Sunday, June 15, 2014

STARS KWENDA BOTSWANA JUNI 24 KUJIWINDA DHIDI YA MSUMBIJI.

TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inatarajiwa kuondoka nchini wiki ijayo kwenda Botswana kuweka kambi ya mwezi mmoja kujiandaa na mchezo dhidi ya Msumbiji kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani Morocco.
Wachezaji wote wa Taifa Stars waliruhusiwa kurejea makwao jana kwa ajili ya kujiandaa na safari hiyo na watakutana tena kesho.
 Stars inayofundishwa na Mholanzi, Mart Nooij itaondoka nchini Juni 27 kwenda Gaborone, ambako itaweka kambi ya mazoezi hadi Julai 7 itakaporejea nchini.  
Taifa Stars itamenyana na Msumbiji ‘Mambas’ katika hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco baada ya kuitoa Zimbabwe juzi kwa jumla ya mabao 3-2, ikianza kwa ushindi wa 1-0  nyumbani na kumaliza kwa sare ya 2-2 juzi mjini hapa.
Mechi yake kwanza itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Julai 19 na 20 mwaka huu, wakati mechi ya marudiano itafanyika Msumbiji kati ya Agosti 2 na 3 mwaka huu. 
Stars pia inatarajiwa kuwa na mchezo wa kujipima nguvu na Uganda kabla ya kumenyana na Msumbiji.

TFF YASIMAMISHA UCHAGUZI SIMBA YAITAKA UENDE KAMATI YA MAADILI.



RAIS wa TFF, Jamal Malinzi, ametangaza kusimamishwa Uchaguzi Mkuu wa Simba hadi Klabu hiyo itakapounda Kamati ya Maadili kwa mujibu wa Katiba ya TFF.
Uchaguzi Mkuu Simba ulipangwa kufanyika Juni 29 na uamuzi huu wa TFF uliotangazwa Leo kwenye Mkutano wake na Wanahabari unaitaka Simba kuunda Kamati ya Maadili ifikapo Juni 30 na Kamati hiyo ndio itakayoshughulikia masuala yote ya Maadili kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu.
Uamuzi huu wa TFF unaendelea kumweka Madarakani Mheshimiwa Ismail Aden Rage hadi hapo Uchaguzi utakapofanyika baada ya Katiba yao kurekebishwa na kujumuisha Kamati ya Maadili.
Uchaguzi wa Simba umekumbwa na vuta nikuvute Klabuni hasa baada ya Mgombea Michael Wambura kuenguliwa kugombea Urais na Kamati ya Uchaguzi ya Simba na yeye kukata Rufaa TFF ambako Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF, chini ya Mwenyekiti wake Wakili Julius Lugaziya, ilimpitisha na kuamua aruhusiwe kugombea.
Hivi karibuni, Yanga walipitisha uundwaji wa Kamati ya Maadili ya Klabu yao ili kutii amri ya TFF kwenye Mkutano Mkuu wao huko Bwalo la Polisi –Oysterbay, Jijini Dar es Salaam.
Lakini hatua hiyo ililazimu Mkutano huo kumwongezea muda wa Mwaka mmoja Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Yusuf Manji, ili aweze kukamilisha masuala ya marekebisho ya Katiba yao na kujumuisha Kamati ya Maadili na pia kuweza kuandaa Mkutano wa Uchaguzi baada ya Katiba mpya kupitishwa na TFF.