
Februari 6, 2014
Wachezaji tisa wa Kanembwa JKT pamoja na
timu yao wanaolalamikiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
kwa kumpiga mwamuzi Peter Mujaya wanatakiwa kujitetea mbele ya Kamati
ya Nidhamu itakayokutana Jumapili (Februari 9 mwaka huu).
Utetezi huo unaweza kuwa wa mdomo kwa
walalamikiwa kufika wenyewe mbele ya kamati itakayokutana saa 4 kamili
asubuhi au kuuwasilisha kwa njia ya maandishi.
Kamati ilikutana jana Jumatano (Februari
5 mwaka huu) kusikiliza malalamiko dhidi ya wachezaji hao na timu yao
kwa tukio hilo lililotokea Novemba 2 mwaka jana kwenye mechi ya Ligi
Daraja la Kwanza (FDL) dhidi ya Stand United FC iliyochezwa Uwanja wa
Kambarage mjini Shinyanga.
Wachezaji hao ni Abdallah Mgonja, Bariki
Abdul, Philipo Ndonde, Mbeke Mbeke, Mkuba Clement, Mrisho Mussa, Nteze
Raymond, Ntilakigwa Hussein na Uhuru Mwambungu. Mlalamikiwa mwingine
ambaye naye anatakiwa kujitetea ni timu ya Kanembwa JKT.
Ikiwa chini ya Mwenyekiti wake Tarimba
Abbas, Kamati hiyo baada ya kusikiliza malalamiko dhidi ya wahusika na
kupokea ushahidi wa aina mbalimbali kutoka kwa mlalamikaji imesema ili
iweze kutenda haki katika shauri hilo ni lazima walalamikiwa wapate
fursa ya kusikilizwa.
Katika hatua nyingine, Kamati hiyo
iliyokutana kwa mara ya kwanza tangu ilipoundwa imesema imesikitishwa na
vitendo vya fujo ndani ya mpira wa miguu, na kuwataka watu
wasijihusishe na aina yoyote ya fujo.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)