SERIKALI kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu imesema kuwa itaendelea kuwapatia wananchi takwimu sahihi zinazohusu sekta mbalimbali ili kuwajengea uwezo wa kushiriki katika ngazi za maamuzi na masuala mbalimbali nchini.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es salaam na Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Omar Yussuf Mzee wakati akifungua rasmi maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika yanaoongozwa na kauli mbiu isemayo Takwimu Huria kwa uwajibikaji na ushirikishwaji wa wadau wote.
Amesema upatikanaji wa taarifa na takwimu sahihi kwa wananchi unaongeza ushiriki wao katika maamuzi na kuwajengea uwezo wa kutathmini utendaji wa Serikali katika masuala mbalimbali yakiwemo mapato na matumizi.
Amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu itaendelea kuhakikisha kuwa takwimu mbalimbali zinapatikana kwa urahisi kupitia mtandao, machapisho na mifumo rahisi ili kuwawezesha wananchi na wadau mbalimbali kuzipata pindi wanapozihitaji.