Kikosi cha Taifa Stars ambacho jana (Juni 1 mwaka
huu) kiliitupa Zimbabwe (Mighty Warriors) nje ya michuano ya Afrika baada ya
kutoka sare ya mabao 2-2 kinarejea nchini leo (Juni 2 mwaka huu) kutoka Harare.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium
Lager itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar
es Salaam saa 12.30 jioni kwa ndege ya Kenya Airways ikitokea Harare kupitia
Nairobi.
Stars imefuzu kucheza raundi inayofuata kwa
ushindi wa jumla ya mabao 3-2, kwani awali (Mei 18 mwaka huu) iliifunga
Zimbabwe bao 1-0 katika mechi ya kwanza iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Katika raundi ya pili, Taifa Stars itacheza na
Msumbiji ambapo itaanzia nyumbani kati ya Julai 19 na 20 mwaka huu, wakati
mechi ya marudiano itafanyika Msumbiji kati ya Agosti 2 na 3 mwaka huu.
Wakati huo huo, Taifa Stars imeendelea kupokea
salamu za pongezi kutoka kwa wadau mbalimbali baada ya kufanikiwa kuvuka
kikwazo hicho cha kwanza katika harakati zake za kucheza Fainali za Afrika
zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.
Salamu hizo zimetoka kwa Chama cha Mpira wa Miguu
Mkoa wa Mbeya (MREFA), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Manyara (MARFA), mjumbe
wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) akiwakilisha
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA), John Kadutu, na mjumbe wa
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Ahmed Idd
Mgoyi.
U15 TANZANIA YATUA MEDALI VIFUANI
Timu ya Tanzania ya wachezaji wenye umri chini ya
miaka 15 iliyoshika nafasi ya pili katika Michezo ya Afrika kwa Vijana (AYG)
iliyofanyika Gaborone, Botswana inawasili leo (Juni 2 mwaka huu) jijini Dar es
Salaam.
U15 ambayo imeshinda mechi tatu, sare moja na
kufungwa moja inawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)
saa 12.30 jioni kwa ndege ya Kenya Airways ikitokea Gaborone kupitia Nairobi.
Tanzania ambayo imepata medali za fedha kwa
kushika nafasi hiyo ikiwa chini yaKocha Abel Mtweve ilizifunga Afrika Kusini
2-0, Botswana 2-0, Swaziland 3-0 na ikatoka sare ya bao 1-1 na Mali. Ilifungwa
mabao 2-0 na Nigeria ambao ndiyo walioibuka mabingwa.
Wachezaji 16 waliounda kikosi cha Tanzania ni
Adam Shayo, Amani Ally, Amos Manguli, Amri Nyuki, Amede Amani, Baraka Rashid,
David Uromi, Goodlove Mdumule, Hance Msonga, Kelvin Kamalamo, Makalius Amrin,
Nasson Chanuka, Paulo Ngowi, Petro Shaban, Rajab Mohamed na Thomas Chindeka.