WAZIRI Mkuu Msaidizi wa Libya Awad Ibrahim Elbarasi amesema serikali ya nchi hiyo imepanga kuwekeza kiasi cha dola milioni 314 kwa ajili ya ujenzi wa viwanja mwaka huu ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya michuano ya Mataifa ya Afrika 2017 kwa mategemeo kwamba michuano hiyo itawaunganisha wananchi baada ya vita ya mwaka 2011. Elbarasi amesema kama ilivyokuwa kwa Nelson Mandela alivyofanya nchini Afrika Kusini ni mategemeo yao wataiunganisha Libya kwa kutumia michuano hiyo. Waziri huyo aliendelea kusema kuwa ujenzi kwa ajili ya viwanja hivyo vipatavyo 11 unatarajiwa kuanza Juni mwaka huu na tayari fedha hizo zimekwishaombwa serikalini. Mwezi uliopita Libya ilidai kuwa itatumia rasilimali zake zote kuhakikisha wanalinda haki yao ya kuandaa michuano ya 2017 baada ya kushindwa kuandaa michuano ya Afrika ya mwaka huu na vita.
BARCELONA USO KWA USO NA NEYMA
KLABU ya arcelona imeonekana kukaribia kumnyakuwa nyota wa klabu ya Santos, Neymar baada ya klabu hiyo kupanga kuanza kufanya mazungumzo naye Julai mwaka huu. Neymar mwenye umri wa miaka 21 amekuwa akisisitiza kuwa anataka kubakia katika klabu yake ya Santos mpaka baada ya michuano ya Kombe la Dunia 2014 lakini amekuwa akipata ushauri kutoka kwa watu mbalimbali kwamba atapata uzoefu wa kutosha barani Ulaya kama akienda mapema. Wachezaji wa Barcelona ambao ni raia wa Brazil, Dani Alves na Adriano wamekuwa wakimshauri nyota huyo kufanya uamuzi sahihi kwa kujiunga na klabu hiyo hivyo kuongeza chachu ya nyota kumwaga wino hapo. Neymar ambaye atakuwa sehemu ya kikosi cha Brazil kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Shirikisho itakayofanyika Juni mwaka huu atasafiri kwenda Hispania muda mfupi baada ya kumalizika kwa michuano hiyo ili kuzungumzia mustabali wake.
FUFA KATIKA MCHAKATO WA KOCHA MPYA
SHIRIKISHO la Soka nchini Uganda-FUFA limesema kuwa lina uhakika wa timu ya taifa ya nchi hiyo kupata kocha mpya kabla ya mechi zao mbili za kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2014 dhidi ya Liberia na Angola zitakazochezwa Juni mwaka huu. Nafasi ya kocha wa nchi hiyo maarufu kama The Cranes ilibakia wazi baada ya Bobby Williamson kutimuliwa wiki iliyopita. Ofisa Habari wa FUFA amesema ni matumaini yao kocha mpya atapatikana kabla ya mechi yao dhidi ya Liberia na anaamini hilo litatokea. Makocha mbalimbali wametuma maombi yao ya kutaka kibarua cha kuinoa The Cranes wakiwemo Dario Bonetti wa Italia, Nikola Kavazovic wa Serbia na Tom Sainfeit wa Ubelgiji ambaye pia amewahi kuinoa Yanga ya Dar es Salaam.
MICHO ASEMA RWANDA ITABAKI MAISHANI MWANGU"
ALIYEKUWA kocha wa timu ya taifa ya Rwanda, Milutin Sredojevic ‘Micho’ ametanabaisha kuwa Rwanda itabakia kuwa sehemu muhimu katika maisha yake pamoja na kutimuliwa kibarua chake jana. Shirikisho la Soka la nchi hiyo-Ferwafa jana lilitangaza kukatisha mkataba na kocha huyo kutokana na matokeo yasiyo yakuridhisha ambayo timu hiyo imekuwa ikiyapata. Hivi sasa Micho mwenye umri wa miaka 43 ambaye mkataba wake ulikuwa umelizike Octoba mwaka huu anafanya kazi na washauri wake wa kisheria pamoja na Ferwafa kuangalia jinsi ya kulipwa stahiki zake. Lakini Micho alisisitiza kuwa pamoja na kutoa hayo lakini soka la nchi hiyo wananchi wake pamoja na watu wote aliofanya nao kazi watabakia sehemu muhimu katika maisha akiwa hapo kuanzia mwaka 2011 alipochukua mikoba ya Sellas Tetteh.