Friday, November 28, 2014

TFF YAKIRI KUFANYA MAKOSA KURUHUSU KUFUNGULIWA DIRISHA DOGO LA USAJILI.


Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limekiri kufanya makosa kuruhusu kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili kabla ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

VPL ilisimama kwa wiki saba Novemba 9 baada ya kuchezwa kwa mechi 49 za raundi ya kwanza hadi ya saba kupisha usajili wa dirisha dogo, mashindano ya Kombe la Uhai yanayoshirikisha Timu B za klabu za Ligi Kuu na michuano ya Kombe la Chalenji.
TFF ilifungua dirisha dogo la usajili Novemba 15 na litafungwa Desemba 15 huku mechi za raundi ya nane hadi ya 13 ya mzunguko wa kwanza wa VPL bado hazijachezwa, hivyo kutoa mwanya kwa baadhi ya wachezaji watakaozihama timu zao kipindi hiki cha usajili kucheza mechi tatu dhidi ya timu moja.


Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa amekiri shirikisho hilo kujisahau katika suala hilo lakini akasisitiza kuwa hakuna tatizo kubwa mchezaji kucheza mechi tatu dhidi ya timu moja.
Mwesigwa amesema haijawahi kutokea hapa kwetu (Tanzania), tumejifunza kitu lakini mchezaji kucheza mechi tatu dhidi ya timu moja VPL haina tatizo, tatizo kubwa ni mchezaji kusajiliwa na zaidi ya timu mbili msimu mmoja. Hili linakatazwa kikanuni.

Kiungo mkongwe wa Simba Amri Kiemba amejiunga na Azam FC kwa mkopo huku klabu hiyo ya Msimbazi ikiwabana wanalambalamba wasimtumie katika mechi zinazozikutanisha timu hizo mbili msimu huu.
TFF kupitia kwa Mkurugenzi wake wa Mshindano, Boniface Wambura imepinga vikali uamuzi huo wa Simba kwa kuwa kanuni zinamruhusu mchezaji huyo kukipiga dhidi ya timu iliyomtoa kwa mkopo kwenda timu nyingine, hata hivyo.
Mchezaji wa Ndanda FC aliyecheza dhidi ya Azam FC msimu huu, akisajiliwa Simba atacheza dhidi ya Azam mara tatu katika mechi za msimu mmoja wa ligi kuu, ikiwa ni mfano wa kilichokosewa na TFF kuruhusu dirisha dogo la usajili msimu huu lifunguliwe ilhali mechi za mzunguko wa kwanza bado hazijakamilika.

CECAFA YASEMA BADO WANAHANGAIKIA MICHUANO YA CHALLENGE CUP KUFANYIKA

BARAZA la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), limesema bado linahangaikia kufanyika kwa michuano ya Kombe la Challenge mwaka huu.

Meneja wa Vyombo vya Habari wa CECAFA, Rogers Mulindwa amesema leo kwamba,  michuano ya Challenge ambayo awali ilikuwa ifanyike Ethiopia, lakini ikajivua uenyeji, bado ipo kwenye uwezekano wa kufanyika.Kamati Kuu ya CECAFA chini ya Mwenyekiti, Mhandisi Leodgar Tenga na Katibu Mkuu, Nicholas Musonye bado inafanyia kazi uwezekano wa kuhakikisha michuano hiyo inafanyika mwaka huu,” amesema Mulindwa.
Mganda huyo amesema kwamba  CECAFA baadaye itatoa taarifa rasmi juu ya mustakabali wa mashindano ambayo hufanyika mwishoni mwa Novemba hadi mwanzoni mwa Desemba.
Nchi wanachama wa CECAFA ni Sudan, Ethiopia, Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi, Somalia, Eritrea, Djibouti, Zanzibar na Sudan Kusini.

KLOPP KOCHA WA DORTMUND ASEMA MASHABIKI WA ARSENAL KUWA KIPIGO CHA 2-0 CHA UEFA HAWAWEZI KUPATA KAZI

MENEJA wa klabu ya Brussia Dortmund, Jurgen Klopp ametania kuwa mashabiki wa Arsenal hawatamuhitaji tena baada ya kuona timu yake ikitandikwa mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya juzi.
Klopp amekuwa akihusishwa na tetesi za kuchukua mikoba ya kionoa Arsenal katika wiki kadhaa zilizopita baada ya kuzuka msukumo kwa Arsene Wenger kufuatia kuanza vibaya msimu wa Ligi Kuu. 
Kocha huyo amekiri hivi karibuni kuwa anadhani anaweza kumudu kuhamia katika Ligi Kuu kama akiamua kuondoka Dortmund lakini sasa anadhani nafasi yake ya kutua Arsenal imetoweka. 

Akihojiwa Klopp amesema hafikirii baada ya kiwango cha Dortmund walichokionyesha katika Uwanja wa Emirates kama mashabiki wa Arsenal watamuhitaji. 
Klopp aliteuliwa kuwa kocha wa Dortmund kuanzia mwaka 2008 na kuisaidia timu hiyo kushinda mataji mawili ya Bundesliga, Kombe la Ujerumani, Supercup na kutinga fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. 

ROY KEANE AJIUZULU WADHIFA WAKE ASTON VILLA WA KOCHA MSAIDIZI.


KLABU ya Aston Villa imetangaza kuwa Roy Keane amejiuzulu wadhifa wake wa kocha msaidizi wa timu hiyo. 
Mapema Keane alikaririwa akidai kuwa anapata tabu kuhudumia vibarua viwili alivyokuwa navyo. 
Keane ambaye pia ni kocha msaidizi wa Ireland amesema sio haki kwa pande zote mbili, hivyo anatakiwa kufanya uamuzi wa kuchagua kibarua kimoja. 
Kocha wa Villa Paul Lambert alithibitisha asubuhi ya leo kuwa taarifa hizo na kudai kuwa ana heshimu uamuzi uliochukuliwa.


GALATASARAY BAADA YA KUNTUPIA PRANDELLI SASA YAMCHUKUA HAMZAOGLU KUZIBA NAFASI.

KLABU kongwe jijini Instabul ya Galatasaray wanatarajia kumteua kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Uturuki Hamza Hamzaoglu kuwa meneja mpya wa klabu hiyo baada ya kutimuliwa kwa Muitaliano Cesare Prandelli. 
Klabu hiyo ilimtimua Prandelli baada ya kuitumikia chini ya nusu ya msimu kutokana na matokeo mabovu ambayo wamekuwa wakipata. 
Hamzaoglu amekuwa akiitumikia Uturuki chini ya kocha mkuu Fatih Terim toka mwaka 2013, na uamuzi wake huo umekuja baada ya kufanya mazungumzo na kocha huyo. 
Bodi ya klabu hiyo ilifikia uamuzi wa kumtimua Prandelli baada ya kutandikwa na Anderlecht kwa mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano usiku na kufuta matumaini yao ya kufuzu hatua ya mtoano. 
Prandelli alitua katika klabu hiyo Julai mwaka huu akichukua nafasi ya Muitaliano mwenzake Roberto Mancini na kupewa mkataba wa miaka miwili uliokuwa na thamani ya euro milioni 2.3.

DR SHEIN ASEMA KATIKA KUKUZA MPANGO WA UCHUMI NA KUONDOA UMASKINI ZANZIBAR SECTA YA UTALII NDIO SECTA YAKUUNGWA MKONO.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dokta, Ali Mohamed Shein amesema kuwa katika Mpango wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umasikini Zanzibar (MKUZA), sekta ya utalii ndio sekta mama na nyegine zimekuwa zikiongeza nguvu hivyo inahitaji kuendelea kuungwa mkono ndani na nje ya nchi.
Dokta, Shein ameyasema hayo wakati alipofanya mazungumzo na Balozi mpya wa Tanzania nchini Canada Jack Mugendi Zoka,  Ikulu mjini Zanzibar aliyefika kwa ajili ya kuaga kwenda katika kituo chake kipya cha kazi nchini humo  kufuatia uteuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete hivi karibuni.
Katika maelezo yake Dokta Shein amemueleza Balozi huyo mpya wa Tanzania nchini Cadana kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikifanyaa juhudi za makusudi katika kuhakikisha sekta ya utalii inaimarika na inaendelea kuwa sekta mama na muhimu hapa nchini.
Akieleza juu ya sekta ya uwekezaji Dokta, Shein amemueleza Balozi Zoka kuwa mbali ya kutilia mkazo uwekezaji katika ujenzi wa mahoteli pia, Serikali imekuwa ikitilia mkazo uwekezaji katika Hospitali za kisasa za binafsi ambazo zinatibu maradhi maalum.

OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU IMESEMA ITAENDELEA KUWAPATIA WANANCHI TAKWIMU SAHIHI ZINAZOHUSU SEKTA MBALIMBALI.

SERIKALI kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu imesema kuwa itaendelea kuwapatia wananchi takwimu sahihi zinazohusu sekta mbalimbali ili kuwajengea uwezo wa kushiriki katika ngazi za maamuzi na masuala mbalimbali nchini.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es salaam na Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar  Omar Yussuf  Mzee wakati akifungua rasmi maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika yanaoongozwa na kauli mbiu isemayo Takwimu Huria kwa uwajibikaji na ushirikishwaji wa wadau wote.
Amesema upatikanaji wa taarifa na  takwimu sahihi kwa wananchi unaongeza ushiriki wao katika maamuzi na kuwajengea uwezo wa kutathmini utendaji wa Serikali katika masuala mbalimbali yakiwemo mapato na matumizi.
Amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu itaendelea kuhakikisha kuwa takwimu mbalimbali zinapatikana kwa urahisi kupitia mtandao, machapisho na mifumo rahisi ili kuwawezesha wananchi na wadau mbalimbali kuzipata pindi wanapozihitaji.