Monday, May 5, 2014

UCHAHUZI WA SIMBA SASA MAMBO YAMEIVA BAADA YA KATIBA KUKAMILIKA.



UCHAGUZI mkuu wa klabu ya Simba sasa umeanza kuwadia baada ya Katiba ya timu hiyo kukamilika huku Kamati ya uchaguzi ikitarajiwa kukutana kesho kwa ajili ya kujadili tarehe rasmi ya kuanza mchakato wa uchaguzi huo.
Kamati ya uchaguzi ya klabu hiyo chini ya Mwenyekiti wake Damas Ndumbalo inatarajia kukutana kesho, kujadili mchakato mzima wa uchaguzi wa klabu hiyo ambao awali ulipangwa kufanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katiba ya Simba ambayo imefanyiwa marekebisho tayari imekabidhiwa jana kwa uongozi wa klabu hiyo kutoka kwa Serikali baada ya kupitiwa kifungu kwa kifungu na kuridhika nayo.
 Awali katiba hiyo ilionekana kuwa na mapungufu na kulazimisha kuipitia upya ili kuondoa mapungufu hayo, huku Mkurugenzi wa Michezo Leornad Thadeo akionekana kufanya kazi nzuri baada ya Simba kuirejesha Ijumaa ya wiki iliyopita.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Dar es Salaam leo, Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, amesema kuwa tayari wamekabidhiwa Katiba ambapo kesho watakutana na kamati ya Uchaguzi kupanga mchakato mzima wa uchaguzi Mkuu wa Klabu hiyo.
Kamwaga amesema, baada ya kamati kukutana leo, taratibu nzima za mchakato huo, zitawekwa wazi kesho, na kuwapa fursa wagombea kuanza mchakato huo.
Alisema kuwa katiba yao imepitisha kuwepo kwa Kamati ya Maadili na Rufaa ambazo Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage atazitangaza wiki ijayo huku pia katiba ikipendekeza kuwepo kwa mgombea mmoja mwanamke wa kuchaguliwa.
Kamwaga alisema, vipengele vyote vimepita katika katiba yao, isipokuwa cha ibara ya 26(4) kuhusu sifa za mgombea.
“Katiba ya sasa ni lazima katika wagombea watano wa kamati ya utendaji nafasi moja awepo mwanamke, hivyo basi nawaomba wanawake mwenye sifa wajitokeze kwa wingi kuwania uongozi ndani ya Simba, na pia wanaweza hata wakawa watatu, lakini nafasi moja ni lazima

AZAM FC YAVUNJA MKATABA NA KONE WAMO AZIZI NA MWAIPOPO

UONGOZI wa klabu ya Azam FC umefikia makubaliano ya kuvunja Mkataba na mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Ismail Kone ambaye alikuwa anamaliza Novemba mwaka huu.
Pande zote mbili zimefikia makubaliano na mchezaji huyo amepewa haki zake na kurejea nchini mwao. Aidha, Azam FC inawashukuru kwa mchango wao, wachezaji wake wanne, Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo, Malika Ndeule na Omar Mtaki kwa kipindi chao chote walichoitumikia klabu hiyo.
Wanne hao wamemaliza mikataba yao na hawataongezewa- klabu inawashukuru kwa mchango wao kwa kipindi chote tangu wajiunge nayo. Azam FC pia imepokea na kuyakubali maombi ya wachezaji wake wawili, Samih Haji Nuhu na Luckson Kakolaki kustaafu kwa sababu mbalimbali.
Nuhu anasumbuliwa na maumivu ya goti ambalo hana matumaini ya kupona karibuni, wakati Kakolaki ameamua kustaafu ili achukue mafunzo ya ukocha. Klabu
imempa ajira ya kudumu Nuhu katika moja ya viwanda vyake, wakati Kakolaki ameingizwa kwenye benchi la Ufundi la akademi ya klabu.
Tayari klabu imekamilisha usajili wa wachezaji wapya watatu, ambao ni washambuliaji Didier Kavumbangu wa Burundi, Ismaila Diarra kutoka Mali na mzalendo Frank Domayo.
Usajili wa Kavumbangu na Diarra unafanya Azam iwe na wachezaji watano wa kigeni, wengine wakiwa ni Kipre Herman Tchetche na Kipre Michael Balou, ndugu wawili na pacha kutoka Ivory Coast na Mganda Brian Umony.
Azam chini ya kocha wake, Mcameroon Joseph Marius Omog imepanga kuboresha zaidi kikosi ili msimu ujao iweze kupata mafanikio zaidi katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kutetea ubingwa wa Bara.