Mbaspo
walianza mbio zao za kutwaa ubingwa kwa kutoshana nguvu ya 3-3 dhidi ya
Mbosa siku ya Jumatatu Juni 24 kabla ya kufanya mauaji makubwa ya 6-0
dhidi ya timu dhaifu ya Mbeya Sekondari siku ya Jumanne. Michezo yote
imefanyika kwenye uwanja wa Magereza jijini Mbeya.
Mbosa
walifikisha point nne juzi Jumatano walipoitandika Mbeya Sekondari 3-0
hivyo kumaliza wakiwa na point nne na magoli sita wakati wapinzani wao
Mbaspo wakifikisha jumla ya magoli tisa ya kufunga. Katika mechi ya
juzi, magoli ya Mbosa yalitiwa kwenye kamba na Michael Mwashilanga,
Riziki Juma na Julius Landa.
Wakati
huo huo, chama cha mpira wa miguu mkoa wa Mbeya kimetangaza kikosi cha
wachezaji 18 kuuwakilisha mkoa huo kwenye michuano ya Taifa ya Airtel
Rising Stars inayoanza kutimua vumbi kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya
Karume jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 2.
Wachezaji
hao ni Ismail Yesaya, Emmanuel Alex, Gift Sanga, Jackson Mwaibambe,
Boaz Mwangole, Costa Sanga, Seif Zubery, Stanley Angelo, Enock Sikaonga,
Kaunda Malata, Joel Kasimila, Hamprey Nyeo, Elia Salengo, Peter Noah,
Emmaneul Mtimbi, Michael Bosco, Richard Kalinga na Zamoyoni Mwashambwa.
Katika
mkoa wa Morogoro, mji kasoro bahari, timu ya Moro Kids imetoka sare ya
bila kufungana na Techfort katika mchezo wa kushambuliana kwa zamu
uliopigwa kwenye uwanja wa shule ya sekondari ya Morogoro juzi Jumatano
na kushuhudiwa na mashabiki wengi wa mji huo
Airtel
Rising Stars vile vile imeanza kutimua vumbi katika jiji la Mwanza
ambapo timu ya Marsh Athletical imedhihirisha umwambe wake katika soka
baada ya kuifunga Nyamagana United 2-0 kwenye uwanja mkongwe wa
Nyamagana.
Timu
za mikoa zimepangwa kuanza kuwasili jijini Dar es Salaam mwishoni mwa
wiki tayari kwa ajili ya kindumbwe ndumbwe cha Airtel Rising Stars ngazi
ya taifa katika uwanja wa Kumbukumbu ya Karume. Wachezaji 16
watachaguliwa wakati wa mashindano hayo ili kuunda timu
itakayoiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa ya Airtel
Rising Stars. Nchi mwenyeji wa michuano hiyo itatangazwa baadaye mwezi
ujao.