Timu ya taifa ya Cameroon imefanikiwa kupata kocha mpya Volker
Finke kuwa kocha mkuu wa timu hiyo huku kibarua chake cha kwanza Mjerumani huyo ni kuhakikisha timu hiyo inafuzu michuano ya
Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil. Finke
anachukua nafasi ya kocha wa muda wa timu hiyo Jean-Paul Akono ambaye
aliwekwa hapo kuziba nafasi ya Denis Lavagne Septemba mwaka jana baada
ya Mfaransa huyo kushindwa kuisaidia timu hiyo kufuzu michuano ya
Mataifa ya Afrika 2012 na 2013. Kocha
huyo mwenye umri wa miaka 65 aliwahi kuifundisha klabu ya SC Freiburg
kuanzia mwak 1991 mpaka 2007 na atakuwa anafundisha kikosi cha timu ya
taifa kwa mara ya kwanza baada ya kutemwa na timu ya Urawa Red Diamonds
ya Japan na timu ya Cologne ya nchini kwake. Katika
mechi za kufuzu Kombe la Dunia, Cameroon wako kileleni mwa kundi I
wakiwa na alama sita katika mechi tatu walizocheza wakifuatiwa na Libya
wenye alama tano, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo-DRC alama nne na Togo
alama moja. Kazi
yake ya kwanza Finke itakuwa ni kukiongoza kikosi cha timu ya taifa ya
nchi hiyo katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Ukraine utakaochezwa jijini
Kiev Juni 2 mwaka huu kabla ya kuhamishia nguvu zao katika mechi za
kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Togo Juni 9, DRC Juni 16 na Libya
Septemba 6 mwaka huu