Friday, April 19, 2013

MURRAY ASHINDWA KUSONGA MBELE
MCHEZAJI nyota tetenesi namba moja wa Uingereza, Andy Murray ameshindwa kusonga mbele katika hatua ya nane bora baada ya kukubali kipigo cha 6-1 6-2 kutoka kwa Stanislas Wawrinka katika mzunguko wa tatu wa michuano ya Monte Carlo Masters inayoendelea huko Monaco. Murray ambaye ameshinda mara nane katika mechi 12 walizokutana Wawrinka wa Switzerland katika mchezo huo alionekana kucheza chini ya kiwango chake cha kawaida nafasi ambayo ilitumiwa vyema na mpinzani wake kuhakikisha anaibuka kidedea. Kupoteza mchezo huo ni pigo kubwa kwa Murray ambaye alikuwa akitumia michuano hiyo kujiandaa kwa ajili ya kutetea taji lake la michuano ya wazi ya Ufaransa. Kwa upande mwingine Novak Djokovic na Rafael Nadal wao walifanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo baada ya kushinda mechi zao.


RAIS wa klabu ya fc Barcelona, Sandro Rosell amebainisha kuwa amepanga kugombea nafasi hiyo kwa kipindi kingine pindi atakapomaliza kipindi cha kwanza mwaka 2016. Rosell alichaguliwa kuwa rais wa klabu hiyo ya Hispania mwaka 2010 ambapo hapo kabla alikuwa mjumbe wa bodi katika uongozi wa aliyekuwa rais wa klabu hiyo Joan Laporta kabla ya kujiuzulu mwaka 2005. Chini ya uongozi wa Rosell Barcelona imefanikiwa kushinda taji moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya, taji lingine moja la Ligi Kuu nchini Hispania na moja la Kombe la Mfalme ambapo msimu huu wako katika nafasi ya kunyakuwa taji lingine la ligi huku wakiwa katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. 
Barcelona inamilikiwa na maelfu ya wanachama ambao huchagua rais na kamati ya utendaji, uchaguzi ambao hufuatiliwa kwa karibu na mashabiki wa soka wa mji huo na nchi nzima kwa ujumla.