
Ligi ya Mabingwa wa Mikoa kutafuta timu tatu zitakazopanda kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao chini ya usimamizi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itaanza Mei 12 mwaka huu.
Mwisho wa mikoa kuwasilisha
majina ya mabingwa wao ni Mei 1 mwaka huu wakati ratiba ya ligi hiyo itapangwa
mbele ya waandishi wa habari Mei 3 mwaka huu kwenye ofisi za TFF.
Uwasilishaji wa jina la bingwa
wa mkoa unatakiwa kufanyika pamoja na ulipaji ada ya ushiriki ambayo ni sh.
100,000. Mfumo wa ligi hiyo ni bingwa wa mkoa X kucheza na bingwa wa mkoa Y
nyumbani na ugenini ambapo mshindi ndiye anayesonga mbele katika hatua
inayofuata.
Usajili wa wachezaji wa timu
hizo ni uleule uliofanyika katika hatua ya mkoa na unatakiwa kuwasilishwa TFF
kwa ajili ya uthibitisho. TFF inapenda kusisitiza kuwa hakuna usajili mpya wa
wachezaji kwa ajili ya ligi hiyo.
KILA LA KHERI AZAM FC
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) linaitakia kila la kheri timu ya Azam FC katika mechi yake ya
kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho dhidi ya AS FAR Rabat ya
Morocco itakayochezwa kesho (Aprili 20 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Azam FC ina fursa nzuri ya
kufanya vizuri kwenye mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Emile Fred kutoka
Shelisheli kutokana na maandalizi iliyofanya, lakini vilevile tunatoa mwito kwa
Watanzania kujitokeza kwa wingi uwanjani kuiunga mkono.
Makocha wasaidizi wa timu zote
mbili, Kalimangonga Ongala wa Azam na Lahcen Ouadani wa AS FAR Rabat
wamezungumza na waandishi wa habari kuhusu mechi hiyo, kuwa wamejiandaa kuibuka
na ushindi.
Kocha Ongala amesema wamepata
DVD za mechi tatu za mwisho za AS FAR Rabat, moja ikiwa dhidi ya timu ya Al
Nasir ya Libya ambayo waliitoa katika raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho
na nyingine mbili za ligi ya Morocco ambazo wanazifanyia kazi kuhakikisha
wanashinda kesho.
Naye Ouadani amesema
hawaifahamu vizuri Azam, lakini wanaujua mpira wa Tanzania baada ya kuangalia
mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Morocco
(Lions of the Atlas) iliyochezwa jijini Dar es Salaam Machi 24 mwaka huu na
Stars kushinda mabao 3-1.
Baadhi ya wachezaji ambao Azam
inatarajia kuwatumia kwenye mechi ya kesho ni pamoja na Aishi Manula, Mwadini
Ally, Khamis Mcha, John Bocco na Salum Abubakar ambao pia wamo kwenye kikosi
cha sasa cha Taifa Stars kilicho chini ya kocha Kim Poulsen.
AS FAR Rabat ina wachezaji sita
kwenye timu ya Taifa ya Morocco. Wachezaji hao ni mabeki Younes Bellakhdar,
Abderrahim Achchakir, Younnes Hammal, na viungo Salaheddine Said, Salaheddine
Aqqal na Youssef Kaddioui.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF)