Friday, December 12, 2014

BBC:HOFU YATANDA TANZANIA KUNYIMWA MSAADA NA MAREKANI

Serikali ya Tanzania iko hatarini kukosa dola za Marekani milioni mia saba sawa na trilioni 1.1 kwa fedha za Tanzania kwa ajili ya mradi wa pili wa mfuko wa changamoto za Milenia (MCC) kutokana na kushamiri kwa vitendo vya rushwa nchini humo.
Marekani imebainisha kuwa mkataba wa pili wa miradi inayofadhiliwa na shirika lake la Changamoto za Milenia (MCC) utategemea hatua zitakazochukuliwa na serikali ya Tanzania dhidi ya wahusika wa kashfa hiyo.
Haya yanajiri wakati Rais Jakaya Kikwete akisubiriwa kutoa maamuzi ya mapendekezo yaliyofikiwa na Bunge kuhusiana na sakata la uchotwaji fedha zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka kaunti ya Tegeta Escrow wiki ijayo.
Katika tamko hilo kwa umma ambalo limewekwa kwenye tovuti ya MCC, bodi ilieleza kutambua umuhimu wa kusubiri na kuona utekelezaji kamilifu wa tamko lililotolewa na Ikulu ya Tanzania Desemba 9, mwaka huu kwamba itachukua hatua za haraka na kutoa maamuzi dhahiri na thabiti kuhusu maazimio ya Bunge juu la suala la IPTL.
Taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ilieleza kuwa wakurugenzi wa MCC waliokutana katika mkutano wao uliofanyika Desemba 10, mwaka huu wamesikitishwa na hali ya rushwa nchini Tanzania.
Uamuzi huo wa Marekani ambayo inafadhili miradi mingi ya mabilioni ya fedha ni mtihani wa pili kwa Rais Kikwete baada ya ule wa maazimio ya Bunge yaliyotaka viongozi wakiwamo mawaziri waliotajwa katika kashfa hiyo kuwajibishwa.
Wanaotakiwa kuwajibishwa na Rais Kikwete ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa, Sospeter Muhongo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Novemba mwaka huu, Serikali ya Marekani kwa kupitia MCC, ilikubali kutoa ruzuku ya hadi Dola za Kimarekani milioni 9.78 kwa ajili ya maandalizi ya miradi ya uwekezaji yenye matokeo makubwa katika sekta ya nishati nchini.
Tanzania ilikuwa mojawapo ya nchi kumi zilizojadiliwa na Bodi ya MCC iliyokutana kuangalia kama nchi hizo zimekidhi vigezo vya kuendelea na mchakato wa kuandaa mikataba mipya.
Wakati wa mkutano wa 16 na 17 wa Bunge, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), alidokeza kusudio la Marekani kukataa kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya MCC, lakini Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alikanusha taarifa hizo.
Juhudi za BBC kumtafuta Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Mark Childress,aweze kuzungumzia juu ya ripoti hiyo ziligonga mwamba kutokana na sababu za kiprotokali .

EVERTON AJIPANGA KUMTIA KANDARASI MPYA SAMWEL ETOO

Wakala wa mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Cameroon, Samuel Eto’o anatarajiwa kuwa nchini Uingereza wakati wa krismasi ili kuzungumzia suala la kuongeza mkataba na klabu ya Everton.
Mkataba aliosaini mshambuliaji huyo wakati akitua Goodison Park kama mchezaji huru katika majira ya kiangazi una kipengele ambacho kinaruhusu mazungumzo kufanyika pindi mechi 15 zinazpokuwa zimechezwa.
Kutoka na umuhimu wa Eto,o katika klabu hiyo baada ya kufunga mabao manne na kusaidia mengine mawili katika mechi 15 za mashindano yote, Everton wanaonekana kuwa tayari na mazungumzo hayo.

 Mara kadhaa kocha wa Everton, Roberto Martinez amekiri kuwa angependa kumbakisha Eto’o mwenye umri wa miaka 33 katika kikosi chake.

WENGER AWA BABAISHA MASHABIKI KATIKA SUALA LA USAJILI

MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amehatarisha kuwaudhi zaidi mashabiki wa timu hiyo baada ya kudai kuwa hatakuwa na haja ya kufanya usajili katika kipindi cha dirisha dogo Januari mwakani kama wachezaji wote katika kikosi chake cha sasa watakuwa fiti.
Kocha huyo raia wa Ufaransa amekuwa katika shinikizo kubwa katika wiki za karibuni baada ya Arsenal kuonekana kushindwa mapema mbio za ubingwa kwa kukubali kipigo cha mabao 3-2 katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Stoke City.
Wenger alishambuliwa na mashabiki wenye hasira katika kituo cha treni wakati akirejea London baada ya mchezo dhidi ya Stoke.
Pamoja na kuwa nyuma ya vinara Chelsea kwa alama 13 Wenger bado bado anaonesha kutoshtushwa na hali hiyo kwa kudai kuwa hatarajii usajili wa Januari kuwa pilikapilika kubwa.

Wenger amesema kama wachezaji watakuwa fiti na uwezo wa kucheza hadhani kama atahitaji kufanya usajili wa aina yeyote.

CHELSEA ITAMKOSA MLINDA MLANGO WAKE MAHIRI COURTOIS KUWA MAJERUHI

KLABU ya Chelsea imepata pigo baada ya mlinda mlango wake Thibaut Courtois kupata majeruhi ya msuli kuelekea katika mchezo wao wa kesho Jumamosi dhidi ya Hul City.
Golikipa huyo wa kimataifa wa Ubelgiji anaungana na Cesc Fabregas anayetumikia adhabu kuwa wachezaji ambao wataukosa mchezo huo wakati Chelsea wakijaribu kurejesha makali yao baada ya kipigo kutoka kwa Newcastle United mwishoni mwa wiki iliyopita.
Akizungumza na wanahabari meneja wa Chelsea Jose Mourinho amesema Courtois alikuwa na matatizo madogo wakati wa mazoezi hivyo hatakuwepo katika mchezo wa kesho.
Mourinho aliendelea kudai kuwa Fabregas amekuwa na msaada mkubwa katika kikosi chake lakini hawatakuwa naye katika mchezo wa kesho akitumikia adhabu yake ila wana wachezaji wengine anaowaamini.

Mourinho sasa atalazimika kuendelea kumtumia Petr Cech ambaye alimtumia pia katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Sporting Lisbon Jumatano iliyopita.

MANENO ALIYO YAANDIKA MH ZITTO KATIKA UKURASA WAKE WA TWITTER SOMA UFAIDIKE

Unyenyekevu {kuwa na kiasi }
Mwaka 2007 Agosti 14, nilisimamishwa Kuhudhuria vikao vya Bunge kwa kosa la kumwita Waziri wa Nishati na Madini Bwana Nazir Karamagi muongo. Kiukweli nilisimamishwa kwa sababu nilitoa hoja Bungeni iliyoiabisha Serikali - Hoja ya Buzwagi.
Wananchi walikasirishwa na kitendo hicho na kuamua kunipokea kwa maandamano makubwa sana nilipoingia Jijini Dar Es Salaam na kwenye mikoa mingine niliyofanya ziara.
Mawaziri waliotumwa kueleza maamuzi ya Bunge walizomewa na kumwagiwa mchanga. Mzee Samwel Sitta, Spika wa Bunge la Tisa, alikuwa anatumiwa sms za 'kifedhuli' kwa mujibu wa maneno yake; nyingine alinitumia kunisihi nizungumze na ' wafuasi' wangu ili waache kufanya hivyo. Hasira ya Wananchi ilikuwa kubwa sana na ilionekana wazi wazi.
Siku ya tarehe 19 Agosti nilitoka Dodoma kuelekea Dar Es Salaam. Kabla sijafika Chalinze ya Dodoma alinipigia simu kaka yangu Abdurahman Mbamba, akanisihi sana kuwa mnyenyekevu kwa maongezi yangu. Nasaha hizi kwa kweli zinaniongoza mpaka leo hii. Kwenye mafanikio ya jambo fulani au hata kutofanikiwa, nakumbuka maneno ya Abdurahman Mbamba.
Nilipokuwa nahutubia Jangwani siku hiyo, niliongea kwa ufupi sana. Watu wakapiga kelele niendelee kuongea. Ningeweza kuongea nitakavyo maana ndio nilikuwa ' star' wa nyakati. Mshale wa nasaha zile ukanichoma ' kuwa mnyenyekevu '!
Nikawaambia wananchi ' siwezi kuendelea kuongea, nina Viongozi wangu hapa'. Alikuwapo Mheshimiwa Freeman Mbowe, Dkt. Willibrod Slaa, Mheshimiwa Augustine Mrema, Maalim Seif Sharif Hamad, ndg. Ibrahim Lipumba na Bwana James Mbatia.
Kwa unyenyekevu nilishuka jukwaani na kutoa nafasi kwa Viongozi kuzungumza. Watu walitaka na ningetaka ningeendelea lakini la hasha, nilikataa.
Rais aliunda Kamati ya kupitia Mikataba ya Madini. Aliniteua katika Kamati ile iliyoongozwa na Jaji Mark Bomani. Watu wangu wengi ' wa karibu' walinisihi nisikubali kuingia kwenye kamati. Mmoja alithubutu kuniambia ' snubb him' akimaanisha Rais.
 Kwamba ningepata umaarufu zaidi. Ningeweza kukataa na kuwafurahisha watu waliotaka kumwaibisha Rais. ' kuwa mnyenyekevu' yakawa ni maneno yananirudia kila wakati.
Hilo na kiu ya kuijua Sekta ya Madini vilivyo yalinishawishi kukubali uteuzi ule. Walionishawishi kukataa hawakunisamehe mpaka leo. Utawasikia wakisema ' Kamati ya Bomani haikufanya lolote'.
Wakati huo huo wanakuwa mstari wa mbele kufurahia mabadiliko makubwa sana kwenye Sekta ya Madini ikiwemo kuongezeka Mapato ya kikodi, umiliki wa Serikali kwenye migodi, Madini ya Vito kuchimbwa na Watanzania pekee na hata kuanza kutozwa kwa Kodi ya ongezeko la mtaji ( capital gains tax ).
Yote hayo yametokana na mapendekezo ya Kamati ya Bomani yaliyozaa Sera mpya ya Madini ya mwaka 2009 iliyopelekea Sheria mpya ya Madini ya mwaka 2010.
Mwaka 2014 tunaufunga kwa suala la akaunti ya Tegeta Escrow. Bunge lilifanikiwa kupitisha maazimio 8 yaliyowasilishwa Serikalini kwa utekelezaji. Maazimio hayo yalipatikana kwa maridhiano ya Bunge zima. Ni mafanikio makubwa ambayo yanashawishi wahusika wakuu kufurahia au hata ku 'claim credit'.
Mbunge mmoja kijana rafiki yangu kutoka Mkoa wa Arusha akaniambia ' brother this is your resurrection ' na usiache. Mwandishi mmoja wa gazeti la kila wiki akaniambia ' it's a come back ' na kunitaka nifanye ziara Nchi nzima kuelezea suala hili.
Wenzangu kwenye Siasa wakaandaa maandamano Jijini Dar ambayo nilikataa. Shemeji yangu mmoja akaniambia ' kwenye ushindi jua pa kuishia'. Maneno haya hayana tofauti na nasaha za Abdurahman.
Sasa kuna juhudi kubwa za kutetea waliotajwa na Taarifa ya Kamati ya PAC. Magazeti, haswa ya Serikali yamekuwa yakiandika habari zenye mwelekeo wa kutetea.
Ikulu imeagiza Taarifa ya CAG ichapwe kwenye magazeti, jambo ambalo halijapata kutokea huko nyuma kwani sio mara ya kwanza PAC kutumia Taarifa ya CAG kuwajibishana.
Makala zinaandikwa kumshawishi Rais asitekeleze maamuzi ya Bunge. Nasaha za ' know where to stop ' na ' kuwa mnyenyekevu ' zinanivuta na kunishawishi kutosema lolote.
Hekima inataka kumwachia Mkuu wa Nchi kuamua kwa namna itakavyompendeza. Tumwache aamue. Unyenyekevu unataka hivyo. Wenye ushawishi tofauti walikuwa na nafasi Bungeni.
Walishindwa ndani ya Baraza la Taifa. Unyenyekevu ni kwa walioshindwa pia.