
chaguzi hizo kimefanya jambo la kihistoria kuweka nguzo za Mwenendo,
Maadili na Miiko ya uongozi wa soka la nchi yetu. Nilifarijika kuwa sehemu ya Mkutano Mkuu huo nikiwa mwalikwa.
5.Nawashukuru viongozi na wafanyakazi
wote wa Sekretarieti ya TFF, wajumbe wa Kamati zote za TFF, Wajumbe wa Kamati
zote za Uchaguzi za wanachama wa TFF na wanachama wao, kwa ushirikiano mkubwa
na wa dhati uliowezesha kuwatumikia wadau wa soka kwa kuzingatia taratibu
zilizowekwa.
6.Nawashukuru sana wajumbe wa Kamati
ya Uchaguzi ya TFF kwa ushirikiano niliopata kutoka kwao kwa muda tuliofanya
kazi pamoja. Si jambo rahisi kusimamia chaguzi za mikoa yote na klabu zenye
wanachama za Ligi Kuu, hata hivyo kwa kushirikiana na wadau mbalimali wa soka
ambao nachukua fursa hii kuwashukuru, kwa pamoja tumeweza kutimiza jukumu hilo
kikamilifu.
7.Nawashukuru sana Wandishi na Wahariri wa
habari za michezo na pia Wahariri Watendaji wa vyombo vya habari, kwa
ushirikiano mzuri nanyi, ushirikiano na uhusiano wa uwazi ambao haukuwa na
mikwaruzo ya aina yoyote kwa kipindi chote (Jan 2005-Jul 2013)
tulichoshirikiana kwa pamoja kulitumikia soka la nchi yetu.
8.Namshukuru sana Rais wa TFF Ndg. Leodegar Tenga kwa imani kubwa aliyonayo kwangu na kwa
wanakamati niliokuwa nao katika kutekeleza majukumu ya umma. Miaka ishirini na
tisa (29) iliyopita nilipata fursa ya kufanya kazi ya mpira miguu kwa mara ya
kwanza na Ndg. Tenga, nikiwa nahodha wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Chuo kikuu
cha Dar es salaam, Desemba 1984, wakati Ndg. Tenga alipojitolea kuifundisha
timu ya Chuo Kikuu cha DSM. Tangu wakati huo hadi sasa imani na
ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya umma niliopata kutoka kwa Ndg.
Tenga haujawai kutetereka hata kwa siku moja. Ni faraja kubwa kwangu kufanya
kazi hizi za umma chini ya kiongozi anayeheshimika na kuaminika na wadau wa
soka hapa nchini, Afrika Mashariki na Kati, Afrika na familia ya soka Duniani
kwa ujumla.
9.Mwisho, kwa viongozi na wadau wote wa mpira wa
miguu, nawashukuru na nawatakia kheri, baraka na mafanikio katika
Uchaguzi Mkuu wa TFF na ujenzi wa soka la nchi yetu..
Asanteni.
Deogratias J. Lyatto
19 Julai 2013, Dar es salaam, Tanzania.