Sunday, June 15, 2014

STARS KWENDA BOTSWANA JUNI 24 KUJIWINDA DHIDI YA MSUMBIJI.

TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inatarajiwa kuondoka nchini wiki ijayo kwenda Botswana kuweka kambi ya mwezi mmoja kujiandaa na mchezo dhidi ya Msumbiji kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani Morocco.
Wachezaji wote wa Taifa Stars waliruhusiwa kurejea makwao jana kwa ajili ya kujiandaa na safari hiyo na watakutana tena kesho.
 Stars inayofundishwa na Mholanzi, Mart Nooij itaondoka nchini Juni 27 kwenda Gaborone, ambako itaweka kambi ya mazoezi hadi Julai 7 itakaporejea nchini.  
Taifa Stars itamenyana na Msumbiji ‘Mambas’ katika hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco baada ya kuitoa Zimbabwe juzi kwa jumla ya mabao 3-2, ikianza kwa ushindi wa 1-0  nyumbani na kumaliza kwa sare ya 2-2 juzi mjini hapa.
Mechi yake kwanza itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Julai 19 na 20 mwaka huu, wakati mechi ya marudiano itafanyika Msumbiji kati ya Agosti 2 na 3 mwaka huu. 
Stars pia inatarajiwa kuwa na mchezo wa kujipima nguvu na Uganda kabla ya kumenyana na Msumbiji.