Friday, April 18, 2014

PAZIA VPL LAFUNGWA, AZAM KUKABIDHIWA KOMBE CHAMAZI

Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inafikia tamati kesho (Aprili 19 mwaka huu) kwa timu zote 14 kuwa viwanjani, huku mabingwa wapya Azam wakikabidhiwa kombe lao Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam katika mechi yao dhidi ya JKT Ruvu.

Mechi zote saba zitachezwa kuanzia saa 10 kamili jioni ambapo Yanga na Simba zitakuwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa mechi ambayo viingilio vyake ni sh. 7,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 10,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 20,000 kwa VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 30,000.

Tayari tiketi zimeanza kuuzwa leo (Aprili 18 mwaka huu) katika vituo saba vya; Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Kariakoo (Kidongo Chekundu), Buguruni Shell, mgahawa wa Steers uliopo Mtaa wa Ohio na Samora, Ubungo OilCom, Dar Live Mbagala na Uwanja wa Taifa.

Mechi nyingine zitakuwa kati ya Tanzania Prisons na Ashanti United (Uwanja wa Jamhuri, Morogoro), Rhino Rangers na Ruvu Shooting (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora), Mbeya City na Mgambo Shooting (Uwanja wa Sokoine, Mbeya), Oljoro JKT na Mtibwa Sugar (Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha) na Coastal Union na Kagera Sugar (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga).
MSIMAMO:
NA
TIMU
P
W
D
L
F
A
GD
PTS
1 
Azam FC
25
17
8
0
50
15
35
59
2 
Young Africans
25
16
7
2
60
18
42
55
3
Mbeya City
25
12
10
3
32
20
12
46
4
Simba SC
25
9
10
6
40
26
14
37
5
Kagera Sugar
25
8
11
6
22
20
2
35
6
Ruvu Shooting
25
9
8
8
26
32
-6
35
7
JKT Ruvu
25
10
1
14
23
39
-16
31
8
Mtibwa Sugar
25
7
9
9
29
30
-1
30
9
Coastal Union
25
6
11
8
16
19
-3
29
10
Mgambo JKT
25
6
8
11
18
34
-16
26
11
Tanzania Prisons
25
5
10
10
25
33
-8
25
12
Ashanti United
25
6
7
12
20
38
-18
25
13
JKT Oljoro
25
3
9
13
18
36
-18
18
14
Rhino Rangers
25
3
7
15
18
37
-19
16
MICHUANO YA BEACH SOCCER KUANZA JUMAPILI
Michuano ya mpira wa miguu ya ufukweni (Beach Soccer) inazinduliwa rasmi keshokutwa (Aprili 20 mwaka huu) kwenye ufukwe wa Escape One uliopo Mikocheni, Dar es Salaam na kushirikisha timu 13.

Uzinduzi huo utaanza saa 5 asubuhi na mechi zitachezwa hadi saa 11 jioni. Michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya kwanza nchini inashirikisha timu 13 kutoka vyuo mbalimbali vya jijini Dar es Salaam.

Vyuo hivyo ni Chuo Kikuu cha Ardhi (AU), Chuo Kikuu cha St. Joseph Tanzania (SJUIT), Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (TUDARCO), Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW), Chuo cha Uandishi wa Habari Dar es Salaam (DSJ) na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

Vingine ni Chuo cha Utumishi wa Umma Magogoni, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Chuo cha Utawala wa Kodi (ITA) na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Michuano hiyo itakuwa inachezwa Jumamosi na Jumapili kwenye fukwe za Escape One na Gorilla Beach iliyopo Kigamboni, Dar es Salaam.

WAZOEFU TAIFA STARS KUTAJWA KESHO
Wachezaji wazoefu wa Taifa Stars watakaoungana na wale 16 waliopatikana katika mpango wa maboresho wa timu hiyo watatangazwa kesho (Aprili 19 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itapiga kambi kwenye hoteli ya Kunduchi Beach kujiandaa kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Burundi itakayochezwa Aprili 26 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wachezaji waliopatikana katika mpango wa maboresho ya Stars wanatarajiwa kuwasili leo (Aprili 18 mwaka huu), na kwenda moja kwa moja kambini kuwasubiri wenzao watakaotajwa kesho (Aprili 19 mwaka huu).

Wachezaji hao ni kipa Benedicto Tinoko Simwanda (Mara), Emma Namwondo Simwanda (Temeke), Joram Nason Mgeveje (Iringa), Omari Ally Kindamba (Temeke), Edward Peter Mayunga (Kaskazini Pemba), Shiraz Abdallah Sozigwa (Ilala), Yusuf Suleiman Mlipili (Temeke) na Said Juma Ally (Mjini Magharibi).

Wengine ni Abubakar Ally Mohamed (Kusini Unguja), Hashim Ramadhan Magona (Shinyanga), Omari Athumani Nyenje (Mtwara), Chunga Said Zito (Manyara), Mohammed Seif Saidi (Kusini Pemba), Ayoub Kasim Lipati (Ilala), Abdurahman Othman Ally (Mjini Magharibi) na Paul Michael Bundara (Ilala).

BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

Thursday, April 17, 2014

WACHEZAJI MABORESHO TAIFA STARS 16 WATAJWA

WACHEZAJI MABORESHO STARS WATAJWA
Kocha Msaidizi wa Taifa Stars, Salum Mayanga ametangaza majina ya wachezaji 16 waliochaguliwa katika maboresho ya timu ya Taifa Taifa Stars kwenye hoteli ya Hill View jijini Mbeya.
TFF_LOGO12Wachezaji hao ni kipa Benedicto Tinoko Simwanda (Temeke), mabeki wa kati; Emma Namwondo Simwanda (Temeke) na Joram Nason Mgeveje (Iringa). Walinzi wa pembeni ni Omari Ally Kindamba (Temeke), Edward Peter Mayunga (Kaskazini Pemba) na Shiraz Abdallah Sozigwa (Ilala).
Viungo ni Yusuf Suleiman Mlipili (Temeke), Said Juma Ally (Mjini Magharibi), Abubakar Ally Mohamed (Kusini Unguja), Hashim Ramadhan Magona (Shinyanga), Omari Athumani Nyenje (Mtwara) na Chunga Said Zito (Manyara).
Washambuliaji ni Mohammed Seif Saidi (Kusini Pemba), Ayoub Kasim Lipati (Ilala), Abdurahman Othman Ally (Mjini Magharibi), Paul Michael Bundara (Ilala). Wachezaji wa U 20 ni Mbwana Mshindo Musa (Tanga) na Bayaga Atanas Fabian (Mbeya).
Alisema mpango huu wa kuboresha timu ya Taifa ambayo inadhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ni endelevu na kusisitiza kuwa hata wale 18 walioachwa watafuatiliwa na TFF na kuitwa panapokuwa na mahitaji.
“Hawa wote wapo kwenye database ya TFF na hawataachwa tu hivi hivi wapotee,” alisema kocha Mayanga.
Wachezaji ha0 waliingia kambini mjini Tukuyu, Machi 21 mwaka huu na wamefanya mazoezi kwa pamoja kwa karibu wiki nne sasa kabla ya kuchujwa.
Wachezaji 16 waliochaguliwa wanatarajiwa kuondoka Tukuyu kesho (Aprili 18 mwaka huu) na kwenda kwenye kambi ya Taifa Stars katika Hoteli ya Kunduchi ambapo wataungana na wachezaji wa Taifa Stars wa siku zote.
Baadaye watachujwa tena ili ipatikane timu moja ya Taifa iliyoboreshwa.
Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjro Premium Lager inaunga mkono utaratibu huu wa maboresho ya Taifa na imewekeza zaidi ya dola milioni 2 kwa mwaka kudhamini Taifa Stars. Huu ndio udhamini mkubwa zaidi ambao Stars imewahi kupata tangu kuanzishwa kwa TFF.
LIGI YA MABINGWA WA MIKOA KUANZA MEI 10
Michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) itakayochezwa kwa ligi ya mkondo mmoja katika vituo vitatu vya timu tisa kila kimoja inatarajia kuanza Mei 10 mwaka huu.
Timu ya kwanza kutoka katika kila kituo ndiyo itakayopanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2014/2015. Kwa vile ligi hii haina mdhamini, hivyo timu zitajigharamia kwa kila kitu.
Vituo vitakavyotumika kwa ajili ya RCL, kanuni pamoja na ratiba vitatangazwa kabla ya kuanza kwa ligi hiyo. Pia kituo kitakachoteuliwa kwa ajili ya ligi hiyo, timu yake haitapangwa katika kituo husika ikiwa ni moja ya njia ya kuhakikisha kanuni ya mchezo wa kiungwana (fair play) inazingatiwa.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

Tuesday, April 15, 2014

DRFA YAIPA HONGERA AZAM FC KUTWAA UBINGWA

CHAMA Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kimeipongeza timu ya Azam FC kwa kufanikiwa kwa mara ya kwanza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2013/2014.

Azam FC ili

jihakikishia kutwaa ubingwa huo Jumapili baada ya kuifunga timu ya Mbeya City mabao 2-1 katika mchezo wa ligi hiyo uliochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine.

Ofisa Habari wa DRFA Mohamed Mharizo alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa ubingwa huo wa Azam ni kielelzo cha kujituma kwao na kuwa na ushirikiano na walistahili kutwaa taji hilo.

“Kwa niaba ya DRFA nachukua fursa hii kuwapongeza wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa timu ya Azam FC kwa ujumla, kwa kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Ni imani yetu DRFA kuwa timu hiyo itawakilisha vyema nchi katika michuano ya Klabu Bingwa barani Afrika, tunawatakia kila la kheri katika michuano hiyo.
“Lakini pia tunaipongeza Yanga kwa kushika nafasi ya pili katika ligi hiyo, nao tunawatakia kila la kheri katika michuano ya Kombe la Shirikisho. Sisi Mkoa tunafarijika sana kuona timu zetu za Mkoa wa Dar es Salaam zinavyofanya vizuri,” alisema.

Monday, April 14, 2014

KATIBU MKUU FIFA JEROME VALCKE KUFUNGUA SEMINA DAR

KATIBU MKUU WA FIFA KUFUNGUA SEMINA DAR

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Jerome Valcke atawasili nchini Mei 1 mwaka huu ambapo atafungua semina ya mawasiliano itakayoshirikisha viongozi wa vyama wanachama wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Akizungumza Dar es Salaam leo (Aprili 14 mwaka huu), Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amesema Valcke ambaye hii ni mara yake ya kwanza kuja Tanzania atafuatana na maofisa wengine wa saba wa FIFA.
Amesema semina hiyo iliyoandaliwa na FIFA itafanyika kwa siku mbili (Mei 1 na 2 mwaka huu) ambapo vilevile Valcke atapata fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari wa ndani na wa kimataifa.
TFF_LOGO12Rais Malinzi amesema washiriki wa semina hiyo ni marais, makatibu wakuu na wakuu wa mawasiliano wa wanachama 12 wa CECAFA ambao ni Burundi, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somali, Sudan, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda.
Naye Mwenyekiti wa CECAFA, Leodegar Tenga ambaye alifuatana na Katibu Mkuu wake Nicholas Musonye amemshukuru Rais wa TFF kwa kukubali kuwa mwenyeji wa semina hiyo kwani itasaidia katika maendeleo ya mpira wa miguu katika ukanda huu.
RAMBIRAMBI MSIBA WA JOSEPHAT MAGAZI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu (FRAT) Mkoa wa Singida, Josephat Magazi kilichotokea jana mkoani Kilimanjaro.
Magazi ambaye pia aliwahi kuwa mwamuzi na kamishna wa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) alikuwa amelazwa katika Hospitali ya KCMC. Mazishi yatafanyika kesho (Aprili 15 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwao Ushirombo mkoani Shinyanga.
Msiba huo ni mkubwa katika fani ya mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Magazi alishirikiana na TFF na wadau wengine wa mpira wa miguu katika masuala ya uamuzi na uongozi, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Magazi, FRAT na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (SHIREFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)