WALIMU wa michezo katika shule za msingi, sekondari na vyuo
wametakiwa kuhamasisha suala la nidhamu kwa wanafunzi ili kuwajengea msingi
ilio bora utakaowafanya wafike mbali.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Tabora, Joyce
Ndonda, aliyekuwa mgeni rasmi katika bonanza maalumu la mchezo wa netiboli,
lililofanyika kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini humo.
Akizungumza na wanamichezo mbalimbali walioshiriki katika
bonanza hilo, Ndonda ameipongeza Chaneta Tabora kwa kuanzisha bonanza hilo na
kuwataka kuendelea na utaratibu huo, kwani ni chachu ya kukuza vipaji kwa
vijana na kuinua hamasa ya michezo.
Aidha kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Mkoa wa
Tabora, Kulwa Kavula, amesema lengo la bonanza hilo ni kuhamasisha wasichana na
wadau wengine kuupenda mchezo huo.
Hata hivyo amewaomba wadau katika halmashauri zote za Mkoa wa
Tabora kuwapa ushirikiano ili waweze kufanikisha harakati za kuinua michezo huo
nchini.