Wednesday, October 15, 2014

SIMBA YAENDELEA KUPOKEA KIPONDO BONDENI AFRICA YA KUSINI 2-0 DHIDI YA JOMO COSMOS

Wekundu wa Msimbazi Simba Sc imekamilisha mechi zake za kirafiki za kujipima nguvu katika kambi yake ya Afrika kwa kufungwa mabao 2-0 na Jomo Cosmos mjini Johannesburg jioni hii.

Pamoja na kufungwa na timu hiyo ya Daraja la Kwanza, inayomilikiwa na kufundishwa na gwiji wa soka Afrika Kusini, Jomo ‘Black Prince’ Sono, Simba SC ilicheza soka ya kuvutia.

katika kambi hiyo huo ni mtanange wa tatu kwa Simba SC katika kambi yake ya Afrika Kusini tangu iwasili Oktoba 8, mwaka huu kwa ajili ya maandalizi ya mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu wao, Yanga SC Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
Katika mchezo wake wa kwanza, Simba SC ililazimishwa sare ya bila kufungana na Orlando Pirates kabla ya kufungwa mabao 4-2 na Bidvest Wits, au Wits University.
Simba SC itaendelea na mazoezi kesho na inatarajiwa kurejea Dar es Salaam Ijumaa tayari kwa mchezo wa Jumamosi, unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini.

TAARIFA KUTOKA TFFUCHAGUZI MDOGO TPLB NOVEMBA 15

Mkutano Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) utafanyika Novemba 15 mwaka huu jijini Dar es Salaam ambapo moja ya ajenda ni uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi moja ya uongozi kwenye bodi hiyo.
Nafasi hiyo ya ujumbe kwenye Kamati ya Uendeshaji ya TPLB iliyokuwa ikishikiliwa na Kazimoto Muzo imebaki wazi baada ya klabu yake ya Pamba ya Mwanza kushuka daraja kutoka la Kwanza hadi la Pili.
Hivyo, wagombea wa nafasi hiyo ni kutoka kwenye klabu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL). Klabu hizo zina nafasi mbili kwenye Kamati ya Uendeshaji ya TPLB ambapo nyingine inashikiliwa na Omari Mwindadi wa klabu ya Mwadui ya Shinyanga.

SDL WAONGEZEWA MUDA WA USAJILI
indexShirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeongeza muda wa usajili wa wachezaji kwa timu za Ligi Daraja la Pili (SDL) kwa siku saba ambapo sasa utamalizika Oktoba 21 mwaka huu.
Awali usajili huo unaofanyika kwa njia ya mtandao (online) ulikuwa umalizike jana (Oktoba 14 mwaka huu), lakini ni klabu chache ndizo zilizoweza kusajili ndani ya muda uliopangwa.
Klabu ambazo hazijakamilisha shughuli hiyo ya usajili, zinatakuwa kukamilisha ndani ya siku hizo saba kwani TFF haitaongeza tena muda wa usajili. Vilevile klabu za SDL zinakumbushwa kuwasilisha majina ya viwanja vya nyumbani ambavyo timu zao zitatumia kwenye ligi hiyo.
TFF ilifanya mafunzo ya usajili kwa maofisa usajili wa klabu hizo Oktoba 6 na 7 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Timu za SDL zimegawanywa katika makundi manne ya timu sita zitakazocheza ligi kwa mtindo wa nyumbani na ugenini. Kundi A lina timu za Mpanda United ya Katavi, Ujenzi (Rukwa), Mvuvumwa FC (Kigoma), Mji Mkuu FC (Dodoma), Milambo (Tabora) na Singida United (Singida).
Kundi B ni Mbao FC (Mwanza), Bulyanhulu FC (Shinyanga), Eleven Stars (Kagera), JKT Rwamkoma (Mara), Pamba (Mwanza) na AFC (Arusha). Kundi C ni Navy, Mshikamano, Transit Camp na Abajalo za Dar es Salaam, Kiluvya United (Pwani) na Kariakoo (Lindi(.
Timu zinazounda kundi D ni Magereza (Iringa), Town Small Boys (Ruvuma), Njombe Mji (Njombe), Volcano FC (Morogoro), Wenda FC (Mbeya) na Mkamba Rangers (Morogoro).
MAREKEBISHO YA RATIBA FDL KUNDI A
Mechi nne za Kundi A la Ligi Daraja la Kwanza (FDL) zimefanyiwa marekebisho ili kutoa fursa ya matumizi ya Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.
Timu za African Lyon na Kimondo FC ambazo awali zilikuwa zicheze Oktoba 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani, sasa zitacheza Oktoba 26 mwaka huu Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Nayo mechi ya Polisi Dar es Salaam na Majimaji ya Songea iliyokuwa ichezwe Oktoba 26 mwaka huu Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, sasa itachezwa Oktoba 27 mwaka huu kwenye uwanja huo huo.
Mechi ya Friends Rangers na Ashanti United iliyokuwa ichezwe Mabatini mkoani Pwani, Oktoba 26 mwaka huu, sasa itachezwa Uwanja wa Karume, Oktoba 28 mwaka huu.
Pia
 mechi ya Lipuli FC na JKT Mlale iliyokuwa ichezwe Oktoba 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa, imesogezwa mbele kwa siku moja. Mechi hiyo sasa itachezwa Oktoba 26 mwaka huu kwenye uwanja huo huo.