Uongozi
wa klabu ya Yanga umesema utapinga maamuzi ya kamati ya Sheria na Hadhi
ya Wachezaji kuhusiana na maamuzi yake ya kumtangaza mchezaji wake,
Emmanuel Okwi kuwa huru.
Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria ya Yanga, Sam Mapande amesema kuwa hawajaridhishwa na maamuzi hayo ambayo yanakinzana na shitaka zima la mchezaji huyo.
Mapande
amesema kuwa kamati ya TFF imeamua sakata la Okwi kinyume na malalamiko
yao kwani hakukuwa na lalamiko la mchezaji huyo wa Uganda kuhusiana na malipo ya fedha zake za usajili.
Alisema
kuwa cha kushangaza, kamati hiyo ya TFF iliamua kusikiliza kesi ambayo
haikuwa mbele yao na kutoa maamuzi ambayo hata wao wameshangazwa nayo.
“Kwanza
kesi yenyewe ilikuwa haijamalizika, walituambia tuwasilishe vielelezo
kuhusiana na kitendo cha mchezaji huyo kufanya mazungumzo na klabu ya
Misri, lakini cha kushangaza maamuzi yametolewa, hili limetushangaza
sana,” alisema Mapande.
Alisema kuwa mazingira
yalikuwa yameandaliwa kuibeba Simba na Okwi kwani hata malalamiko yao
kwa Simba hayakusikilizwa. “Malalamiko yetu yalikuwa wazi kabisa, yapo
kimaandishi, hatukuwai kulalamikiwa, suala la fedha za usajili la Okwi
limetoka wapi, kama lilikuwepo, mbona hatujajulishwa kimaandishi kama
utaratibu ulivyo,” alisema.
Alisema kuwa Kamati
hiyo kumruhusu mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo Zacharia Hans Pope ambaye
pia ni mwenyekiti wakamati ya usajili ya Simba kuwemo katika kikao
hicho kinyume na taratibu za Fifa kupitia kifungu namba 19 kinachoeleza
mgongano wa kimaslah.
MAAMUZI YA KIKAO CHA JANA
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekutana leo (Septemba 7
mwaka huu) na kupitia masuala mbalimbali ikiwemo mgogoro wa kimkataba kati ya klabu ya Yanga na mchezaji Emmanuel Okwi.
Mkataba
huo ulipitiwa na Kamati ikiwemo kumsikiliza mchezaji mwenyewe pamoja na
upande wa Yanga, na kuridhika kuwa mkataba kati ya pande hizo
umevunjika.
Ukiwa ni mkataba wa pande mbili, Yanga ilikiuka kipengele namba 8 kuhusu malipo ya ada ya usajili.
Yanga
ikiwa mwajiri, haikutekeleza kipengele hicho cha kimkataba hadi kufikia
Juni 27 mwaka huu ilipoandika barua TFF kuomba mkataba huo uvunjwe. Kwa
maana hiyo Okwi ni mchezaji huru, hivyo yuko huru kujiunga na timu
yoyote.
Mkataba
ni uhusiano kati ya mwajiri (Yanga) na mwajiriwa (Okwi), ambapo Kamati
imebaini kuwa uhusiano huo haupo,hivyo hakuna mazingira ya pande hizo
mbili kuendelea kufanya kazi pamoja.
Pamoja
na Yanga kuwasilisha pingamizi la kuwepo mmoja wa wajumbe katika kikao
kwa sababu za kimaslahi (conflict of interests), walifahamishwa kuwa
kilichopo mbele ya kamati ni mgogoro wa kimkataba kati ya Yanga na Okwi,
na si usajili.
Pia
lilijitokeza suala la Okwi kutakiwa na klabu ya Wadi Degla ya Misri.
Kamati imeiagiza Sekretarieti ya TFF kulifanyia uchunguzi suala hilo na
kulitolea taarifa katika kikao kijacho.
Hata
hivyo mjumbe huyo hakushiriki katika kuchangia hoja na kutoa maamuzi.
Uamuzi wa kamati ulifanyika baada ya majadiliano, hivyo hakukuwa na
suala la kupiga kura.
Kuhusu
pingamizi la Coastal Union kwa Abdi Banda, Kamati imebaini kuwa klabu
hiyo imevunja mkataba kati ya pande hizo mbili kwa kushindwa kumlipa
mchezaji huyo mshahara wa miezi mitatu mfululizo kama takwa la mkataba.
Klabu ya Coastal Union iliwakilishwa na mmoja wa viongozi wake, wakati Banda aliwakilishwa na mwanasheria wake.
Vilevile
Kamati imekubaliana na pingamizi la Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa
Morogoro (MRFA) kuhusu wachezaji waliofanyiwa uhamisho kutoka katika
mkoa wake bila kulipiwa ada za usajili, hivyo klabu husika zinatakiwa
kulipa ada hizo.
Pia
Kamati imeagiza klabu zote zilizosajili wachezaji bila kuwafanyia
uhamisho, kulipa ada za uhamisho kwa pande husika kabla ya kuanza ligi,
vinginevyo leseni zao zitazuiwa hadi watakapolipa.
Mashauri mengine ya pingamizi yatasikilizwa baadaye kwa vile klabu husika hazikupata fursa ya kufika mbele ya kamati.