Uongozi wa mabingwa wa
ligi kuu soka ya Vodacom Tanzania Bara Dar Es Salaam Young African
imemtambulisha rasmi mshambuliaji MRISHO HALFAN NGASA kuwa mchezaji wao
kwa ajili wa msimu ujao wa ligi hiyo. NGASA alikuwa anacheza kwa mkopo kwa wapinzani wa jadi wa Yanga , Simba akitokea katika Klabu ya Azam ya Jijini Dar Es Salaam. Akimtambulisha
rasmi mbele ya Waandishi wa Habari hii leo Makao Makuu ya Klabu hiyo
Katibu wa Yanga LAWRANCE MWALUSAKO amesema wamefikia hatua hiyo baada ya
kufanya mazungumza na mshambuliaji na kuamua kurejea katika Klabu yake
hiyo ya zamani. MWALUSAKO amesema NGASA ambaye amekiri kuwa na mahaba ya dhati na Klabu hiyo ameingia mkataba wa miaka miwili. Akizungumza
baada ya kutambulishwa rasmi NGASA amesema anamshukuru Mungu kwa
kumwezesha kurejea katika Klabu yake hiyo ya zamani ambaye amesema ni
kama Nyumbani kutokana na mapenzi aliyonayo. Mshambuliaji
huyo pia amewataka mashabiki wake kuendelea kumuunga mkono na anaimani
kuwa atafanya vizuri katika Klabu hiyo ambayo amewahi kuichezea huko
nyuma.