Kocha mpya wa klabu ya
Paris Saint-Germain-PSG, Laurent Blanc ameanza vibaya kibarua chake baada ya mchezo
wake wa kwanza wa kirafiki kujiandaa na msimu wa ligi kumalizika kwa
mabingwa hao wa soka nchini Ufaransa kupokea kichapo cha mabao 3-1 kutoka
kwa timu ya Sturm Graz ya Austria. Wenyeji
ndio waliotangulia kushinda bao la kwanza dakika ya 26 kupitia kwa
mchezaji Robert Beric akiyatumia vyema makosa ya beki kinda wa PSG
Antoine Conte kabla ya Marco Djuricin kuongeza bao la pili dakika mbili
baadae. Sturm
ambao walionekana kuwa fiti zaidi baada ya kuanza mazoezi wiki mbili
kabla ya PSG waliongeza bao la tatu katika dakika ya 76 kupitia kwa
Nikola Vujadinovic wakati PSG walipata bao lao la kufutia machozi
kupitia kwa Hervin Ongenda dakika tano kabla mpira haujamalizika. PSG
wataendelea na maandalizi yao kwa ajili ya kujiwinda na msimu mpya kwa
mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya Rapid Vienna Ijumaa.