Tuesday, December 2, 2014

POLISI MORO NA MWADUI FC ZAMTOLEA MACHO KINDA MIRAJI ADAM LA SIMBA

Timu Polisi ya Morogoro na Mwadui FC ya Shinyanga zimewasilisha barua kumuomba beki wa pembeni Miraj Adam wa Simba SC kwa mkopo baada ya kushushwa Simba B.
Polisi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania inapambana na Mwadui FC, inayopigania kupanda Ligi Kuu pia kuwania huduma za beki huyo aliyetokea timu ya vijana ya Wekundu hao wa Msimbazi.
Mwadui wanaamini wanaweza kumpata kwa urahisi beki huyo kwa sababu ya mahusiano mazuri ya kocha wao, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na klabu ya Simba SC.
Lakini Polisi nayo inaamini inaweza kumpata kwa urahisi beki huyo wa kulia, Miraj, kwa sababu inacheza Ligi Kuu kwa sasa na Morogoro si mbali sana na Dar es Salaam anakoishi mchezaji huyo.

Kwa sasa, Miraj ameshushwa kikosi cha pili baada ya mechi saba za awali za Ligi Kuu, lakini Simba SC bado haijaamua kumtoa kwa mkopo hadi hapo itakapofanikisha kusajili mchezaji mwingine wa nafasi hiyo.