Saturday, April 5, 2014

TAIFA STARS, BURUNDI KUCHEZA APRILI 26

Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itacheza mechi ya kirafiki na Burundi (Intamba Mu Rugamba) Aprili 26 mwaka huu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager tayari ipo kambini Tukuyu mkoani Mbeya ikijiandaa kwa ajili ya mechi hiyo ikiwa na wachezaji waliopatikana katika programu maalumu ya kusaka vipaji.
Baadaye wachezaji wengine wa Taifa Stars ambao wapo nje ya programu ya kusaka vipaji wataungana na wenzao kabla ya kutengeneza kikosi cha mwisho kitakachoivaa Burundi.
Mechi hiyo itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itachezeshwa na waamuzi wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kutoka nchini Kenya.
TIMU YA WATOTO WA MITAANI YACHACHAFYA BRAZIL
Timu ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania imefanikiwa kuingia nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Dunia yanayofanyika Rio de Janeiro nchini Brazil baada ya jana kuifunga Indonesia kwa jumla ya mabao 5-3.
STREET_CHILD
Hadi muda wa kawaida wa mchezo huo unamalizika timu hizo zilikuwa zimefungana mabao 2-2 ndipo ikatumia mikwaju ya penalti kuamua mshindi. Tanzania ilipata penalti tatu dhidi ya moja ya wapinzani wao.
Kwa matokeo hayo, Tanzania sasa itacheza mechi ya nusu fainali leo dhidi ya Marekani ili kupata timu zitakazocheza mechi za fainali na kutafuta mshindi wa tatu. Mechi za fainali na kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa kesho (Aprili 6 mwaka huu).
Timu nyingine zilizoingia nusu fainali na mechi zake zinachezwa leo (Aprili 5 mwaka huu) ni Burundi itakayocheza na Pakistan.
Katika mechi zilizopita, Tanzania ilitoka sare ya mabao 2-2 na Burundi, ikaitandika Argentina mabao 3-0 ikailaza Nicaragua mabao 2-0 na ikafungwa na Philippines mabao 2-0.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

Friday, April 4, 2014

WAZEE WA JANGWANI YAMKATIA RUFAA MCHEZAJI WA JKT MGAMBO.

Mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania bara yanga sc imekata rufaa dhidi ya mchezaji Mohammed Neto wa Mgambo Shooting ikidai anacheza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kinyume cha kanuni za usajili.
Yanga SC wanalalamikia usajili wa mchezaji huyo una mapungufu kwa kuwa ni raia wa kigeni, lakini hana Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC).
Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Evodius Mtawala amekiri kupokea rufaa ya Yanga SC, lakini hakuwa tayari kuzungumza zaidi. “Ndiyo tumepokea, ila nipo kwenye kikao siwezi kuzungumza zaidi,”alisema Mtawala, anayekaimu nafasi ya Celestine Mwesigwa aliye Afrika Kusini kwa sasa.
Dhamira ya Yanga SC kutaka rufaa hiyo inaweza kuwa kukomboa pointi walizopoteza kwa Mgambo JKT Jumapili iliyopita kwa kufungwa mabao 2-1 Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga katika mchezo wa Ligi Kuu.
Lakini kwa mujibu wa kanuni za sasa za Ligi Kuu, baada ya usajili hutolewa muda maalum wa pingamizi kwa wachezaji na anapopitishwa hata ikikatwa rufaa, haibadili matokeo zaidi mchezaji au kiongozi aliyefanya udanganyifu kuchukuliwa hatua.
Lakini pia katika utaratibu wa sasa wa usajili, kila mchezaji mpya katika Ligi Kuu anatakiwa kuwasilisha ama cheti cha kuzaliwa au hati ya kusafiria- ambavyo pamoja na kusaidia umri wa mchezaji kujulikana pia huainisha uraia wake.
Neto alicheza kwa dakika 30 tu mechi dhidi ya Yanga baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu. Alipewa kakadi ya njano ya kwanza akikataa kukaguliwa na refa Alex Mahagi na ya pili kwa kuzozana na refa huyo akipinga kusachiwa kama amebeba hirizi.
Yanga SC inahaha kuhakikisha inafufua matumaini ya kutetea ubingwa wake na sasa inahamishia nguvu zake mezani, baada ya mambo kuwaendea kombo uwanjani na kuachwa na Azam FC katika mbio hizo.
Azam FC inaongoza kwa pointi zake 53 baada ya kucheza mechi 23, ikifuatiwa na Yanga SC yenye pointi 46 za mechi 22 na Mbeya City yenye pointi 45 za mechi 23 ni ya tatu.

VPL:SIMBA KUIVAA KAGERA SUGAR,MBEYA CITY VS ASHANTI UNITED.

Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaingia raundi ya 24 kesho (Aprili 5 mwaka huu) kwa mechi mbili ambapo Kagera Sugar itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Mechi nyingine itakuwa kati ya Mbeya City ambayo itakuwa mgeni wa Ashanti United kwenye Uwanja wa A

zam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam. Ashanti United inayofundishwa na Abdallah Kibaden ipo katika mkakati wa kukwepa kushuka daraja.
Keshokutwa (Aprili 6 mwaka huu) kutakuwa na mechi kati ya Coastal na Mgambo Shooting Stars (Mkwakwani, Tanga), Oljoro JKT na Tanzania Prisons (Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), Rhino Rangers na Mtibwa Sugar (Ali Hassan Mwinyi, Tabora) na Yanga dhidi ya JKT Ruvu (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam).

Raundi hiyo itakamilika Aprili 9 mwaka huu kwa mechi kati ya Ruvu Shooting na Azam itakayochezwa Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
 
NI MWADUI AU STAND UNITED VPL MSIMU UJAO
Ni ipi kati ya timu za Mwadui na Stand United, zote za Shinyanga itakayocheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao itajulikana kesho (Aprili 5 mwaka huu) baada ya kundi C kuhitimisha mechi za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu huu.
Mwadui yenye pointi 28 ndiyo inayoongoza, na itacheza na Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma. Nayo Stand United yenye pointi 26 itaikaribisha Toto Africans kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.tff_LOGO1

Mechi nyingine zitakuwa kati ya Pamba na Kanembwa JKT itakayochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wakati Polisi Mara na Polisi Tabora zitakwaruzana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.
Timu ambazo tayari zimepanda daraja kutoka FDL kucheza VPL msimu ujao ni Ndanda SC kutoka kundi A na Polisi Morogoro ya kundi B.

21 ZA KUCHEZA RCL ZAJULIKANA
Timu 21 kati ya 27 zitakazocheza Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kutafuta tiketi ya kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao tayari zimejulikana.
Timu hizo ni Abajalo SC (Dar es Salaam), AFC (Arusha), African Sports (Tanga), Bulyanhulu FC (Shinyanga), Geita Veterans (Geita), JKT Mafinga (Iringa), JKT Rwamukoma (Mara), Kariakoo SC (Lindi), Kiluvya United (Pwani), Milambo SC (Tabora) na Mshikamano FC (Dar es Salaam).
Nyingine ni Mvuvumwa FC (Kigoma), Navy SC (Dar es Salaam), Njombe Mji (Njombe), Pachoto Shooting Stars (Mtwara), Panone FC (Kilimanjaro), Singida United (Singida), Tanzanite (Manyara), Town Small Boys (Ruvuma), Ujenzi FC (Rukwa) na Volcano (Morogoro).
WATANO WAFANYA MTIHANI WA UWAKALA WA WACHEZAJI
Watanzania watano wamefanya mtihani wa uwakala wa wachezaji wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambao ulifanyika jana (Aprili 3 mwaka huu) duniani kote.
Watahiniwa katika mtihani huo ambao ulikuwa na maswali kutoka FIFA na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) walikuwa Godlisten Anderson, Jesse Koka, Lutfi Binkleb, Rwechungura Mutahaba na Silla Yalonde.