Sunday, July 21, 2013

KIPA MARK MPYA WA CHELSEA AWEKA WAZI KUPIGANIA NAMBA NDANI YA CLUB HIYO"

Golikipa mkongwe aliyenaswa na club ya Chelsea katika kipindi cha usajili wa majira ya kiangazi, Mark Schwarzer ameibuka na kudai kuwa anapigania kupata namba katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo msimu ujao. Akihojiwa na waandishi wa habari katika ziara ya kujiandaa na msimu mpya ya klabu hiyo jijini Kuala Lumpur, Malaysia, Schwarzer amesema wakati akisajiliwa na timu hiyo alijua kwamba wana makipa bora na mpambano wa kutafuta nafasi ya kuanza utakuwa mgumu. Lakini alidai kuwa kwa juhudi na kiwango kizuri atakachoonyesha ana matumaini anaweza kupangwa katika kikosi cha kwanza timu hiyo msimu ujao. 
Meneja wa Chelsea Jose Mourinho amesema wiki iliyopita kuwa Schwarzer ataleta ushindani na hamasa kwa golikipa namba moja wa klabu hiyo Petr Cech baada ya kufanya usajili huo wa kushangaza. Schwarzer ambaye amecheza katika Ligi Kuu nchini Uingereza kwa zaidi ya miaka 15 ni mmoja ya wachezaji wachache waliocheza mechi zaidi ya 500 katika historia ya ligi hiyo.