Monday, September 2, 2013

WENGER AFUNJA UKIMYA

KLABU ya Arsenal imekubali kutoa kitita cha paundi milioni 42.4 kwa ajili ya kumsajili kiungo Mesut Ozil kutoka Real Madrid ya Hispania. Ozil mwenye umri wa miaka 24 naye amefikia makubaliano binafsi na klabu hiyo lakini anatakiwa kufanyiwa vipimo vya afya kabla Arsenal hawajakamilisha usajili huo ambao utavunja rekodi ya klabu hiyo. Kwasasa Ozil yuko katika majukumu ya kimataifa hivyo vipimo vya afya atafanyiwa nchini kwao Ujerumani. Arsenal pia wako katika mazungumzo na Chelsea kwa ajili ya kumsajili kwa mkopo mshambuliaji Demba Ba huku wakiwa tayari wamekamilisha usajili mwingine wa mkopo kwa kipa wa Palermo Emiliano Viviano.

ILALA, KASKAZINI UNGUJA ZAANZA COPA KWA SARE

Timu za Ilala na Kaskazini Unguja zimetoka sare ya mabao 3-3 katika moja ya mechi za ufunguzi za michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 iliyoanza leo (Septemba 2 mwaka huu) katika vituo mbalimbali nchini.


Wafungaji wa Ilala katika mechi hiyo iliyochezwa asubuhi Uwanja wa Tamco ulioko Kibaha, Pwani yalifungwa na Ally Shaban (mawili) wakati lingine lilifungwa na Haruni Said. Mabao ya Kaskazini Unguja yalifungwa na Jecha Ally (mawili) na Shehe Ally.


Katika kituo cha Mbeya, Njombe imeanza vizuri baada ya kuifunga Katavi mabao 2-1. Mabao ya washindi yalifungwa na Rackson Mligo dakika ya 13 wakati lingine lilifungwa na Kelvin Gama dakika kumi kabla ya filimbi ya mwisho.


Bao la Katavi katika mechi hiyo iliyochezwa uwanja wa Sekondari ya Iyunga lilifungwa dakika ya 15 kupitia Joseph Edward.


Wenyeji Mbeya wameitandika Ruvuma mabao 3-0 katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Iyunga. Mabao ya washindi yalifungwa na Joel Mwasambungu dakika 9 wakati mengine yalifungwa na Jackson Mwaibambe dakika ya 18 na 55.  


Kesho (Septemba 3 mwaka huu) katika kituo hicho kutakuwa na mechi kati ya Rukwa na Katavi itakayochezwa saa 4 asubuhi wakati Iringa na Ruvuma zitaumana kuanzia saa 2 asubuhi.


Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

HENRY JOSEPH AITWA TAIFA STARS

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen amemjumuisha mchezaji Henry Joseph wa Simba kwenye kikosi chake kinachojiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Gambia itakayochezwa Septemba 7 mwaka huu jijini Banjul.

Tayari Joseph amesharipoti kwenye kambi ya timu hiyo iliyoko hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam. Taifa Stars ambayo iko chini ya udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager imeingia kambini tangu Agosti 29 mwaka huu, na leo jioni itafanya mazoezi yake kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.

Programu ya timu hiyo inaonesha kuwa kesho (Septemba 3 mwaka huu) itafanya mazoezi yake asubuhi na jioni kwenye uwanja huo huo wa Kumbukumbu ya Karume.

Wakati huo huo, kesho (Septemba 3 mwaka huu) saa 6 kamili mchana Kocha Kim Poulsen atakuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari.

LIUNDA KUTATHMINI WAAMUZI CL
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Leslie Liunda wa Tanzania kuwa mtathmini wa waamuzi kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Coton Sport ya Cameroon na Esperance ya Tunisia.

Mechi hiyo ya kundi B itachezwa Septemba 21 mwaka huu kwenye Uwanja wa Omnisport Roumdeadjia mjini Garoua, Cameroon. Kamishna atakuwa Bema Doumbia wa Ivory Coast.

Waamuzi wanatoka Madagascar wakiongozwa na Hamada Nampiandraza. Wasaidizi wake ni Jean Eric Pierre Andrivoavonjy, Ferdinand Velomanana Linoro na Bruno Marie Andrimiharisia.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)