Friday, November 28, 2014

CECAFA YASEMA BADO WANAHANGAIKIA MICHUANO YA CHALLENGE CUP KUFANYIKA

BARAZA la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), limesema bado linahangaikia kufanyika kwa michuano ya Kombe la Challenge mwaka huu.

Meneja wa Vyombo vya Habari wa CECAFA, Rogers Mulindwa amesema leo kwamba,  michuano ya Challenge ambayo awali ilikuwa ifanyike Ethiopia, lakini ikajivua uenyeji, bado ipo kwenye uwezekano wa kufanyika.Kamati Kuu ya CECAFA chini ya Mwenyekiti, Mhandisi Leodgar Tenga na Katibu Mkuu, Nicholas Musonye bado inafanyia kazi uwezekano wa kuhakikisha michuano hiyo inafanyika mwaka huu,” amesema Mulindwa.
Mganda huyo amesema kwamba  CECAFA baadaye itatoa taarifa rasmi juu ya mustakabali wa mashindano ambayo hufanyika mwishoni mwa Novemba hadi mwanzoni mwa Desemba.
Nchi wanachama wa CECAFA ni Sudan, Ethiopia, Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi, Somalia, Eritrea, Djibouti, Zanzibar na Sudan Kusini.